26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

FAMILIA ZA WALIOUAWA NA ASKARI SUMA JKT ZAJA JUU

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

FAMILIA ya marehemu Julius Kilusu (45), imeiomba Serikali kuhakikisha haki inatendeka kwa kufikishwa katika vyombo vya sheria askari wa Suma JKT waliohusika katika mauaji ya ndugu yao pamoja na kuilipa fidia familia yake ya wake watatu na watoto 12 aliyoiacha.

Kilio hicho kilitolewa jana na baadhi ya ndugu wa Kilusu aliyeuawa na askari wa Suma JKT juzi, wakati walipokuwa wakiaga mwili wake nje ya chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mt. Meru.

Kilusu alizikwa jana katika Kijiji cha Ngipitali, Kata ya Oldonyosambu, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Wakizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo baadhi ya ndugu wa marehemu; Yusuph Lialo, Mosses Ngaluma na Sanare Siboku, waliiomba Serikali iwafikishe katika vyombo vya kisheria wahusika wote wa tukio hilo.

Lialo alieleza kuwa ndugu yake alikuwa ni mkulima na mfanyabiashara na kwamba wakati mauti yanamkuta hakuwa akijihusisha na ufugaji.

Alisema hata siku ya tukio alipigwa risasi shambani kwake eneo la Tanzania Maua umbali wa zaidi ya kilomita 7 kutoka eneo la shamba hilo la Serikali, wakati akiendelea na shughuli zake za kilimo.

“Kama familia tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizi kwani nakumbuka siku ya tukio nilikuwa naye muda mfupi kabla hatujaachana na baadaye nikapigiwa simu kuelezwa amefariki kwa kupigwa risasi na alikuwa nje ya msitu kabisa, ameuawa katika shamba lake karibu na makazi ya watu,” alisema na kuongeza:

“Serikali tunataka itusaidie tupate haki ya kuuawa kwa ndugu yetu kwa wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria kwani hakuwa na mifugo na alikuwa akijishughulisha na shughuli zake za kilimo siku ya tukio, hivyo wamemfanyia hujuma na tunaomba Serikali itazame familia iliyoachwa na marehemu kwani walikuwa wanamtegemea iweze kulipwa fidia.”

Kwa upande wake Ngaluma, alisema marehemu alikuwa mtu mtulivu na alikuwa akijishughulisha na biashara ambapo alikuwa na duka jijini Nairobi, Kenya na kwamba kama familia wamepoteza mtu muhimu.

Diwani wa kata hiyo, Raymond Lairumbe, alisema baada ya uongozi wa Serikali wa wilaya na mkoa kwenda kuzungumza na wananchi hao walikubali kuzika ndugu yao ambapo Serikali inagharamia gharama za maziko pamoja na zile za matibabu ya majeruhi waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo.

“Viongozi wengine jana walienda kutoa pole kwa familia na kuwafariji wakiwemo viongozi wa Askari wa Suma JKT na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania,  Profesa Dos Santos Silayo na viongozi wengine na Serikali iliahidi kugharamia gharama zote ila kuhusu familia zinaachwaje hili bado hatujajua,” alisema Diwani huyo

Kwa mujibu wa Diwani huyo, idadi ya majeruhi imeongezeka ambapo jana watu wengine watatu waligundulika kuwa na risasi mwilini.

“Lopeny Lesane aliyetibiwa katika Hospitali ya St. Elizabeth, Naishiye Megilienanga na Evaline Meliyo ambapo Lesane alikuja kugundulika ana risasi mguuni hivyo kupelekwa katika Hospitali ya Mt. Meru kwa uchunguzi zaidi.

“Hao akina mama wawili, Evaline alijeruhiwa mkono wa kulia na Naishiye katika paja, walijeruhiwa wakiwa ndani ya nyumba zao kutokana na risasi kurushwa ovyo na hivyo kutoboa nyumba na kuwafikia ila wanadai waliogopa kujitokeza baada ya kujeruhiwa na tumewaleta hapa Mt. Meru na wamekutwa na risasi mwilini, wanaendelea kufanyiwa uchunguzi,” alisema.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Elias Mashala, alikiri kupokea majeruhi hao na kwamba utaratibu wa kuwapatia matibabu unaendelea.

WATATU KUZIKWA LEO

Watu wengine watatu waliofariki katika tukio hilo ambao ni Mbayani Melau (27), Lalashe Mwibuko (25) na Seuri Melita (32), wote wakiwa ni wakazi wa Kata ya Olkokola, wanatarajiwa kuzikwa leo katika vijiji tofauti vilivyopo kwenye kata hiyo.

Juzi Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Jeshi hilo linaendelea kuwahoji askari sita wa Suma JKT.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles