27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAOKOAJI WAKARIBIA KUWAFIKIA WACHIMBAJI WALIOFUKIWA MGODINI

EMMANUEL IBRAHIM-GEITA Na JUDITH NYANGE-MWANZA

VIKOSI vya kuwaokoa wachimbaji wadogo 13 waliofukiwa na kifusi cha Mgodi wa Dhahabu wa RZ Unioni uliopo Nyarugusu mkoani Geita, vimefanikiwa kufukua umbali wa mita 23 kati ya mita 30 na kuwakaribia.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa juhudi za uokoaji chini ya usimamizi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Ofisi ya Madini Kanda ya Ziwa Magharibi ikishirikisha kampuni za migodi GGM na Busolwa.

Kutokana na hatua hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga, amewaonya wawekezaji wa migodi mkoani Geita hasa wanaoendesha uchimbaji bila ya kuzingatia kanuni za usalama hivyo kuhatarisha maisha ya wafanyakazi wake.

Kyunga alisema ajali ya mgodi huo iliyotokea Januari 25, mwaka huu usiku imedhihirisha kuwa wawekezaji wake walikuwa wazembe wasiozingatia maelekezo ya wataalamu ya uchimbaji ikiwamo ujengaji wa miundombinu yake kwa ajili ya usalama.

Aliwataka ndugu na jamaa wa watu hao 13 waliofukiwa na kifusi ndani ya mgodi huo kuwa na subira wakati waokoaji wakiendelea na uokoaji.

“Niwaombe ndugu na jamaa kuendelea kuvuta subira wakati waokoaji wakiendelea na zoezi la uokoaji wapendwa wetu hao ambao tunaamini watakuwa hai chini ya mgodi huo, tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuwaokoa kama watakuwa hai,” alisema Kyunga.

MATUMAINI YAONGEZEKA

Jitihada za kuwakuta wakiwa hai zimezidi kuongezeka baada ya waokoaji kufikia umbali wa mita 23 kati ya 30 kutokana na mpira wa kuingiza hewa kukutwa ukiendelea kupeleka hewa ndani ya shimo hilo kwa umbali wa mita hizo 23.

Akizungumza jana eneo la tukio hilo, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Magharibi, Yahaya Samamba, alisema zoezi hilo litakamilika na upo uwezekano mkubwa wa watu hao kuwa hai na salama kutokana na hewa wanayoipata kupitia mpira unaoingiza kwa kutumia mashine.

“Kazi ya ufukuaji vifusi imeendelea hatua kwa hatua toka jana asubuhi hadi saa 11:02 jioni, licha ya kukumbana na changamoto kadhaa zikiwemo za upungufu wa mashine zaidi zenye uwezo wa kufanikisha zoezi hilo kwa haraka.

“Tumeunda kamati ya uokoaji na kamati yetu imehusisha kampuni zote zilizoleta mashine zao kwa ajili ya uokoaji, niwaombe wananchi na wachimbaji kutulia na kuacha lawama kwa sasa ili kuelekeza nguvu zake kwa kazi ya uokoaji,” alisema Samamba.

Mmoja wa wananchi wanaofuatilia tukio hilo la uokoaji, Saidi Mrisho, alidai hakuna hatua za haraka za uokoaji kwa kuwa zoezi hilo limechukua muda mrefu hali inayoweza kusababisha vifo kwa walio hai na kuiomba Serikali kuangalia umuhimu wa kuwa na vikosi maalumu vya uokoaji.

“Jambo hili linasikitisha, hebu fikiria tangu usiku jana (juzi) hadi leo siku nyingine tumekutana tena watu wako ndani ya kifusi, watapona kweli hawa, licha ya matumaini tunayopewa nadhani Serikali inapaswa kujifunza na kuangalia namna ya uokoaji na si kwa mtindo huu wanaoufanya,” alisema Mrisho.

MTAALAMU WA MIAMBA AELEZA SABABU

Mtaalamu Mshauri wa Miamba wa Kujitegemea, Shigela Aloyce, alisema sababu zinazoweza kusababisha miamba kuporomoka zipo nyingi ikiwemo ya kuwepo kwa nyufa ardhini ambapo wachimbaji hushindwa kuweka nguzo imara na mwishowe kuporomoka.

“Unakuta wachimbaji wanachimba vizuri   eneo lenye miamba iliyooza wakati wa kiangazi, sasa mvua zinaponyesha kwa wingi husababisha ardhi kutitia na kama kutakuwa na watu katika eneo hilo huweza kupata madhara makubwa.

“Milipuko wanayoitumia kupasua baadhi ya miamba katika eneo la uchimbaji husababisha nyufa ambazo hufika kipindi na kushindwa kuhimili vishindo na kuporomoka,” alisema Aloyce.

Aliongeza kusema kuwa suala la uimara wa miamba wa sehemu husika pia linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa hasa kwa wachimbaji ambao huchimba maeneo ya karibu na pale mwamba unaowatenganisha unapokosa uimara huporomoka.

Aliwashauri wachimbaji kutafuta ushauri wa wataalamu wa miamba kabla ya kuanza shughuli ya uchimbaji wa madini katika eneo lolote.

Matukio yaliyowahi kutokea hapa nchini:

Nyangarata-Shinyanga

Tukio la aina yake ambalo wachimbaji wadogo watano kati ya sita waliokolewa wakiwa hai katika Mgodi wa Dhahabu Nyangarata, Kahama mkoani Shinyanga baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo na kuishi ardhini kwa siku 41.

Wachimbaji hao walifukiwa Oktoba 5, mwaka juzi saa tano asubuhi wakati wakiendelea na shughuli zao za uchimbaji chini ya ardhi na kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, ardhi ya juu ya machimbo hayo ilititia na kuporomoka kutokana na mvua iliyonyesha na hivyo kuwafunika wachimbaji hao.

Katika tukio hilo linatajwa kuwa la pili kwa ukubwa kutokea baada ya lile lililotokea Septemba, mwaka juzi, ambapo wachimbaji 11 waliokolewa kutoka katika mashimo hayo baada ya kutitia mara mbili huku mmoja akitolewa akiwa amekufa.

Jitihada za uokoaji zilifanikisha kuokolewa wachimbaji wengine sita huku wengine wakishindwa kufikiwa kutokana na kukosekana kwa taarifa sahihi za idadi ya watu waliokuwa katika eneo hilo hivyo waliweza kutolewa katika mashimo hayo Novemba 15, mwaka juzi wakiwa wamekaa ardhini kwa siku 41.

Wachimbaji hao walikuwa wakiishi umbali wa mita 100 kutoka juu ya ardhi, walisema mwenzao, Musa Spana, alikufa siku chache baada ya kufukiwa na kifusi hicho kutokana na kukosa chakula na waliookolewa ni Chacha Wambura, Amos Muhangwa, Joseph Burulwa, Msafiri Gerald na Wonyiwa Moris.

Moshono-Arusha

Tukio jingine kubwa na la kusisimua lilitokea Machi 31, 2013 ambapo watu 14 kati ya 20 na magari mawili ya kubeba mchanga walifariki dunia baada ya  kufukiwa na kifusi katika machimbo ya Moramu yaliyopo Moshono mkoani Arusha.

Tukio hilo lilitokea baada ya gema kuporomoka ghafla na kuwafunika watu 20 na magari mawili yaliyokuwa ndani ya shimo hilo wakati shughuli za uchimbaji zikiendelea.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa zamani, Mizengo Pinda, alitangaza rasmi Serikali kuyafunga machimbo hayo alipowatembelea na kuwajulia hali majeruhi waliookolewa katika tukio hilo.

Sabora – Geita

Aprili 12, 2010 vilio na simanzi vilitawala mkoani Geita baada ya wachimbaji wadogo 60 kufukiwa na kifusi katika moja ndani ya mashimo ya mgodi wa dhahabu uliopo Kijiji cha Sobora, Kata ya Kaseme huku 16 wakihofiwa kufa na wengine zaidi 20 kujeruhiwa.

Mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na Kampuni ya IAMGOLD iliyokuwa na leseni ya utafiti na si uchimbaji dhahabu na baada ya wachimbaji wadogo kusikia dhahabu ‘imefuka’ walivamia eneo hilo na kuanza kuchimba.

Licha ya Jeshi la Polisi kuwaondoa wachimbaji katika eneo hilo, lakini hawakwenda mbali, kwa sababu walikaa kuuzunguka mgodi huo huku wakisubiri kauli ya Serikali iliyotarajiwa kutolewa baadaye.

Msalala-Shinyanga

Wachimbaji wadogo wadogo 19 wa dhahabu walifariki dunia baada ya kuporomoka kwa mashimo yaliyopo  katika Kijiji cha Karore, Kata ya Runguya, Tarafa ya Msalala wilayani Kahama na  kufunikwa na kifusi cha udongo.

Wachimbaji hao walivamia machimbo hayo yaliyoachwa kuchimbwa muda mrefu na kuanza shughuli ya uchimbaji kutokana na kutokuwa imara na mvua iliponyesha iliporomosha kifusi kilichowafukia na kusababisha vifo vyao.

Mgusu-Geita

Novemba 29, mwaka juzi wachimbaji watano wa dhahabu walifariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi katika eneo la Prospect 30 linalomilikiwa na Mgodi wa Geita (GGM) lililopo Mgusu mkoani Geita.

Tukio hilo lilitokea saa sita usiku baada ya wachimbaji hao kuvamia eneo hilo ambalo si salama na lililowahi kupigwa marufuku kwa shughuli za uchimbaji na kuanza kuchimba kinyume cha sheria.

Wachimbaji hao walifukiwa wiki mbili tu tangu wachimbaji wengine watano kuokolewa wakiwa hai katika machimbo ya Nyangarata wilayani Kahama mkoani Shinyanga, baada ya kufukiwa na kifusi kwa siku 41.

Mkinga-Tanga

Februari 10, mwaka juzi wakazi wawili wa Kata ya Kigongoi wilayani Mkinga, walifariki dunia papo hapo baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo walipokuwa wakichimba madini aina ya vito katika eneo la mgodi unaomilikiwa na Charles Kifunta.

Ajali hiyo ilitokea baada ya Nyange Mussa (21) mkazi wa Kitongoji cha Hemsambia na Kagembe Shabani (19) wa Kitongoji cha Shashui, kushukiwa na gema la udongo (kifusi) walipokuwa ndani ya mgodi na kufariki papo hapo huku Alex Remo (24) akijeruhiwa.

Iramba-Singida

Novemba 2, mwaka jana wanawake watatu wachimbaji madini mkoani Singida, walipoteza maisha na wengine wawili kujeruhiwa baada ya mwamba kumeguka na kuwaporomokea kisha kufunikwa na kifusi cha udongo wa shimo walimokuwa eneo la Zambia, Kitongoji cha Matongo Kijiji cha Mgongo wilayani Iramba.

Chunya-Mbeya

Desemba 27, mwaka juzi wachimbaji wadogo wawili walihofiwa kufa baada ya kufukiwa na kifusi wakiwa kazini katika machimbo bubu ya dhahabu yaliyopo eneo la Mnadani, Kata ya Sangambi, Chunya mkoani Mbeya.

Taarifa za kufukiwa kwa wachimbaji hao, zilifahamika baada ya mmoja wa wachimbaji kuingia mgodini na kusikia sauti za watu wakiomba msaada wa kuokolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles