23.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

MWANAFUNZI ARU KIZIMBANI KWA KUDAI KUNA NJAMA DHIDI YA UHAI WA LEMA

Na MANENO SELANYIKA

-DAR ES SALAAM

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam (ARU), Juvenal Shirima, jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kuchapisha taarifa zinazodaiwa kuwa ni za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Mtuhumiwa huyo ambaye anadaiwa kuwa kada wa Chadema, alisomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali Adolf Mkini, mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Mkini alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja la kuchapisha taarifa za uongo, Januari 13, mwaka huu maeneo mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam.

Alidai kupitia mtandao wa WhatsApp kwenye kundi linalotumia jina la ‘Lowassa Foundation and Bunge Live’ alichapisha taarifa za uongo.

Wakili Mkini, alinukuu maneno hayo  yanayodaiwa kuandikwa na Shirima yanayosomeka: “Nimepata rhema ya mipango michafu sana iliyokuwa inapangwa na bado inapangwa dhidi ya uhai wa (Mb), Godbless Lema…”

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana kuhusika na kosa hilo. Wakili Mkini alisema upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na hana pingamizi na dhamana ambapo aliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mwambapa alimpa masharti ya dhamana mtuhumiwa huyo ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 10 kwa kila mmoja pamoja na barua kutoka kwa waajiri wao ambao ni taasisi yoyote inayotambulika kisheria.

Mshtakiwa huyo alinusurika kwenda mahabusu baada ya kutimiza masharti ya dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Februari 19, mwaka huu.

Mbunge Lema ambaye hadi sasa yupo rumande kwa kukosa dhamana, anakabiliwa na kesi mbili za uchochezi  dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Katika kesi ya kwanza ya jinai namba 440, Lema anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi Oktoba 22, mwaka jana maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro, katika mkutano wa hadhara, alitoa maneno yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii.

Kesi nyingine inayomkabili Lema ni ya Jinai namba 441, ambapo anakabiliwa na shtaka la uchochezi na anadaiwa kutoa matamshi yenye chuki, kuibua nia ovu kwa jamii.

Inadaiwa Lema alisema kuwa: “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani, iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu. Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya Katiba, Rais huyo ataingiza Taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles