28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Familia ya Tundu Lissu yamshangaa Ndugai

EVANS MAGEGE

SIKU moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kusema anafikiria kusitisha mshahara na malipo yote ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kutokana na ofisi yake kutokuwa na taarifa sahihi ya mahali alipo kwa sasa na anachokifanya huko, familia ya mbunge huyo imemshangaa kwa kutoa kauli hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, kaka wa Lissu, Wakili Alute Mughwai, alisema anashangazwa na Spika Ndugai kuwa na fikra hiyo wakati akijua wazi yeye mwenyewe pamoja na ofisi yake inafahamu mahali alipo Tundu Lissu na sababu kuu iliyompeleka huko.

Akizungumza kwa utulivu wa hali ya juu, Mughwai akielezea kile kinachothibitisha Ndugai na Bunge lina taarifa za maandishi mahali alipo Lissu, alisema katika kumbukumbu zake kwa niaba ya familia, amepata kuwasiliana na Ofisi ya Bunge kwa njia ya barua mara sita na kujibiwa mara tano.

Alisema katika moja ya barua alizopata kuwasiliana na Ofisi ya Bunge ni ile ya kutaka ilipie gharama za matibabu ya Lissu kwa sababu bado ni mbunge halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kutokana na ombi hilo, Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai, alimjibu Mughwai Novemba 27, 2017, akimtaka aeleze ni stahiki zipi ambazo ndugu yao anastahili apewe na Bunge.

Mughwai alikwenda mbali zaidi kwa kutoa ufafanuzi wa jinsi Ofisi ya Bunge ilivyokuwa inatambua Lissu alipo na nini anachokifanya, ambapo ofisi hiyo iliwahi kumwandikia barua nyingine ikimweleza kuwa wanatuma madaktari kwa ajili ya kwenda kuangalia maendeleo ya afya ya Lissu.

“Kuna barua nyingine walinitumia Ofisi ya Bunge wakinieleza kuwa wana mpango wa kutuma madaktari pale kwa ajili ya kwenda kusaidia kwenye matibabu ya Lissu pale Nairobi, lakini niliwajibu tayari Lissu tumemhamishia Ubelgiji, niliwapa anwani zote za hospitali ambayo Lissu alikuwa akipatiwa matibabu.
“Lakini tukumbuke Spika Ndugai amewahi kuulizwa na waandishi wa habari kwa nini hajakwenda kumtembelea hospitali mbunge wake (Tundu Lissu), akajibu kwamba alikuwa amebanwa na shughuli, kwamba akipata muda atakwenda kumtembelea na hii kauli sijawahi kumsikia kaikanusha,” alisema Mughwai. 

Zaidi alisema Lissu alipokuwa Hospitali ya Nairobi, Balozi wa Tanzania nchini Kenya aliwahi kufika hospitali kumjulia hali, vivyo hivyo alipohamishiwa Ubelgiji, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini humo, Edward Sokoine alimtembelea mara mbili.

Alisema hatua zote hizo za mabalozi ambao ni wawakilishi wa nchi kwenye mataifa mengine kumtembelea Lissu zinaonyesha kuwa Serikali ilikuwa inafahamu mahali alipo Lissu na anafanya nini, kwamba hata uongozi wa Bunge ungeweza kupata taarifa zote zinazohusu Lissu kupitia kwa balozi hizo.  

HOJA YA MSHAHARA

Akizungumzia hoja ya kusitishiwa mshahara kwa ndugu yao, Mughwai alisema Lissu anastahili kulipwa mishahara yake yote, isipokuwa posho za vikao ambavyo hajahudhuria kwa sababu hadi sasa ni mbunge halali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na mtazamo huo, Mughwai alisema Spika Ndugai ana uzoefu wa muda mrefu katika utumishi wa uongozi wa mhimili huo wa Serikali, hivyo anaamini atamtendea haki mbunge wake, Lissu.

“Namuomba Spika Ndugai asisukumwe kwa kupewa jazba na hao akina Msukuma na Makonda,” alisema Mughwai.

KATIBU WA BUNGE

Gazeti hili lilimtafuta mara kadhaa bila mafanikio Spika Ndugai ili kutaka kufahamu kama amekwishatekeleza kile alichosema anafikiria kuchukua uamuzi juu ya mshahara wa Lissu.

Kutokana na hilo, Gazeti hili liliwasiliana na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai, ambaye ndiye Mtendaji wa Shughuli zote za Bunge, ili kupata ufafanuzi wa kanuni ambazo Bunge linaweza kutumia kusimamisha mshahara na malipo yote ya Lissu.

Baada ya kusikiliza swali hilo, Kagaigai alinyamaza kwa sekunde kadhaa, kisha akajibu kuwa amebanwa na majukumu, hivyo atamtafuta baadaye mwandishi kwa ajili ya kujibu swali hilo.

Baada ya muda kupita mwandishi alijaribu tena na tena kumpigia simu, lakini Kagaigai hakupokea.

Mbali na Kagaigai, mwandishi wa gazeti hili alimtafuta kwa mara nyingine kwa njia ya simu Spika Ndugai, lakini naye hakupokea simu.

KANUNI ZINASEMAJE?

Uchambuzi wa gazeti hili katika Kitabu cha Kanuni za Bunge, cha Januari 2016, umebaini kanuni  namba 146 ambayo ipo sehemu ya 18  ukurasa wa 96, ikiwa na vipengele vitano ambavyo maelezo yake yanatafsiriwa na baadhi kwamba huenda yakatumiwa na Spika Ndugai kutekeleza fikra yake ya  kusimamisha mshahara na malipo yote ya Lissu.

Kanuni hiyo ni 146 inaeleza; (1)Kuhudhuria vikao vya Bunge na Kamati zake ni wajibu wa  kwanza wa kila mbunge.

(2)Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake kwa mujibu wa Ibara ya 71(1)(c) ya Katiba na Spika ataiarifu Tume ya Uchaguzi.

(3) Mbunge atakapokosa kuhudhuria nusu ya vikao vya Mkutano mmoja bila sababu ya msingi atapewa onyo.

(4) Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria vikao vya Bunge na Kamati zake kwa sababu maalumu atatakiwa kupata kibali cha Spika.

(5) Kwa madhumuni ya fasili ya (4) ya kanuni hii, kibali kitatolewa katika Ofisi za Bunge za Dodoma, Dar es Salaam au Zanzibar.

KAULI YA MSUKUMA

Msingi wa kauli ya Spika kufikiria kusimamisha mshahara wa Lissu ni hoja iliyoibuliwa juzi bungeni na Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku (Musukuma), ambaye alimuomba mwongozo Spika, kwa kuhoji Lissu hayupo hospitali, bungeni, Tanzania wala hajulikani anafanya kitu gani huko aliko, hivyo hana sababu ya kuendelea kulipwa.

Katika mwongozo huo, Musukuma alihoji ni lini Bunge litasitisha mshahara wa Lissu,  kwa kuwa ameshapona na anazurura, huku Bunge likiendelea kumlipa mshahara.

 “Kwa kuwa leo (jana) tunajadili taarifa ya kamati na tunajadili taarifa ya Wizara ya Afya na kwakuwa zipo sheria zinazoweza kumruhusu mtu kuitwa mgonjwa, lakini tunaona Mheshimiwa Tundu Lissu anazunguka kwenye nchi mbalimbali, lakini huku anasomeka kama mgonjwa.

“Sasa Mheshimiwa Spika nilikuwa naomba mwongozo wako ni lini Bunge litasitisha mshahara wake, kwakuwa ameshapona, anazurura na Bunge linaendelea na yeye hayupo na mnaendelea kumlipa mshahara.

“Na anazunguka nje anatukana Bunge, anatukana viongozi. Nilikuwa naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika,” alihoji Musukuma.

MAJIBU WA SPIKA NDUGAI

Akijibu, Spika Ndugai alisema ipo haja ya kusimamisha malipo ya aina yoyote ile ya Lissu, hadi hapo Ofisi ya Bunge itakapopata taarifa rasmi yuko wapi na anafanya nini.

“Ni kweli jambo hili kwa ndugu yetu, mbunge mwenzetu Tundu Antipas Lissu linahitaji kuangaliwa kipekee, kwa maana ya kwamba mbunge hayupo jimboni kwake, hayupo hapa bungeni anapofanyia kazi, hayupo hospitalini, hayupo Tanzania.

“Na taarifa zake Spika hana kabisa, wala hajishughulishi hata kumwambia niko mahali fulani au nafanya hivi na kama ni mgonjwa hakuna taarifa yoyote ya daktari, halafu unaendelea kumlipa malipo mbalimbali,” alisema.

Spika Ndugai alisema hoja ya Musukuma ni ya msingi na kuna haja ya kusitisha malipo yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles