24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Fainali uchaguzi mkuu 2015

mtz1Na Mwandishi Wetu

NI fainali, ndivyo unavyoweza kusema kwa wakati huu ambao zimebaki saa 24 kwa wagombea wa nafasi ya urais, ubunge na udiwani kutupa kete yao ya mwisho leo kwa ajili ya kunadi sera zao na kuwashawishi Watanzania ili wawapigie kura kesho.

Vyama viwili kati ya vinane vilivyosimamisha wagombea wake wa nafasi ya urais vinavyochuana vikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya washirika wao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimeonekana kujipanga kimbinu na kimkakati kutumia siku mbili za mwisho za kampeni (jana na leo) ili kujihakikishia ushindi.

Taarifa kutoka ndani ya Chadema na CCM, zinaonyesha kuwa mbinu na mikakati inayotumiwa na vyama hivyo katika kampeni hizo za lala salama ni pamoja na kuwafikia wapiga kura katika maeneo yenye wapiga kura wengi na maeneo yenye ushindani mkubwa wa kisiasa.

Mbinu nyingine ni kuhakikisha wanatumia nguvu ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kuwafikia wapigakura wengi na kwa wakati mmoja.

Watu wanaofuatilia mwenendo wa kampeni hizo ambazo wakati zinahitimishwa leo zitakuwa zimechukua siku 64, wanasema si jambo la bahati mbaya kwa mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, kufanya kampeni zake jana jijini Dar es Salaam na kupanga kuhitimisha leo jijini Mwanza akisindikizwa na Rais Jakaya Kikwete.

Pia wanasema si jambo la bahati mbaya kwa mpinzani wake wa karibu, Edward Lowassa wa Chadema kuutumia usiku wa kuamkia leo kuhutubia Taifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na hotuba yake kurushwa katika mitandao ya kijamii.

Si hivyo tu pia Lowassa pamoja na vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na NLD kuamua kuhitimisha kampeni zao leo katika Jiji la Dar es Salaam.

Kwa muktadha huo huo, hatua ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kuhitimisha kampeni jijini Mwanza, katika Jimbo la Nyamagana linalotetewa na mgombea wa Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Ezekiel Wenje, kumetajwa kuwa na lengo la kulinda kura za upinzani.

Msemaji wa Chadema, Tumainiel Makene, juzi alikaririwa akisema shughuli nyingine za ufungaji wa kampeni za Ukawa zitafanyika katika majimbo na kanda za chama hicho ambapo kutakuwa na wagombea ubunge pamoja na viongozi wa chama.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na wapiga kura wengi wanaofikia 2,775,295 ikifuatiwa na Mwanza ambayo inawapiga kura 1,448,884 na Mbeya yenye wapiga kura 1,397,653 huku Mkoa wa Morogoro ukiwa wapiga kura 1,271,951.

Kwa misingi hiyo hiyo, CCM ambayo katika uchaguzi huu ndiyo inayoonekana kuwa na wakati mgumu, imeamua kutupa kete yake ya mwisho kwa kutuma vigogo wake katika mikoa korofi na yenye upinzani mkali.

Mikoa hiyo kwa mujibu wa Mjumbe wa Kamati ya Kampeni wa CCM, January Makamba, ni pamoja na Mbeya ambako amepelekwa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kwenda kuhitimisha kampeni leo na Kigoma ambako amepelekwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Phillip Mangula.

Maeneo mengine ambayo yanatajwa kuwa ni korofi kwa CCM, ni pamoja na Mtwara ambako amepelekwa Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi,  Kilimanjaro, Yusuph Makamba na Musoma, Jaji Joseph Warioba.

Mwenendo wa kampeni unaonyesha kuwa pamoja na Lowassa na Magufuli kuhodhi sehemu kubwa ya kampeni za mwaka huu, lakini katikati yao wamo wangombea wengine wa urais kupitia vyama vya ACT –Wazalendo, Anna Mghwira.

Wagombea wengine ni Hashim Rungwe wa Chauma, Fahmi Dovutwa wa UPDP, Macmilan Lyimo wa TLP, Janken Kasambala wa NRA, Lutasola Yemba wa ADC.

Kati ya wagombea hao ni Mghwira na Rungwe tu ambao nyendo zao za kisiasa zimeonekana kutazamwa kwa karibu na baadhi ya watu wanaofuatilia kampeni za mwaka huu.

Mghwira licha ya kwamba chama chake ni kichanga, lakini uwepo wa mwanasiasa machachari, Zitto Kabwe, kunatajwa kuweza kukiweka chama hicho katika nafasi ya tatu.

Msemaji wa ACT- Wazalendo, Abdallah Khamis, aliliambia MTANZANIA Jumamosi jana kuwa mgombea wao atahitimisha kampeni zake za urais mjini Singida ambako ni nyumbani kwao.

Mbali na Mghwira, mgombea urais wa Chaumma, Hashim Rungwe ambaye katika kampeni zake amejipambanua kama jeshi la mtu mmoja naye atahitimisha kampeni zake leo.

Rungwe anahitimisha kampeni za urais mwaka huu akiacha rekodi ya kutotegemea nguvu ya vyombo vya habari au mabango kujitangaza kama ilivyoshuhudiwa kwa wagombea wengine.

Watu wanaofuatilia mwenendo wa kampeni zake wanasema Rungwe hakuweka mbele nguvu ya bendera au aina ya mavazi yanayotambulisha chama chake, lakini aina ya siasa aliyoifanya katika kampeni za mwaka huu zimeonekana kumuweka katika nafasi nzuri ya kisiasa ukilinganisha na wagombea wengine wa urais wa vyama vya UPDP, TLP, Chauma na NRA.

Inaelezwa kuwa tangu mwanzo hadi leo wakati kampeni zinafika ukomo, ratiba ya kampeni za Rungwe haikuwa wazi au haikueleweka kwa sababu hakuwa na utaratibu wa kuita na kukusanya watu bali alipita sehemu mbalimbali zenye mikusanyiko ya watu kama sokoni, vituo vya daladala na wakati mwingine alifanya mikutano pembezoni mwa barabara.

Duru zaidi za mambo zinadai kuwa aina ya siasa aliyoifanya Rungwe katika kampeni za mwaka huu, zinaweza kuwa ni hazina kwa chama chake katika chaguzi zijazo.

Naye mgombea urais kupitia Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Chief. Lutasola Yemba, alifunga rasmi kampeni za chama chake jana huko Ujiji mjini Kigoma.

Ukiachilia mbali wagombea hao watano, wangombea wa vyama vya TLP, UPDP na NRA walionekana kwa nadra katika kampeni, ratiba zao za kampeni hazikuwa wazi na mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni jana halikufanikiwa kupata ratiba za kufunga kampeni kutoka katika vyama hivyo.

Pamoja na yote, wagombea hao wanaingia katika fainali za mchuano mkali wa kampeni wakiongozwa na vinara wake ambao ni Lowassa pamoja na Dk. Magufuli ambao wameleta hamasa kubwa kwa wananchi  ambao kesho watajitokeza kupiga kura na kuamua mshindi.

 

Idadi ya wapiga kura

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jumla ya wapiga kura wanaotarajiwa kujitokeza kesho ni 22,751,292 na Zanzibar ni 503,193 na watapiga kura kwa rais, wabunge na madiwani.

Idadi ya wapigakura kwa mwaka huu inatazamwa kuwa tofauti na ile ya mwaka 2010, ambapo watu waliojiandikisha walikuwa 20,137,303, lakini waliopiga kura ni watu 8,398,394 sawa na asilimia 42.64.

Ikumbukwe kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2005, wananchi waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 16,407,318 na waliopiga kura walikuwa 11,365,477 sawa na asilimia 69.3 ya waliojiandikisha.

Kutokana na hamasa ilivyo, baadhi ya viongozi wa NEC waliozungumza na gazeti hili wanasema kampeni za mwaka huu zinaonyesha kuwa idadi ya wapigakura inaweza kuwa mara dufu ya kiwango cha chaguzi zilizopita kutokana na hamasa ya siasa za mabadiliko iliyochochewa na kuhama kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutoka CCM na kwenda Chadema.

Lowassa aliyekatwa jina lake katika kinyang’anyiro kilichoshirikisha makada 38 wa CCM, anatazamwa kama mtu aliyejiandaa kwa muda mrefu kugombea urais hivyo tayari alikuwa amekwishaweka ngome imara ya kumuunga mkono ndani na nje ya chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles