25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

Mita 200 yapigwa marufuku

Pg 4 oct 24Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetamka bayana kwamba hairuhusiwi watu kukutana mahali popote bila kujali umbali wake siku ya uchaguzi kesho.

Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu waliokuwa wakisikiliza mvutano wa kisheria kuhusu kukaa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura.

Mwenyekiti wa jopo hilo, Sekieti Kihiyo na Jaji Lugano Mwandambo kwa nyakati tofauti walipokuwa wakisoma uamuzi huo, walisema wamezingatia hoja zilizowasilishwa na pande mbili zilizokuwa zikivutana.

Majaji hao wawili pamoja na Jaji Aloycius Mujuluzi katika uamuzi wao walisema kifungu cha sheria na Uchaguzi namba 104(1) kinakataza mikutano bila kujali umbali wake.

“Katika jengo linalopigiwa kura ambalo baadaye linageuka kuwa la kuhesabia kura hairuhusiwi kuonekana nembo ya chama chochote, picha ya mgombea ama alama yoyote itakayoonyesha ni mwanachama wa chama fulani.

 

“Umbali wa mita 200 hairuhusiwi kuonekana mabango, bendera, picha, nembo na vitu vingine vyovyote vitakavyoonyesha uanachama wa chama fulani,” lilisema jopo hilo.

Hata hivyo, jopo hilo lilisema uamuzi wa Wakili Peter Kibatala, Wakili Omari Msemo wa kumwakilisha mteja wao Amy Kibatala kutafuta tafsiri ya kifungu hicho cha sheria ulikuwa sahihi.

Baada ya kutoa uamuzi huo, Kibatala aliweka wazi kwamba Jumatatu wanatarajia kukata rufaa kuupinga kwa sababu unaminya haki za wananchi.

“Tunatarajia kukata rufaa, hata kama haitasaidia katika uchaguzi huu, itasaidia katika uchaguzi ujao, tukiacha kufanya hivyo haki za wananchi zitaminywa,” alidai.

Upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliwakilishwa na mawakili nane akiwemo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Tulia Ackson, Wakili Mkuu wa Serikali, Obadia Kimeya, Sarah Mwaipopo, Alesia Mbuya, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Richard Kilaga, Aida Kisumo.

Wengine ni Emmanuel Avishe na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hamidu Mwanga kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akiwasilisha hoja, Dk. Tulia alidai kwamba vifungu alivyotumia mleta maombi kuwasilisha maombi yake mahakamani hakuna mahali ambapo vimevunjwa kwa mujibu wa sheria.

Alidai kwamba, kifungu cha sheria ya uchaguzi namba 104(1) kinakataza mikutano ya aina zote bila kujali umbali.

Dk. Tulia alidai kifungu namba 72 cha Sheria ya Uchaguzi kinaelekeza watu wanaotakiwa kuwepo mahali zinapohesabiwa kura ambao ni mawakala, wagombea, waangalizi wa uchaguzi na wengine wanaoruhusiwa, ambaye hakutajwa katika kifungu hicho hatakiwi kuwepo.

Alidai kilichozungumzwa na NEC kuhusu kukaa umbali wa mita 200 yalikuwa ni maelekezo na yaliyozungumzwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, ilikuwa amri na alichozungumza Rais Kikwete kilikuwa msisitizo.

Dk. Tulia alidai maelekezo yaliyotolewa na NEC yalifuata utaratibu na aliyosisitiza Rais Kikwete alifuata maelekezo yaliyotolewa na NEC ili kuwepo kwa uchaguzi wa amani, huru na wa haki.

Alidai sheria inakataza kufanyika kwa mikutano mahali popote siku ya uchaguzi na kwamba umbali wa mita 200 unahusiana na mtu kuonyesha alama, picha, bendera za chama zinazosapoti chama ama mgombea kutoka katika kituo cha kupigia kura.

 

Wakili Peter Kibatala alipokuwa akiwasilisha hoja zake alidai anaiomba mahakama iweze kutoa tamko kuhusu maana halisi na kusudio la kisheria la kifungu namba 104(1) cha sheria ya uchaguzi sura namba 343.

Pia anaomba mahakama iangalie maana ya kifungu hicho katika haki za wapiga kura ama watu wengine wenye shauku ya kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura.

Kibatala alidai msingi wa shauri hilo ni matamko yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi kwamba mpiga kura ama mtu mwingine mwenye shauku wasikae mahali popote katika kituo cha kupigia kura, hata kama kutakuwa umbali wa mita 200 kutoka katika kituo ambacho zoezi la kupigia kura linaendelea.

Maelekezo hayo yalitolewa tena na Rais Jakaya Kikwete katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya kifo cha mwalimu Nyerere, Oktoba 14 ambapo si tu kusisitiza katazo bali alikwenda mbali zaidi na kuonyesha kwamba asiyetii atachukuliwa hatua za kisheria.

Wakili Kibatala alidai lengo la kifungu hicho cha sheria ni kuzuia mikutano ya kampeni siku ya uchaguzi kwa sababu siku hiyo ni ya kupiga kura na si watu kukaa umbali wa mita 200 kwa utulivu.

Alidai sheria hiyo haimaanishi kwamba asiyefanya kampeni anazuiliwa kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200 na kwamba mtu anaweza kuvunja sheria mahali popote.

Mleta maombi ni Amy Kibatala ambaye ni mgombea ubunge wa Viti Maalumu Kilombero (Chadema) ambaye pia amejitambulisha kuwa ana masilahi katika uchaguzi huo.

Kibatala alifungua kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles