21.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Fagio la chuma kupita ATCL

makamenewNA EVANS MAGEGE

SERIKALI imeiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kuisafisha menejimenti ya shirika hilo katika kipindi cha miezi mitatu.

Imetaka menejimenti yote itimuliwe au ibadilishwe kwa sababu imejiridhisha kuwa haiwezi kusaidia kuivusha kufikia malengo yake ya kuifufua ATCL.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati akizundua menejimenti mpya ya ATCL ofisini kwake Dar es Salaam.

Alisema Bodi ina hiari ya kuamua kuitimua au kuibadilisha menejimenti iliyopo na kwamba itakayoundwa itapewa muda wa miezi sita kutathmini mwenendo wa utendaji kazi wake.

“Uongozi uliopo sasa binafsi siuoni kama utanivusha, labda unaweza kunivusha kama watabadilisha mawazo yao na wanavyofanya kazi lakini kwa mtazamo wangu wanavyofanya kazi kwa sasa hawawezi kunivusha.

“Hivyo nawapa miezi mitatu, nataka kuona mabadiliko makubwa kwenye menejimenti. Kama ni kuwaondoa au kuwabadilisha baadhi mimi nahitaji mabadiliko makubwa na ninaamini hamtaniangusha.

“Na kama mtaamua wote muwaweke wapi hiyo si kazi yangu ni kazi ya bodi. Mimi nahitaji mabadiliko makubwa na lazima yafanyike najua mkimalizana na menejimenti ATCL lazima itasimama,” alisema Prof. Mbarawa.

Sambamba na agizo hilo, Waziri Mbawara alitangaza kuanzisha mfumo wa kupima wa utendaji kazi wa watendaji, menejimenti, bodi ya wakurugenzi na katibu mkuu ambao sasa watalazimika kusaini mikataba ya makubaliano ya kutekeleza malengo waliyojiwekea.

Kwamba Waziri atasaini makubaliano hayo na Bodi ya Wakurugenzi na Katibu Mkuu atasaini makubaliano hayo na Mtendaji Mkuu wa ATCL ambaye pia atasaini mikataba ya aina hiyo na watendaji walio chini yake.

“Mikataba hii itashuka chini kwa maana ya Mtendaji Mkuu wa Shirika naye ataweka mikataba na watendaji wote wa shirika walio chini yake kisha tutapitia mikataba yote kila baada ya miezi sita.

“Kwa kuwa tunaanza upya hatuwezi kutoa mikataba ya muda mrefu hivyo kila baada ya miezi sita lazima tupitie mikataba kama mtashindwa ninyi wenyewe kufanya kazi kwa ufanisi ni bora tuwafungulie mlango muondoke na muwaambie watendaji wa ATCL kama watashindwa waambieni kwaheri,” alisema Prof. Mbarawa.

Waziri huyo pia alimtaka mwenyekiti mpya wa bodi, Mhandisi Emmanuel Korosso na wajumbe wake kusimamia maboresho ya mpango kazi wa biashara za shirika, uadilifu, kasi ya utendaji kazi pamoja na ubunifu.

Aidha, aliiagiza bodi hiyo kuziba mianya ya wizi wa mafuta ya ndege, kutolipiwa mizigo inayosafirishwa kwenda Comoro, ukiritimba na upotevu wa mapato.

“Kama tunavyojua usafiri wa anga una ushindani mkubwa hapa nchini kwa hiyo kama Serikali na shirika letu la ndege lazima tuhakikishe tunaboresha mpango mkakati wetu wa biashara ili kuendana na wakati. Si ule uliopitwa au ule wa mwaka jana, tunataka wa leo.

“Nataka uadilifu wa hali ya juu. Inafahamika ndani ya ATCL kwa muda mrefu hakuna uadilifu na kama huna uadilifu hata kama umefanya mpango mkakati wa namna gani hautakusaidia.

“Uadilifu usimamiwe kuanzia kwenye bodi, watendaji wa juu hadi wa chini ndani ya shirika ili kuongeza kasi ya utendaji kazi. Katika yote haya lazima kuwapo na ubunifu,” alisema Prof. Mbarawa.

Wakati huo huo, Prof. Mbarawa alieleza kuwa Serikali ina mpango wa kununua ndege mbili aina ya Jet zitakazotumika kwa usafiri wa abiria.

Alisema tayari maandalizi ya kununua ndege hizo yamekwishaanza na zinatarajiwa kuwasili nchini mapema mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,580FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles