25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 8, 2022

Contact us: [email protected]

IPTL kaa la moto

iptl-kaa-la-moto*Zitto, Bashe wampa JPM ushauri mzito

Na WAANDISHI WETU

UAMUZI wa Mahakama ya Kimataifa (ICSID) kuitaka Tanesco kuilipa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Kimarekani milioni 148.4 sawa na Sh bilioni 320, lakini pia IPTL kutakiwa kurejesha zaidi ya Dola za Marekani, milioni 100 (sh bilioni 216.2) kwa Tanesco zikiwa ni fedha ambazo zililipwa kabla ya ukokotozi kufanywa upya, umefufua upya mzimu wa sakata hilo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 20.

Kauli za sasa za wanasiasa ikiwamo ile ya Zitto Kabwe, Hussein Bashe na Elibariki Kingu kutaka vigogo wanaofaidika na mitambo kwa kutumia mlango wa nyuma wajulikane na hata kuchukuliwa hatua kali, ndizo zinazoonekana kuwasha moto upya juu ya sakata hilo.

Zitto Kabwe ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), ndiye aliyeongoza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) katika Bunge la 10 kuchunguza juu ya suala hilo na kisha kutoa maazimio nane likiwamo lile la kuitaka Serikali ifilisi mitambo hiyo.

Jana kwa nyakati tofauti wanasiasa hao ambao pia ni wabunge waliandika maandiko yenye mwelekeo unaofanana wakitamka Rais John Magufuli kushughulika na mizizi hadi matawi ili kulifikisha mwisho sakata hilo.

Katika andiko lake jana, Zitto alirejea hukumu ya sasa akisema imegusa maeneo yale yale ambayo yalipendekezwa katika Taarifa Maalumu ya PAC Novemba 2014.

Zitto anasema ilimchukua siku mbili kusoma hukumu hiyo hadi kuielewa na kugundua iwapo Serikali ingetekeleza maazimio yote ya Bunge leo hii nchi ingekuwa kwenye nafasi nzuri ya kulimaliza suala hilo ambalo alidai limenyonya fedha za Watanzania.

Zitto aliyataja masuala makuu mawili ambayo alisema yakieleweka juu ya kashfa ya IPTL, maamuzi yanaweza kufanyika na kulimaliza.

“Suala la kwanza baada ya mbia Kampuni ya Mechmar kufilisika nchini Malaysia, ni nani mwenye haki na mali za IPTL? Tozo ya malipo ya umeme uliozalishwa ilizidishwa? Kwenye taarifa ya PAC tulionyesha kwa vielelezo na ushahidi kwamba kampuni ya PAP haikuwa na umiliki kihalali wa asilimia 70 ya hisa za IPTL,” aliandika Zitto.

Katika kuthibitisha hilo, Zitto alisema hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alionyesha dhahiri kuwa vyeti vya hisa za kampuni ya Mechmar kwenye IPTL walikuwa nazo Benki ya SCB-HK kama dhamana ya mkopo waliowapa IPTL.

Alisema kamati ya PAC vile vile  ilionyesha kwa ushahidi kuwa PAP hawakufuata sheria za Tanzania katika kumiliki IPTL ikiwemo kukwepa kodi kupitia kampuni iliyoitwa PiperLink ya British Virgin Island.

Alisema Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) walikiri mbele ya Kamati kuwa wakati Mahakama Kuu inatamka kuwa PAP wapewe masuala (affairs) ya IPTL  hawakuwa na uhalali wa kufanya biashara Tanzania kwani hawakuwa wamepewa kibali na Kamishna Mkuu wa Kodi cha kuthibitisha utwaaji wao wa kampuni hiyo.

“Hivyo Kamati ililiambia Bunge kuwa PAP ni matapeli wa kimataifa waliopiga ganzi mfumo wa Serikali ya Tanzania kwa kutumia rushwa na hivyo kuhalalishiwa umiliki wa IPTL ili kuchota fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow BoT,” alisema Zitto.

Alisema katika hukumu yake ICSID imethibitisha kuwa PAP hakuwa mmiliki wa IPTL na hivyo alilipwa fedha za Tegeta Escrow kimakosa.

Katika hilo alisema hoja hiyo imethibitisha kile ilichowahi kushauri PAC na Bunge kwa ujumla lakini cha ajabu walipingwa vikali na Serikali ya awamu ya nne ambayo alidai iligeuka mtetezi wa PAP.

Katika hoja ya pili, Zitto alihoji iwapo PAP wangekuwa wamiliki halali wa IPTL walilipwa ziada?

“Hoja kubwa ya PAC ilikuwa ‘ni kwanini tulifanya haraka kutoa fedha kabla ya uamuzi wa kiwango gani kilipwe?’ Hoja hii ndiyo iliyochagiza kuwa mle ndani ya Tegeta Escrow kulikuwa na fedha za umma,” alisema Zitto.

Alisema uamuzi wa kukokotoa ulitolewa Februari, 2014 lakini katika mjadala mzima wa sakata la Escrow Serikali ilikataa kata kata kutekeleza uamuzi huo na hivyo kuumbuliwa na uamuzi wa sasa wa mahakama.

Alisema hoja iliyotolewa kupitia magazeti ya jana na wakili wa Tanesco, Richard Rweyongeza, ilikuwa ya PAC ambayo ilitokana na maagizo ya CAG .

Alisema hoja ya CAG ambayo ilikataliwa na Serikali na Tanesco ilikuwa ikielekeza Tanesco kukaa chini na SCB-HK kupiga hesabu upya jambo ambalo limesababisha jana Rweyongeza akiri kuwa shirika hilo liliwalipa zaidi IPTL.

Zitto alisisitiza kuwa uamuzi wa sasa wa  ICSID unaiweka nchi kwenye nafasi nzuri ya kulimaliza suala la IPTL ambalo alidai limekuwa likiumiza nchi kutokana na kutakiwa kulipa tozo ya kuzalisha umeme mara mbili ya kiwango tulichopaswa kulipa.

Kuhusu mmiliki mpya wa mitambo ya IPTL kupitia kampuni ya PAP, Singh Harbinder Sethi, Zitto alimtaja kama tapeli wa hisa alizochukua kupitia mitambo hiyo huku wamiliki wake wakiwa hawajulikani zaidi wakifahamika kwa jina la Simba Trusts ya Australia.

Pamoja na hayo yote, Zitto aliishauri Serikali kutekeleza hukumu hiyo bila kusita lakini pia kuiamrisha PAP kurejesha fedha zote za ziada ilizolipwa kutoka akaunti ya Escrow.

Alisema Serikali inapaswa kuitaka kampuni ya PAP kuilipa benki ya SCB-HK kutokana na hati iliyowasilisha Benki Kuu kwamba madai yoyote yakitokea katika IPTL, PAP ndio watalipa.

“Serikali pia inatakiwa kuchunguza na kuwashtaki maofisa wote wa Serikali walioshirikiana na Sethi kuchota fedha BoT,” alishauri.

Aliishauri pia Serikali kuilipisha faini Benki ya StanBic Tanzania kwa kushiriki kwenye vitendo vya kutakatisha fedha kufuatia miamala ya Escrow iliyoifanya.

Zitto pia alirudia ushauri ule ule uliowahi kutolewa na PAC ndani ya Bunge wa kufunga kabisa suala la IPTL kwa kuvunja mkataba na kuitwaa mitambo kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Natumai watu wenye nafasi za uongozi wa umma ambao maamuzi yao yamefikisha nchi hapa watachutama na kuondoka katika uongozi wa umma, tumefikishwa hapa na wizi na tamaa za watu madalali wa matapeli. Ninaamini Rais John Pombe Magufuli hatakubali nchi hii kuendelea kupigwa na matapeli,” alisema Zitto.

 

BASHE

Kwa upande wake Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, aliandika kupitia facebook akihoji aliyemleta Sethi nchini.

Bashe alikwenda mbali na kuhoji aliyemwagiza Gavana wa BoT kutoa fedha za Escrow.

“Je, wale waliokwenda Stanbic Benki Basement na kuchukua fedha na magari meusi walimpelekea nani? Je, nani anamiliki IPTL kwa asilimia hizo 70? Je, kule nje ilikosajiliwa wamiliki ni kina nani?” alihoji Bashe.

Kwa mujibu wa Bashe, suala la Escrow limekua ni hoja mjadala, mazungumzo, taarifa na masikitiko.

Alisema Escrow, IPTL ni wizi uliobarikiwa na kuhalalishwa kwa nguvu na matokeo yake ikawa dhana na mtindo mpya wa wizi.

Aliuelezea mtindo huo kwa kutoa mfano ambao dalali ananunua nyumba kwa pesa yako halafu anakukodishia kisha inagundulika alikuuzia nyumba ambayo haikuwa mali yake.

“Inabidi umlipe mwenye nyumba fedha tena ili uweze kuendelea kuikodisha nyumba ile ambayo awali ilinunuliwa kwa pesa yako. Mwisho unajikuta umelipia mara mbili nyumba ambayo siku ya mwisho anafaidika nayo dalali na wewe unaendelea kuwa mpangaji. Huu wizi ni ‘made in Tanzania,” aliandika Bashe.

Mbunge huyo alishangaa kuona kuwa katika sakata hilo bado unaendelezwa mtindo wa kuhangaika na watu wanaotumwa na kuwalinda wezi.

“Bado tumeendelea na mtindo ule ule wa kuhangaika na mrina asali ambaye alitumwa kurina asali akaweka kwenye madumu na kumkabidhi aliyemtuma huku yeye akiishia kupata ujira wa kulamba vidole.

“Kama nchi tuanze kuwatafuta walioagiza urinaji wa asali na kuchukua madumu ya asali tusisumbuke na warinaji ambao ujira wao ulikua ni kulamba asali iliyobaki kwenye vidole.

“Nasema hivi, kama nchi tutaifishe mtambo, kisha Sethi akamatwe atuambie mwajiri wake ni nani? Kisha tumtafute huyu aliyewatuma warina asali na yeye kupelekewa asali kwenye madumu hawa watendaji walitumwa tu,” alisema Bashe.

Hata hivyo, Bashe alipendekeza Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira ambaye pia alikuwa mmiliki mwenza wa IPTL, asiguswe wakiwamo wale waliofaidika na mgawo wake wa fedha alizopatiwa kutokana na umiliki wake wa asilimia 30.

 

KINGU

Kwa upande wake Kingu aliwafananisha watu walionyuma ya IPTL na genge hatari ambalo lipo tayari kuumiza na hata kuangamiza yeyote anayejaribu kugusa masilahi yao.

Kingu ambaye katika andiko lake lililokuwa likisambaa kwenye mitandao ya kijamii ametumia maneno ya Mungu, alisema kundi hilo ambalo lina nguvu katika vyombo vyote vya maamuzi na kwamba hata yeye linaweza kumuundia mpango wa kumwangamiza, alisisitiza akisema hata hivyo majira ya Mungu hayachezewi.

Kingu alimuomba Rais Magufuli asaidie watu wake ambao ni dhaifu katika dunia hii lakini wenye nguvu kubwa isiyoonekana katika mamlaka ya duniani.

Pia alilitaka Bunge kusimamia maamuzi yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,682FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles