23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

DPP amfungulia mashtaka uhujumu uchumi mtuhumiwa ubakaji, ulawiti

WAANDISHI WETU –Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, amesema ofisi yake imemfungulia mashtaka ya uhujumu uchumi, Ahmed Abdulkarim Mohamed kutokana na makosa ya kuwalaghai wanawake na kuwaingilia kimwili kinyume na matakwa yao.

Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Mganga alidai kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akiwarubuni wanawake ambao wengi ni wake za watu na wenye familia kwa minajili ya kufanya nao biashara, kisha kuwawekea dawa na kuwaingilia kimwili na kinyume na maumbile.

Alidai pamoja na vitendo hivyo, mtuhumiwa amekuwa akiwapiga picha ambazo huzitumia kuwatisha na kuwadai fedha ili asizitume mitandao ya kijamii, akijua kwa kuwa ni watu wenye heshima, waume na familia zao hawatakubali kuruhusu picha zao zisambae mitandaoni.

“Huyu jamaa amekuwa akiwarubuni kina mama wenye uwezo pamoja na raia wa kigeni, akishakutana nao anawalewesha kwa dawa kisha kuwabaka na kuwaingilia kinyume na maumbile, tayari waathirika ni wengi ambao tunawaomba wajitokeze,” alidai.

Alisema kutokana na aina ya vitendo walivyofanyiwa, kesi dhidi ya mtuhumiwa iliyofunguliwa Agosti 21, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itasikilizwa kwa faragha na haitaruhusiwa watu wengine kuwepo zaidi ya mtuhumiwa na walalamikaji.

Mganga alisema tayari walalamikaji watano wamejitokeza na kuna idadi kubwa zaidi ya walalamikaji ambao anawahakikishia kuwapo usiri iwapo watajitokeza ili kutoa ushahidi dhidi ya mtuhumiwa huyo.

Alidai mtuhumiwa amekuwa akitumia majina tofauti ya watu maarufu, likiwemo la Ahmed Abdulkarimu Mudhihir na wakati mwingine amewahi kujiita Mwamvita Makamba na amekuwa akifanya utapeli huo kwa wanawake wenye familia zao.

Alisema awali, mtuhumiwa alipelekwa Mahakama ya Kindondoni, lakini aliachiwa kwa dhamana na aliendelea kutekeleza uhalifu huo, hivyo alipobaini kuhusu tuhuma zake kwa kuwa anawajibika kulinda usalama na haki za watu na kuhakikisha hakuna anayebughudhiwa, aliamua kumfungulia mashtaka hayo ya uhujumu uchumi.

“Kutokana na vitendo vya kutumia picha za walalamikaji kuwadai fedha na anadaiwa kuiba fedha kwa baadhi ya walalamikaji, hivyo tumemfungulia kesi hiyo namba 85 ya uhujumu uchumi ambayo inaambatana na kesi namba 83 na 69 ya utakatishaji fedha na kesi hizi zote ziko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mganga alisema wamemkamata Ezekiel Warioba kwa tuhuma za kuendesha maudhui ya mtandaoni bila kuwa na leseni na tayari alikiri kosa lake katika Mahakama ya Kisutu, na amehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 5 na kutaifishwa kompyuta mpakato yake aina ya Apple na simu ya iPhone aliyokuwa akitumia.

Alisema Warioba alishtakiwa katika kesi namba 116 kwa mujibu wa kifungu cha 103 cha Sheria ya Maudhui ya Mitandaoni (EPOCA), na baada ya kukiri kosa mahakama ilitoa hukumu hiyo dhidi yake.

Mganga alisema pamoja na hukumu hiyo, bado mahakama inaendelea kumfuatilia kwa karibu na kuwaasa wanahabari kuacha kuendesha maudhui ya mitandaoni bila kuwa na leseni kwa kuwa sheria itachukua mkondo kwa yeyote.

Alisema pamoja na ofisi yake kuchukua hatua hizo, jukumu la kulinda amani na utulivu ni la kila mmoja, na si la vyombo vya ulinzi na usalama peke yake.

Alisema suala la usalama wa kila mtu, mali zake na haki ya kuishi bila kubughudhiwa si mambo ya kupuuzwa, na kila mtu anawajibika kukemea na kuchukua hatua pale anapoona haki za watu zinakiukwa.

Imeandikwa na Chelsea Tillya (UDSM), Erick Mugisha na Andrew Msechu

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles