31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama: Kesi ya Lissu iendelee

KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeamuru kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu iendelee.

Hatua hiyo imekuja baada ya hoja nane za pingamizi zilizowasilishwa na Serikali kukosa mashiko.

Mapingamizi hayo yaliyowasilishwa na mawakili wa Serikali zaidi ya 10 yalitupwa jana mbele ya Jaji Sirilius Matupa, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kukubaliana na hoja za Wakili wa Lissu, Peter Kibatala.

Akitoa uamuzi, Jaji Matupa alisema anakubaliana na hoja za Wakili Kibatala, kwamba hakukuwa na haja ya kuambatanisha uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge Lissu katika maombi yaliyopo mahakamani.

“Hoja zilizotolewa na wajibu maombi, hawawezi kutarajia utapata joto kwa kukaa kwenye friji, nashawishika na Kibatala kwamba hoja za kupinga mamlaka ya kisheria aliyopewa kaka yake Lissu kufungua kesi kwa niaba yanahitaji ushahidi na njia pekee ya kupinga kiapo ni kuwasilisha kiapo kinzani.

“Vigezo sita vilivyowasilishwa kupinga maombi haviwezi kuwa msingi wa kumaliza  kesi, lazima tusikilize kesi vizuri, matumizi ya pingamizi ni mapana sana, kama kuna hoja za kusikiliza katika shauri, pingamizi haliwezi kuwa sababu ya kuondoa kesi.

“Ukiondoa mapungufu yaliyopo katika hati ya kiapo, mahakama hii itasikiliza shauri hili, hoja zote za wajibu maombi zinatupiliwa mbali,” alisema Jaji Matupa.

HOJA ZA KIBATALA

Kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Kibatala, katika kupinga hoja za kutaka maombi ya mteja wake kutupwa, alidai kuwa hoja za wajibu madai hazina mashiko na akaiomba mahakama izitupilie mbali.

Alidai hoja ya kutokuambatanisha uamuzi wa Spika uliomvua ubunge Lissu ni kwamba hilo si hitaji la lazima la kisheria.

Kibatala alidai kwa mujibu wa Kanuni ya 5 ya Mwenendo wa Mashauri ya Mapitio ya Maamuzi ya Mamlaka za Kiserikali, hakuna mahali ambapo panataja kuwa ni lazima kuambatanisha uamuzi unaolalamikiwa katika maombi ya marejeo ya uamuzi wa mamlaka za kiserikali.

Alidai kwa mujibu wa Kanuni ya 4, hata waliozitunga hawakuweka hilo kama hitaji la lazima kwa kuwa wakati mwingine uamuzi wa mamlaka za kiserikali hufanyika kwa maneno tu na kutekelezwa.

Kuhusu hoja kwamba alichokifanya Spika halikuwa tangazo bali taarifa tu kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, kwamba kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kiko wazi, Kibatala alidai alichokifanya kina uamuzi ndani yake.

Alidai mwenyekiti wa NEC hawezi kwenda bungeni kungalia nani hayuko bungeni bila ruhusa ya Spika,

Kibatala alidai kwa upande wa mamlaka ya kisheria kwa kaka wa Lissu, Alute

Mughwai kufungua shauri hilo, hoja hiyo si ya kisheria kwa kuwa ni hoja inayohitaji ushahidi.

Kibatala alidai mwombaji alihukumiwa bila kusikilizwa, kwamba Spika alifanya uamuzi kwa tuhuma alizotoa mwenyewe.

Alidai hakuna sababu ya msingi katika uamuzi wa Spika Job Ndugai, alishindwa kuzingatia mambo ya msingi kabla hajatoa uamuzi.

“Spika hakuwa na nia njema, alimnyima Lissu haki yake ya kutibiwa na baadaye mshahara,” alidai.

HOJA ZA SERIKALI

Mawakili wa Serikali kwa upande wao kwa kuongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Clement Mashamba, waliwasilisha hoja nane za kupinga maombi hayo wakidai hayajakidhi vigezo vitano kati ya sita na kwamba aliyemwakilisha Lissu hana mamlaka ya kufanya hivyo, hivyo wanaomba yatupwe kwa gharama.

Akianza kuwasilisha hoja, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abubakar Mrisha alidai maombi yaliyowasilishwa mahakamani hayakidhi vigezo kwa sababu maombi au mashauri yanapofikishwa mahakamani lazima yawe yamezingatia vigezo sita.

“Kigezo cha kwanza kama maombi yaliletwa ndani ya miezi sita baada ya jambo husika kutolewa uamuzi, pili mwombaji awe anaelewa vizuri shauri, maamuzi yawepo kisheria, iwe hakuna namna nyingine ya kufanya kuhusu huo uamuzi, kama mahakama itasikiliza na kuona kuna haja ya kutoa uamuzi na sita maombi yanatakiwa yawe katika nia njema na wala si kwa kupotosha au kuwa na lengo la kujinufaisha binafsi.

“Mheshimiwa jaji, katika maombi yaliyopo mahakamani, ni kigezo kimoja walichotimiza, nacho ni kuyawasilisha maombi ndani ya miezi sita, ukitazama vigezo vitano vimekosekana.

“Hakuna maamuzi yoyote yaliyoambatanishwa katika maombi, ili mahakama iweze kuyapitia na kuyatolea uamuzi, maombi yoyote ni muhimu kisheria kuambatanisha maamuzi yanayomkumba.

“Katika kiapo cha Alute, alichoambatanisha ni nakala ya magazeti sio maamuzi, na kwamba hakuna uamuzi wowote uliotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, alichofanya ni kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Uchaguzi kwamba kuna kiti kiko wazi,” alidai na kuomba maombi yatupiliwe mbali kwa gharama.

Wakili wa Serikali Mkuu, Lucas Marunde, alidai waleta maombi wanaomba mahakama imlazimishe Spika alete tamko lake la kumvua ubunge Lissu mahakamani na wadai wapewe nakala.

“Mheshimiwa jaji kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi namba 37(3) sura ya 343 ya mwaka 2015 inasema mbunge anapokuwa hayupo katika kiti chake kwa mikutano mitatu mfululizo ya Bunge bila kutoa taarifa kwa Spika, anamfahamisha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwamba kiti kiko wazi,” alidai.

Alidai si Spika anayetoa tamko, Spika anatoa taarifa na hajishughulishi na kitu kingine chochote, katika kesi hiyo mwombaji hakuwepo katika kiti chake cha ubunge.

Wakili Marunde alidai hakuna maamuzi yoyote kutoka kwa Spika, hivyo wanaomba maombi yatupwe kwa gharama.

Hoja nyingine ziliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, George Mundepo ambaye anadai kwamba mleta maombi, Alute Mughwai hana sifa ya kufungua maombi hayo kwa niaba ya Lissu.

Anadai sheria inaruhusu madai kufunguliwa na muhusika au anayemwakilisha mwenye mamlaka kisheria, lakini shauri lililopo limewasilishwa na Tundu Lissu kupitia mwakilishi wake Alute Simon Mughwai.

“Kanuni zinaeleza wakati wa kuomba ridhaa maombi yasainiwe na mwombaji au mwakilishi wake, maombi yaliyopo mahakamani yameambatanishwa na hati ya kumpa mamlaka kisheria kumwakilisha Lissu kwa sababu kashindwa kufanya hivyo mwenyewe.

“Julai 9 mwaka 2019 Lissu kasaini hati hiyo akiwa Ubelgiji ikionyesha pia kiapo kimesainiwa na kupokelewa nchini humo, Wakili aliyeshuhudia Safolf Magay kasaini na kugonga muhuri kwa anuani ya Tanzania.

“Wakili hajaonyesha kibali alichopewa kufanya kazi nchini humo, kwa hoja hizo kunafanya kiapo cha Alute kuwa si halali, maombi si halali kwani yaliambatana na kiapo batili, hivyo yatupwe kwa gharama,” alidai.

Alidai Wakili Sadolf anafanya kazi nchini, hajawahi kuleta hati ya kiapo akionyesha alikwenda Ubelgiji na wala haikuonyesha kama wakili huyo alipata kibali kwa sheria ya Ubelgiji kufanya kazi nchini humo.

Lissu pamoja na mambo mengine anaomba zuio la muda la kuapishwa kwa Mbunge mteule Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu na maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge.

Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Maombi hayo dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba Kibali cha kufungua shauri la kupinga uamuzi huo.

Kwa mujibu wa maombi namba 18 ya mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.

Anaiomba mahakama hiyo itengue na kutupilia mbali uamuzi huo wa Spika Ndugai kumvua ubunge.

Mwombaji huyo anaomba mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa Mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa CCM.

Katika hati ya dharura, Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo, Mtaturu ambaye Julai 19 mwaka huu alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, ataapishwa kushika wadhifa huo.

Hivyo anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na masilahi yake yote yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.

Uamuzi wa kumvua ubunge ulitangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Juni 28, mwaka huu wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, huku akitaja sababu mbili.

Spika Ndugai alizitaja sababu hizo kuwa ni kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na sababu ya pili ikiwa ni kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo Spika Ndugai alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni Katiba ya Nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles