27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

DK. SHEIN, KINANA, MBOWE KUUNGURUMA DIMANI

Kinana mbowe shein

Na IS-HAKA OMAR- ZANZIBAR

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wanatarajiwa leo katika maeneo tofauti tofauti kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani, Zanzibar.

Kwa upande wa Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa kampeni hizo utakaofanyika kwenye Kiwanja cha Shule (Skuli) ya Fuoni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

Pamoja naye atakuwepo Kinana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai pamoja na viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali za taasisi hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Idara ya Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu, alipozungumza na vyombo vya habari juu ya maandalizi ya ufungaji wa kampeni za chama hicho.

Jabu alisema maandalizi ya kufungwa kwa kampeni hizo yamekamilika kupitia miongozo, ratiba na masharti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema Dk. Shein atawaeleza wananchi kuhusu sera, mikakati na mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo huku akiwataka wafuasi wa vyama kutofanya vurugu.

“Tunawaomba wafuasi wetu na wananchi kwa ujumla mjitokeze kwa wingi katika mkutano huo kesho (leo) ili muweze kusikiliza sera na mipango endelevu inayotekelezeka kwa vitendo itakayoelezwa na Dk. Shein pamoja na viongozi wengine,” alisema Jabu.

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe ambaye atafunga kampeni visiwani huo kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema wanatarajia kufanya vyema katika uchaguzi huo kwa kupata kata 21 kati ya 22 na ubunge katika Jimbo la Dimani.

“Tunaitaka Serikali iheshimu maamuzi ya wananchi, vyombo vya dola, wasimamizi wa uchaguzi wasifungamane na upande wowote bali wafungamane na upande wa sheria, hii imekuwa rai ya Chadema katika kila chaguzi lakini tumeona mara nyingi vyombo vya dola ikiwemo Tume yenyewe ya uchaguzi inavyotumika kupanga matokeo ya uchaguzi ama maamuzi ya wananchi,” alisema Mbowe.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani Unguja, Hafidh Ali Twahir, kufariki dunia mwaka jana akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake bungeni mjini Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles