Dk. Shein azindua vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi

0
478

MWANDISHI WETU-ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema matumizi ya vitambulisho vipya vya Mzanzibari mkaazi yataiwezesha Serikali kuweka na kuhifadhi kumbukumbu za matukio ya watu wote katika Daftari la Usajili na Utambuzi.

Dk. Shein aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kadi mpya za kielektroniki za Mzanzibari mkaazi, katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil, Kikwajuni mjini Unguja.

Alisema vitambulisho hivyo vitasaidia Serikali, taasisi na watu binafsi kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zenye mnasaba na huduma za maendeleo ya kijamii.

Aidha, alisema kuwepo kwa mfumo huo wa matumizi ya vitambulisho vipya utaisadia Serikali katika kuwatambua watu wanaostahiki kupata haki za msingi, kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984.

“Itawezesha kumtambua mtu anayestahiki kupata haki yake kama vile malipo ya pensheni, haki za matibabu, kujiunga na masomo na nyinginezo,”  alisema.

Dk. Shein alisema kutokana na vitambulisho hivyo, Serikali itapata urahisi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato, hivyo kuimarisha huduma muhimu za kijamii, ikiwemo afya, elimu, barabara, ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Alisema kimsingi Serikali inapaswa kuwa na nyenzo katika udhibiti wa amani na utulivu wa watu wake, hivyo ni dhahiri vitambulisho vipya vitakavyotumika hivi sasa ni vyenye ubora wa hali ya juu na uwezo wa kuhifadhi taarifa  nyingi za mtumiaji.

Alieleza kuwa vitambulisho hivyo vimetengenezwa kwa teknolojia ambayo si rahisi kughushiwa, vikiwa na uwezo mkubwa wa kiusalama wa taarifa za mtumiaji, akibainisha kutumika katika nchi kadhaa duniani.

Dk. Shein alitoa wito kwa wakaazi wote wa Zanzibar waliofikia umri wa miaka 18 kwenda kujisajili ofisi za Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii zilizopo wilaya zote nchini, sambamba na wale ambao bado hawajajiandikisha kufanya hivyo.

Aidha, aliwataka watendaji wanaohusika na utayarishaji wa vitambulisho hivyo kuwa makini na waangalifu katika utoaji wake.

Vile vile aliwataka wakuu wa mikoa kusimamia vizuri taarifa za uhakiki wa watu walioko katika maeneo yao, kuanzia ngazi za shehiya, wadi na wilaya ili kuhakikisha wanawatambua pamoja na taarifa zao zilizo sahihi.

“Ni muhimu mlifanyie mapitio daftari la wakaazi katika shehiya, ambalo ndio msingi wa uthibitisho wa kujua taarifa za utambuzi na makazi ya watu waliomo katika maeneo yenu,” alisema.

Dk. Shein aliwataka wananchi kutambua jukumu la kuisadia Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii katika kutambua wakaazi wa maeneo yao badala ya kuiachia jukumu hilo pekee.

Aidha, aliwataka wananchi kuondokana na tabia ya kutumia njia za mkato katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo, akibainisha hatua hiyo imekuwa chanzo cha kuibua rushwa.

“Naendelea kukunasihini watendaji wote wa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar, mfanye kazi zenu kwa uadilifu, uzalendo na mfungamane na misingi ya haki na sheria pamoja na kufuata taaribu zilizowekwa katika kuendesha ofisi,” alisema.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Haji Omar Kheir, aliwataka wananchi wote wenye sifa za kisheria kufika katika vituo vya usajili vilivyopo kila wilaya nchini.

Alisema kitambulisho kipya cha Mzanzibari mkaazi ndicho kitakachotumika katika upatikanaji wa huduma mbalimbali muhimu kama vile upatikanaji wa leseni, miamala ya fedha, mahitaji katika taasisi za umma pamoja na zile zenye mahitaji ya vitambulisho.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili na Matukio ya Kijamii Zanzibar, Dk. Hussein Khamis Shaaban, alisema ofisi hiyo itaendelea na mikakati ya kusajili na kuwapatia vitambulisho wananchi wote wenye sifa za kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here