25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Daktari bingwa aeleza kiharusi kinavyomaliza vijana, watoto

AVELINE KITOMARY   -DAR ES SALAAM

DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Patience Njenje, amesema ugonjwa wa kiharusi unashika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo duniani kote.

Amesema mbali na wazee, pia vijana na watoto wanapata ugonjwa huo kwa wingi.

Dk. Njenje alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), asimilia 11.8 ya vifo duniani vinatokana na kiharusi, huku nafasi ya kwanza ikichukuliwa na magonjwa ya moyo.

Alisema pia kwa mujibu wa takwimu hizo, ugonjwa wa kiharusi ni wa tatu kwa kusababisha ulemavu kwa asilimia 4.5 ya watu duniani kote.

Hata hivyo Tanzania tafiti zinaonyesha kati ya watu 100,000, watu 108 hadi 316 wana ulemavu uliosababishwa na kiharusi.

Dk. Njenje alisema hayo ikiwa ni kuadhimisha Siku ya Kiharusi Duniani ambayo hufanyika kila Oktoba 29.

Alisema kundi lililoathirika zaidi ni watu wenye miaka 65, huku vijana na watoto nao wakikumbwa na ugonjwa huo.

“Kiharusi ni ugonjwa unaotokea pale ubongo unapokosa damu kwa dakika chache, ugonjwa huu umekuwa ukisababisha vifo na pia ni ugonjwa wa tatu unaosababisha ulemavu,” alisema Dk. Njenje.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa wa kiharusi wanachelewa kufika hospitali kutokana na kuwa na uelewa mdogo kuhusu ugonjwa huo.

“Ugonjwa huu tumezoea kuona ukiwapata watu wazima, lakini sasa inaonekana kuwapata watu wenye umri wa chini ya miaka 45.

“Hospitali ya Muhimbili inapokea wagonjwa kati ya watatu hadi wanne kwa siku ambao wengi wao wanafika kati ya siku tatu hadi saba baada ya kupata kiharusi.

“Hivyo asilimia kubwa ya wagonjwa wanafika hospitalini wakiwa tayari wameshachelewa, kwa kawaida ugonjwa huo ukiwahi hospitali kabla ya masaa sita, unaweza ukatibiwa na ukapona,” alibaisha Dk. Njenje.

Kwa mujibu wa Dk. Njenje, kisababishi kikubwa cha kiharusi ni shinikizo la juu la damu kwa asilimia 80 huku  magonjwa ya moyo yakichangia pia.

“Vingine ni selimundu, matumizi ya dawa za kulevya, matumizi mabaya ya pombe, ulaji wa vyakula vya mafuta, ugonjwa wa kisukari, uzito mkubwa na VVU,” alisema.

Dk. Njenje alieleza kuwa kinga ya ugonjwa huo ni watu kupima afya mara kwa mara ili kugundua magonjwa yanayoweza kusababisha kiharusi na kuyadhibiti mapema.

“Udhibiti wake ni kwa kunywa dawa na kubadilisha mfumo wa maisha kwa kufanya mazoezi angalau dakika 30-45 kila siku, kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na mafuta kwenye chakula,” alisema Dk. Njenje.

KIHARUSI KWA WATOTO

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Zameer Fakih alisema watoto wengi wanaopata kiharusi ni wale wanaougua ugonjwa wa selimundu na wachache wa ugonjwa wa moyo.

Dk. Fakih alisema takwimu za kidunia zinaonyesha mtoto mmoja kati ya 4,000 wanaozaliwa kila siku hupata kiharusi.

“Kugundua tatizo la kiharusi kwa mtoto tunafanya  vipimo vya CT scan na kujua historia, kiharusi kinaanza kuonekana na baada ya watoto kuanza kufanyiwa  vipimo vya ubongo sababu kubwa ni mishipa ya damu kuziba.

“Watoto wenye selimundu ndio wanapata tatizo la kiharusi.

“Julai 2017 hadi Juni 2018 watoto 33 walikuwa na kiharusi na katika kliniki kwa wiki kati ya mtoto mmoja mpaka watatu wanakutwa na tizo la kiharusi.

“Ugonjwa mwingine ni ule wa moyo, tatizo la mirija ya moyo kuziba. Lakini hii ni kwa asilimia ndogo inasababisha kiharusi ila wengi ni wale wa selimundu,” alisema Dk. Fakih.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles