23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaume watakiwa wasinyonye maziwa ya mama anayenyonyesha

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Lishe kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Grace Moshi, ametoa rai kwa wanaume wenye tabia ya kunyonya maziwa ya mama kuacha ili kuwapa nafasi watoto kupata lishe bora.

Hayo yametokana na mtindo wa baadhi ya kina baba kulazimisha kunyonya maziwa ya mama huku watoto wakikosa lishe bora kutokana na kiwango cha maziwa kupungua.

Grace alisema mtoto ili awe na afya njema, anahitajika kunyonya maziwa ya mama kwa miezi sita bila kula chochote.

Alizungumza hayo jana Dar es Salaam na waandishi wa habari wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa mawaziri wa afya wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),  

“Mara kwa mara nimeona kina mama wakilazimisha kuwapa watoto uji au chakula kingine ikiwemo maji, maziwa haitoshi, hii si sawa, maziwa ya mama ni chakula kilichokamilika,” alisema Grace.

Alitolea mfano walipokuwa katika ziara za kikazi kuhamasisha unyonyeshaji watoto wachanga, alisema waliwahi kupata maswali kutoka kwa kina mama ikiwa maziwa yatawatosha watoto kwani waume zao wanalazimika ziwa moja liwe la mtoto jingine la kwao.

“Msicheke hili, mnaweza kuona kama masihara, lakini wapo kina baba wananyonya maziwa ya wake zao. Tusaidieni kuhamasisha ili hili lipungue,” alisema.

Grace alisema mtoto anapozaliwa anatakiwa kunyonya maziwa ya mama tu kwa kipindi cha miezi sita bila kupewa kitu kingine ili kumfanya awe na lishe nzuri.

Kuhusu lishe nchini, alisema kama nchi imepiga hatua kubwa katika eneo la lishe ukilinganisha na huko nyuma.

Alisema malengo yaliyowekwa duniani ni kwamba suala la lishe lisiwe zaidi ya asilimia 30 ambapo kwa Tanzania iko katika asilimia 32 ambayo ni juu ya lengo ambalo limewekwa katika eneo hilo.

Hata hivyo alisema kwa Tanzania katika eneo la lishe ilikuwa na changamoto, lakini kupitia mikakati ya wizara imefanikiwa kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles