28.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

Dk. Shein ataka utafiti uvuvi, kilimo

Na Mwandishi Wetu – Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuweka kipaumbele katika kufanya utafiti unaohusiana na sekta za wizara hiyo kwa kuzingatia mazingira halisi na mahitaji ya wananchi, sambamba na matukio mbalimbali ikiwemo milipuko ya maradhi ya mazao na mifugo.

Dk. Shein ametoa wito huo jana wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya Nanenane Chamanangwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema kupitia utafiti huo, wizara itaweza kupata taaluma na utaalamu mpya na kuwafundisha wakulima, akibainisha kuwepo masuala kadhaa yanayohitaji kufanyiwa utafiti.

Akitolea mfano, Dk. Shein alisema yanapotokea maradhi ya mifugo au mazao, wizara hiyo haipaswi kuishia kupiga dawa pekee, bali inatakiwa kuwa mstari  wa mbele katika kutafuta chanzo cha maradhi hayo, kubuni njia za kuyaondoa pamoja na kuonyesha njia ili yasiweze kutokea tena.

Alisema katika siku za hivi karibuni wakulima wengi wamejikita katika kilimo cha mazao mbalimbali ya biashara, ikiwemo matikitiki, tungule, matango na viazi kupitia matumizi ya mbolea za kemikali.

Dk. Shein alisema pamoja na uzuri wa kuendeleza kilimo hicho, ipo haja ya kufanya uchunguzi wa kitaalamu kuhusu faida na hasara za kilimo cha aina hiyo, hasa katika afya ya udongo, ardhi, mazingira pamoja na virutubishi katika mazao yanayotokana na kilimo hicho.

Alisema tangu asili kisiwa cha Pemba kinasifika kwa kuwa na ardhi yenye rutuba nzuri, jambo lilolosababisha kupatikana mavuno mazuri kupitia matumizi ya mbolea za asili (kilimo hai), hali ambayo hivi sasa imebadilika.

“Mimi naamini kilimo hai kwa kutumia mbolea za asili bado kina umuhimu mkubwa ndani ya jamii yetu, hata hivyo suala la kukiendeleza na upatikanaji wa masoko ya mazao yanayotokana na kilimo hicho linahitaji kufanyiwa utafiti,” alisema Dk. Shein.

Alisema wengi duniani wanaendelea kula vyakula vinavyotokana na kilimo hai kutokana na ladha ya asili pamoja na kuwepo uwezekano wa kupungua athari za kemikali.

Dk. Shein alisema suala la utafiti huzijengea jina taasisi pamoja na nchi katika medani za kitaalamu duniani, kwa kuzingatia mazao yatokanayo na kilimo hai huuzwa kwa bei ya juu sana, ikilinganishwa na mazao yanayotumia mbolea za kemikali.

Alisistiza umuhimu wa wizara  kuwahamasisha wananchi kuhusu uanzishaji wa mashamba ya viungo (spice farm), ikiwa ni hatua ya kuvutia watalii pamoja na kuwapatia wananchi kipato cha kuendesha maisha yao.

Dk. Shein alisema mashamba hayo yanaweza kuwa sehemu za huduma za vyakula vinavyotumia viungo, na wageni wataweza kuona uhalisia wa matumizi yake.

“Mnaweza kuwahamasisha wananchi kuanzisha sehemu za maonyesho ya wanyama wetu wa asili zitakazokuwa vivutio muhimu kwa wazee na watoto hasa siku za sikukuu, kuna baadhi ya wanyama kama kima na tumbili wanaweza kuwa kivutio kikubwa kwa watalii na wananchi,” alisema Dk. Shein.

Katika hatua nyingine, Dk. Shein alisema hatua ya Serikali kuanzisha maonyesho maeneo ya Dole-Unguja na Chamanangwe- Pemba, inatoa fursa kwa wananchi kutambua shughuli zinazofanywa na taasisi zinazoshiriki, ikiwa njia mojawapo ya kujitangaza na kupata masoko.

Alisema pamoja na wananchi kutambua umuhimu wa kufanyika maonyesho hayo, idadi kubwa ya washiriki katika hafla hiyo ni uthibitisho wa kuunga mkono na kuthamini juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta za Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, kupitia mipango mikuu ya maendeleo ya Zanzibar na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa CCM (2015-2020), ambayo imefikiwa kwa asilimia 95.

Dk. Shein alisema Serikali imejipangia mikakati maalumu kwa lengo la kuongeza uzalishaji  kupitia mbinu bora, teknolojia ya kisasa, ujenzi wa miundombinu, utoaji wa thamani na upatikanaji wa masoko, pamoja na mitaji na uhifadhi wa chakula ili kuongeza tija, kukuza uchumi na kuondoa umasikini.

Alisema kuwa hatua hiyo imeifanya Serikali kuongeza bajeti ya kilimo, ambapo  mwaka 2020/21 imeongezwa kutoka Sh bilioni 88.17 (2019) hadi  Sh bilioni 129.86 (2020), ikiwa sawa na asilimia 47.3.

Dk. Shein alisema mazao mengine ya chakula, matunda na mbogamboga nayo yaliongezeka kutoka tani 289,481 (2010) hadi tani 404,285 mwaka 2020, akibainisha zao la muhogo kuvunwa tani 137,692.7, huku tani 65,321.2 za ndizi zikivunwa ambapo kisiwa cha Pemba zilivunwa tani 23,970.5

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,637FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles