25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mashindano ya kuchimba makaburi yanavyotikisa Ulaya

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

UKISIKIA duniani kuna mambo basi malizia kwa kusema ‘tembea ujionee’. Wakati uchimbaji makaburi ikionekana ni kazi ya ajabu hata ikiwa ngumu kuwashawishi vijana wa kileo kujihusisha nayo wapo walioiona kuwa ni fursa kwa kuianzishia mashindano.

Kazi hiyo imeanza kujizolea umaarufu mkubwa katika mataifa mbalimbali ya Ulaya hasa kwa miaka ya hivi karibuni, kutokana na mashindano mbalimbali ya uchimbaji kaburi yanayofanyika.

Kwa kuanzia, hiyo utaipata huko Trencin nchini Slovakia ambako sasa wananchi wake hawashangai kusikia mashindano ya aina hiyo.

Ieleweke kuwa Slovakia si nchi pekee yenye mashindano hayo, kwani itakumbukwa kuwa hata Hungary nayo na lilipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2016, timu 18 zilishiriki mjini Debrecen.

Ni katika shindano hilo ambalo mshindi wake alikwenda Slovakia, jumla ya timu 18 zilishindana huko Hungary, ambapo kigezo kikubwa cha kaburi sahihi ilikuwa ni lenye upana wa futi 2 na inchi 7, urefu wa futi 6 na inchi 6 na kina cha futi 5 na inchi 3.

Kama ambavyo huwa kwenye mchezo wa tenesi wakati mwingine shindano la Slovakia kila timu huwa na watu wawili ambao kwa pamoja hushirikiana kuhakikisha kaburi linakamilika ndani ya muda mfupi.

Shindano linapoanza, kila timu huwa na mbinu zake za ushindi – kama mmoja atachimba na mwingine kuondoa udongo au watafanya vinginevyo ili mradi kuibuka washindi mbele ya wapinzani wao ambao nao watakuwa kwenye eneo lao.

Ukija kwa Slovakia, moja kati ya masharti ya kila timu ni kuhakikisha hakuna kifaa cha kisasa kilichotumika kuchimba zaidi ya chepe na sururu, tofauti na inavyokuwa Hungary kwani kule vifaa kama shoka huwa vinaruhusiwa, kwa mujibu wa gazeti la Guardian.

Ili kumpata mshindi kwa njia ya halali na kuepuka malalamiko kutoka kwa wenzao, shindano huwa na jopo la majajaji ambao kimsingi nao huwa si wageni kwenye kazi hiyo ya uchimbaji makaburi.

Majaji wanatakiwa kuwa na ujuzi wa kutosha juu ya kaburi bora, kigezo kikubwa ikiwa ni lenye kina cha futi 5, urefu wa futi 6.5  na upana wa futi 3. Hiyo ni kwa mujibu wa vigezo vya kule Slovakia, ambavyo vinatofautiana na ilivyo Hungary.

Mashindano ya Slovakia yanayotajwa kuwa ndiyo makubwa zaidi, hushirikisha timu kutoka nchini humo, pia zingine za Poland, Hungary na Jamhuri ya Czech.

Baada ya kuchimba, si tu majaji humtangaza mshindi, bali vigezo hivyo hufuatatiwa na mmoja kati ya watu waliopo kwenye jopo lao kujaribu kwa kuingia kaburini, kana kwamba mtu aliyefariki.

Aidha, katika shindano hilo ni kawaida kusikia yakiibuka malalamiko kutoka kwa baadhi ya washiriki, hasa wale walioshindwa kufanya vizuri. Hao mara nyingi hulalamikia sehemu waliyopewa kuchimba, wakisema ilikuwa ngumu kutokana na kuwa na mawe na kokoto.

Ladislav mwenye umri wa miaka 43 na kaka yake Csaba Skladan (41), wamewahi kuibuka kidedea katika mashindano ya Slovakia mwaka 2016, wakitangazwa kuwa ndiyo wachimbaji bora wa makaburi barani Ulaya baada ya kutumia sekunde 54 pekee kuchimba lenye vigezo sahihi vilivyotakiwa na majaji.

Baada ya kaburi lao kutajwa kuwa ndilo lenye mvuto zaidi kuliko mengine, Skladan alisema; “Nimefurahi tumeshinda ni jambo zuri kwetu baada ya miaka 15 kwenye kazi hii (ya kuchimba kaburi),”.

Lakini je, nini lengo la ujio wa mashindano hayo barani Ulaya? Ni kwamba kazi zimekwisha kiasi kwamba wamegeukia huko? 

Msemaji wa shindano hilo la Slovakia, Christian Striz, anasema; “Lengo ni kujaribu kupunguza huzuni iliyopo kila watu wanapozungumzia msiba, badala yake lionekane ni jambo la kawaida tu kwamba linaweza hata kufanyiwa mzaha.

Striz anaongeza kuwa shabaha ya shindano hilo ni kuipa heshima kazi ya uchimbaji makaburi baada ya kubaini kuwa wanaofanya shughuli hiyo wamekuwa wakidharauliwa.

 “Lengo ni kuonesha watu ilivyo kazi ngumu kuchimba kaburi.”

Julie Hillman, mmoja kati ya wanawake wachache nchini Uingereza wanaofanya kazi ya kuchimba makaburi anatilia mkazo kauli ya Striz akisema; “Watu wanafikiri kuwa uchimbaji makaburi ni ajabu lakini haiko hivyo.

Naye Iren Kari aliyeshiriki katika uandaaji wa shindano la Slovakia, aliliambia Shirika la Habari la AP kuwa wanataka kuyafanya mashindano hayo kuwa maarufu zaidi ulimwenguni ili kukabiliana na wale wanaoidharau kazi ya kuchimba makaburi.

Lakini, Kari anahitimisha makala haya kwa kuibua changamoto kubwa inayowakumba katika harakati zao za kuifanya kazi ya kuchimba makaburi kuheshimika kupitia mashindano wanayoandaa. 

“Bado kuna changamoto ya kuwapata vijana wanaoweza kuchukua nafasi ya wale wazee wanaokaribia kuachana na kazi hii,” alisema Kari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles