22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango atoa siku 14 gharama za usafirishaji mizigo ATCL, apokea ndege mpya

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango ametoa maagizo matano huku akimtaka Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kufanya uchambuzi wa gharama za usafirishaji wa mizigo katika ndege ya Air Tanzania ndani ya siku 14.

Maagizo hayo ametoa Oktoba 3, jijini Dar es Salaam na Dk. Mpango wakati wa hafla ya mapokezi ya ndege aina ya B 737- Max 9 yenye uwezo wa kubeba abiria 181 na ndege nyingine mbili za mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT) uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini na taasisi.

Amesema amepokea changamoto za gharama kubwa ya usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi katika viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro na Abeid Aman Karume Zanzibar ikilinganishwa na viwanja vya nchi jirani.

“Ninawaaelekeza Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Fedha washirikiane na wenzao wa Zanzibar ili kuchambua na kubaini kiini cha changamoto hiyo na kupendekeza hatua zinazopaswa kushughulikiwa.

“Tazameni hizo tozo na kodi mbalimbali, ikiwemo ‘Navigation, fees’ mfanye uchambuzi wa uhakika ndani ya siku 14 kuanzia leo na mlete mapendekezo serikalini,” amesema Dk. Mpango.

Amesema serikali haitovumilia uzembe wowote utakaojitokeza tena ndani ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kama ilivyowahi kuwa ndani ya miaka ya nyuma.

“Bado kuna malalamiko ya wateja wa ATCL kuhusu huduma za usafiri ikiwemo kuhairisha safari au kusogeza mbele muda wa kusogeza safari na kuna lele nyingi sana hivyo baada ya kupokea ndege hiyo matarajio ya Watanzania ni kuwa sasa ATCL watamaliza kero hiyo,” amesema Dk. Mpango.

Katika hatua nyingine, Dk. Mpango amesema ameridhishwa na hatua iliyofikia katika utekelezaji wa makubaliano ya awali ikiwemo kufanya tathmini ya upanuzi wa uwanja wa ndege Terminal II kitaalamu ili kuandaa mkataba wa usanifu wa ujenzi pamoja na tathmini ya sampuli za udongo kutoka eneo la mradi.

“Hivi sasa mradi wa uboreshaji na upanuzi wa jengo la pili la abiria katika kiwanja Cha Julius Nyerere uweze kuanza rasmi na ninauelekeza uongozi NIT, marubani wakufunzi na marubani wanafunzi wakazitunze ndege hizo ambazo zinanunuliwa kwa ajili ya kufundishia marubani ili ziweze kudumu na kuendelea kufundishia marubani walio wengi zaidi,” amesema.

Amemuelekeza Profesa Mbarawa kuangalia Chuo cha NIT kibajeti kuanzia mwaka ujao wa fedha ili maombi yao ya ndege nyingine mbili ambazo zina Injini mbili ziweze kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

WAZIRI MBARAWA

Awali, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliahidi kutekeleza majukimu yake kwa ufanisi kwa maslahi ya nchi.

Amesema ndege hiyo inaongeza mtandao wa biashara kati ya ATCL na nchi nyingine na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Aidha, ametangaza kiwanja cha ndege cha Dodoma kuanza kufanya kazi kwa saa 24 kuanzia jana huku wakiweka mkakati wa kuweka taa katika viwanja vya Iringa na Songea kuviwezesha kufanya kazi kwa saa hizo.

Akizungumza baada ya kuwasili kwa ndege hiyo, Mtendaji Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijengea ATCL kutoa huduma shindani nchini.

Amesema ndege iliyowasili inauwezo wa kubeba abiria 181 ni ya masafa ya kati na kuruka kwa saa nane bila kutua.

Amesema kuwasili kwa ndege hiyo kunaiwezesha ATCL kuwa na ndege 14 hivyo aliwataka Watanzania kujiandaa kupokea ndege nyingine mbili kabla ya mwishoni mwa mwaka huu.

“Katika mwaka wa fedha 2016-2017 ATCL ilipokea abiria 106,138 na mwaka 2021-2028 walikuwa milioni 1.7, mapato yaliyopatikama mwaka 2022-2023 ni Sh bilioni 372.8 na kupitia ndege ya mizigo kuanzia Juni mwaka huu ilibeba Tani 337 huku matarajio yakiwa Tani 468,” amesema Matindi.

MKUU WA CHUO NIT

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Usafirishaji Tanzania(NIT), Profesa Zakaria Mganilwa, alisema Serikali imekuwa inathamini mchango wa sekta ya usafirishaji nchini.

Amesema ndege mbili za injini moja aina ya Cessna Skyhawk 172 kwa Chuo cha NIT ndege moja imenunuliwa Sh bilioni 1.2 jumla ya zote ni Sh bilioni 4.4

“Tanzania Bado inakabiliwa na chagamoto ya uhaba wa wataalamu wa ndege kwani wanaorusha ndege kubwa nchini ni 304 ambapo wazawa ni asilimia 43 tu,” amesema Profesa Mganilwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles