24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Wakulima Buchosa walia na bei ya mbegu

Na Clara Matimo, Mwanza

WAKULIMA wa mahindi katika halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wamelalamika kupanda kwa bei ya mbegu za mahindi aina ya DK 777, DK 31 na DK 89 kutoka Sh 12,000 msimu uliopita hadi Sh 18,000 msimu huu wa kilimo jambo ambalo linakwamisha juhudi za Serikali kuiinua sekta ya kilimo na kutokomeza tatizo la njaa.

Wakizungumza na Mtanzania Digital kwa nyakati tofauti katika halmashauri hiyo, baadhi ya wakulima hao wameiomba Serikali kupunguza changamoto hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na wafanyabiashara wanaotaka faida kubwa baada ya kugundua mbegu hizo zinapendwa na wakulima.

Mkulima, Amos Bush kutoka Kata ya Bukokwa, amesema msimu uliopita mfuko mmoja wa mbegu hizo wenye ujazo wa kilogramu mbili walikuwa wanaupata kwa wastani wa Sh 12,000 hadi 13,000 lakini kwa sasa wanalazimika kuununua kwa wastani wa Sh 17,000 hadi Sh 18,000.

“Naiomba serikali kuweka msimamo wa bei maana kabla ya msimu wa kilimo kuanza mbegu huwa na bei moja lakini msimu wa kilimo unapoanza bei hulipuka,  asubuhi bei hii jioni hii kunakuwa hakuna bei maalumu na inapanda kiholela, hata sisi tunashindwa kuelewa ni kitu gani kimesababisha bei kupanda kiasi hicho,” amesema Bush.

Naye, Elizabeth James mkulima Kata ya Nyehunge na Tindalwesile Richard wa kata ya Bukokwa wameitaka Serikali kushughulikia suala hilo ili kila mkulima wilayani humo alime kwa tija na kunufaika kiuchumi kwani kwa sasa wanashindwa kulima eneo kubwa kutokana na kushindwa kumugu gharama za mbegu.

Mkulima William Katinde amesema: “Mbegu za mahindi zimepanda sana bei kwa maana hii ni changamoto kwa mkulima wa kawaida hawezi kununua na ataendelea kulima kilimo kisichokuwa na manufaa. Wanatuletea mbegu ni suala zuri sana lakini kutokana na bei kama mkulima ana heka 10 inamaana ataingia gharama kubwa sana,”amesema.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo Kata ya Nyehunge, Abel Sato amesema wafanyabiashara wamepandisha bei ya mbegu hizo kutokana na mahitaji kuwa makubwa kwani mbegu hizo ni nzuri zinavumilia ukame, zinatoa mavuno mengi na hazishambuliwi na magonjwa kwa urahisi hivyo wakulima wengi wanazihitaji.

“Siku zote wafanyabiashara hutafuta fursa, sasa kwa kuwa wameona aina hiyo ya mbegu inapendwa sana baada ya wakulima kupata elimu juu ya umuhimu wa kutumia mbegu bora ili wavune mazao mengi ndiyo wamepandisha bei,” amesema Sato.

Afisa Kilimo Kata ya Bukokwa, Jackson Masatu amesema kupanda kwa bei ya mbegu hizo za mahindi imekuwa ni changamoto kwa wakulima wa kata yake maana kuna wengine walipanga kulima heka nyingi lakini imebidi waahirishe kutokana na kushindwa kumudu gharama za mbegu.

“Kawaida heka moja mkulima akipanda vizuri kwa mistari itamgharimu kilo nane hadi 10 sasa kwa ambaye kipato chake ni kidogo inakuwa vigumu kupata fedha hizo na kununua mbegu,” amesema Masatu.

Akitolea ufafanuzi sababu za kupanda kwa bei ya mbegu hizo, Afisa Kilimo Halmashauri ya Buchosa, Nestory Mjojo amesema serikali haina cha kufanya kuwazuia wafanyabiashara kupanga bei zao  maana hilo ni soko huria na wafanyabiashara wanaifanya kama biashara zingine.

“Lakini kwa kuwa wajibu wa serikali ni kutatua changamoto za wananchi wake, tayari tumekwishatenga bajeti ya Sh milioni 21 tumekwishaandika  dokezo tunaendelea na taratibu za manunuzi   kwa ajili ya kununua mbegu na kuwauzia wakulima kwa bei ambayo haitawaumiza  hivyo nawaomba wakulima wavumilie kidogo changamoto hiyo tutaitatua muda wowote kuanzia sasa,” ameeleza Mjojo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles