27.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango aiomba Benki ya Dunia kusaidia zaidi kilimo

Na Mwandidhi wetu-Dar es Salaam

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameiomba Benki ya Dunia (WB) kujikita zaidi katika kusaidia sekta ya kilimo nchini ili kuweza kuwainua kiuchumi wakulima, hasa wale wa kati na wadogo.

Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa jana, ilisema Dk. Mpango aliyasema hayo wakati wa kikao cha majadiliano na timu ya WB ambayo inafanya kazi nchini Tanzania na wengine kutoka Makao Makuu ya benki hiyo nchini Marekani. 

Dk. Mpango alisema katika mkutano huo walipitia utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na benki hiyo nchini na kujadili miradi inayoanza kufikiriwa kwa utekelezaji kwa mwaka unaokuja.

“Moja ya vitu vilivyonifurahisha mwaka jana kwenye mjadala, niliwaaomba sana kwamba hatuwezi kuendelea kuitaka Benki ya Dunia isaidie kwenye miradi mingine tu, ni lazima nguvu kubwa ielekezwe kwenye kilimo, kwa sasa  msaada wake katika kilimo ni kidogo sana,” alisema Dk. Mpango.

Aidha Dk. Mpango alielezea dhamira ya Tanzania kushirikiana na benki hiyo ili kuanzisha programu itakayohakikisha tija inapatikana kwenye sekta nzima ya kilimo na mifugo.

 Dk. Mpango alisema WB imeridhishwa na kasi ya mabadiliko yanayofanyika katika sekta ya kilimo kwa maana ya uzalishaji kuongezeka, lakini vile vile  wakulima wa kati wamezidi kuongezeka. 

Pia alisema Benki ya Dunia imeshafanya utafiti wao wa kutosha ambao umeonyesha kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo kwa maana ya uzalishaji kuongezeka.

 Aliishukuru kwa kukubali tena kuleta timu ya wataalamu nchini, ambayo itakaa na sekta nzima ya kilimo na ufugaji ili kuona ni namna gani itasaidia kuinua sekta hiyo na  kuwasaidia wakulima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles