31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali Mwananyamala kumaliza tatizo kinamama kulala chini

AVELINE  KITOMARY NA BRIGITHA MASAKI-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amemtaka mkandarasi anayejenga jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, kukamilisha ujenzi  kabla Desemba 30 ili liweze kupunguza msongamano kwa kina mama.

Jengo hilo la ghorofa tano linalogharimu Sh bilioni 2.1, litapunguza msongamano katika hospitali hiyo ambayo wanaojifungua kwa mwaka ni 120,000 huku uwezo wake ni kuhudumia kina mama 50,000 hadi 60,000. 

 Akizungumza wakati alipotembelea hospitali hiyo, Makonda alisema jengo hilo litakalokuwa na vifaa vya kisasa, linatakiwa kuwa na vitanda 200. Kwa sasa vipo 100.

 “Baada ya kumweleza Rais Magufuli kuwa tuna changamoto Mwanyamala ya wodi ya kina mama, alitoa Sh bili 2.1 ya kukamilisha jengo na tunaenda kuongeza vitanda 100 kwa ajili ya kina mama kujifungulia. Usumbufu wa kujifungulia chini unaondoka sasa.

“Jengo hili lina ghorofa nne, ukijumlisha na ya chini ni ghorofa tano, litakuwa la kisasa na lenye tija na huduma mpya zitakuwepo tofauti na hospitali nyingine za rufaa nchini, litakuwa na huduma ya CT scan.

“Mkandarasi alipanga kukamilisha ujenzi mwakani mwezi Aprili, lakini mimi nimemwambia mpaka Desemba 30 awe amekamilisha kwani fedha zipo. Kuanzia tarehe moja jengo litaanza kutumika na litapunguza msongamano,” alibainisha Makonda.

Alisema Mkoa wa Dar es Salaam bado unaendelea na ujenzi wa hospitali mbalimbali, ikiwemo mpango wa ujenzi wa Hospitali ya Kawe, Bunju na Hospitali ya Rufaa ya Mabwepande. 

“Mkoa wa Dar es Salaam unahudumia watu wengi kutoka mikoa mbalimbali. Kwa takwimu za mwaka jana  watu milioni 6.8 walikuja kutibiwa hapa, watu wengi hukimbilia Dar, kwahiyo ni bora hospitali kama hizi zikaboreshwa.  

“Tayari kuna mchakato na wadau ambao ninaendelea nao wa kuhakikisha Kawe inapata kituo cha afya na kuna kingine cha Bunju, na pia tunatafuta pesa za kukamilisha Hospitali ya Rufaa ya Mabwepande. Tukikamilisha, Kinondoni itakuwa imeaga shida ya mama na mtoto,” alisema.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Daniel Nkungu, alisema kwa sasa wana wodi sita kwa kina mama, huku wengine wanalala chini, kwahiyo hatua hiyo itasaidia kuondoa msongamano. 

“Kwa sasa tuna wodi sita, hazitoshi kwa  kina mama wanaojifungua. Kwa mwaka tunazalisha kina mama 120,000 na kwa mwezi 1,000. Hawa wote wanahitaji mahali pazuri pa kujifungulia,pa kupumzikia baada ya kujifungua.  

“Kwa jengo hili litatupatia ahueni kwa uzazi  kwa kipindi kama mwezi wa 3, 4, 5 na 6 wanakuwa wanabanana sana, hata wengine wanalala chini.

“Kitanda kimoja  kina mama wanakuwa wanne  na wanabanana, tukipata vitanda vingine 100 itasaidia kupunguza msongamano,” alisema Dk. Nkungu.

Aidha Makonda aliahidi kuanzisha tuzo kuwazawadia wahudumu wa afya wanaofanya vizuri katika kazi zao ili kuongeza hamasa ya utendaji kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles