Muuguzi adaiwa kumbaka mtoto anayemuuguza mama hospitalini

0
844

Na Abdallah Amiri-Igunga

MUUGUZI mmoja wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, amedaiwa kumbaka binti wa miaka 16 (jina linahifadhiwa), mkazi wa Mtaa wa Buyumba, Kata ya Igunga Mjini, ambaye alikuwa akimuuguza mama yake aliyekuwa amelazwa hospitalini hapo.

 Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Dk. Ruta Deus, alikiri kuwepo kwa tuhuma hizo.

 “Ni kweli tukio hilo lipo na hiyo si mara ya kwanza kwani siku za nyuma muuguzi huyo (jina tunalo) akiwa Kituo cha Afya Tarafa ya Igurubi alifanya tukio kama hilo, hivyo hii ni mara ya pilli na huo ni ukiukwaji wa taratibu na kanuni za kiutumishi,” alisema Dk. Deus.

Alisema suala hilo tayari liko polisi na wao wanaendelea kuchukua hatua dhidi ya muuguzi huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini hapo, mama wa msichana huyo, Wande Salum (42) aliyekuwa amelazwa wodi no. 3, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 10, mwaka huu, saa 4 usiku.

 Wande alidai kuwa muuguzi huyo alifika katika wodi hiyo kuangalia hali yake na baada ya kumuona alimwambia ambadilishe dawa.

 Alidai kuwa muuguzi huyo aliomba aondoke na mwanawe aliyekuwa akimuuguza na walipofika ofisini alimchoma sindano ya usingizi kisha kumbaka kuanzia saa 4 usiku hadi saa 8.

Wande alidai baada ya kuona muda umekuwa mrefu pasipo mwanawe kurudi wodini, aliomba msaada kwa baadhi ya wagonjwa wenzake wenye hali nzuri wamsaidie kumtafuta.

Alidai kuwa baadhi ya manesi waliokuwa zamu walipopata taarifa hiyo, waliungana na baadhi ya wagonjwa kumtafuta mwanawe na walimkuta eneo la nyasi wanakofulia nguo kina mama akiwa hajitambui, huku akiwa amemwagiwa maji mwilini.

 Wande alidai kuwa baada ya kumwondoa katika nyasi hizo, walikuta akivuja damu sehemu za siri kutokana na kubakwa kwa muda mrefu na muuguzi huyo.

Aidha mama huyo alisema kitendo alichofanyiwa mwanawe ni cha kinyama na hakipaswi kufumbiwa macho, huku akiomba vyombo vya dola kumsaka muuguzi huyo apatikane na kufikishwa mahakamani.

 Baadhi ya kina mama wanaokwenda kutibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Rehema Julias na Sada Mwinamila, walisema hivi sasa wameingiwa na hofu kutokana na kitendo hicho na kuiomba Serikali kutofumbia macho suala hilo.

 Alipotafutwa muuguzi huyo kwa njia ya simu, ilikuwa imezimwa.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema bado hajapokea taarifa yoyote dhidi ya muuguzi huyo.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Barnabas Mwakalukwa, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo dhidi ya muuguzi huyo, alisema bado hajapokea taarifa hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here