26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Biteko: Nchi inajivunia Haki, Uhuru, Umoja na Amani

*Amwakilisha Rais Samia uwekaji Wakfu Askofu mpya Jimbo Katoliki la Bukoba

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imeeleza kuwa inatambua kuwa kuna tofauti nyingi nchini ikiwemo za makabila na madhehebu lakini tunu inayounganisha watu wote ni haki, uhuru, umoja na amani ambayo Mwenyezi Mungu ameijalia nchi na kwamba hilo ni jambo la kujivunia.

Hayo yamebainishwa mapema leo Jumamosi Januari 27,2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Bukoba, Mhashamu Jovitus Mwijage ikiwa ni tukio la kihistoria kutokana na kupita takriban miaka 50 kutoka kufanyika sherehe kama hiyo ya uwekaji wa wakfu.

Ameeleza, Serikali inatambua kuwa kuna tofauti nyingi nchini ikiwemo za makabila na madhehebu lakini tunu inayounganisha watu wote ni haki, uhuru, umoja na amani ambayo Mwenyezi Mungu ameijalia nchi.

“Mheshimiwa Rais anatambua kutofautiana ikiwemo katika  mawazo  lakini kama mnavyojua kuwa amekuwa ni muumini wa maridhiano kwani anayaishi na anatoa nafasi kwa kila mmoja kutoa mawazo yake bila kubughudhiwa,” amesema Dk. Biteko

Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Kaitaba wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa na Mbunge wa Bukoba Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato.

Akitoa Salamu za Dk. Samia kwa waumini na wananchi waliohudhuria sherehe hizo, Dk. Biteko ameeleza kuwa, Rais  ataendelea kutoa ushirikiano kwa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ili kwa pamoja walete maendeleo nchini.

Amesema, Rais anatambua kuwa bado kuna changamoto mbalimbali nchini ambazo Serikali inafanya kila jitihada ili kuzindoa lakini hili litafanyika kwa ufanisi endapo hakutakuwa na mgawanyiko nchini kama ambavyo ilivyo sasa.

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amemtakia kila la heri Askofu Mwijage katika majukumu yake mapya kwenye kanisa na malezi ya jamii kwa ujumla na kueleza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa  imani kuwa ni kiini cha ustaarabu na uungwana miongoni mwa jamii.

Ameongeza kuwa, kuwekwa wakfu kwa Askofu Mwijage kunatoa mafundisho mengi ikiwemo kutotanguliza hofu pale kunapotokea majukumu mapya kutokana na Askofu huyo kuwa tayari kutumikia  majukumu yake  bila kuweka vikwazo mbele na kwamba hili ni somo kwa wananchi wengine kuwa tayari kutekeleza majukumu bila kutanguliza vikwazo.

Wakati huohuo, Dk. Biteko amempongeza aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Askofu Methodious Kilaini ambaye leo ametangaza kustaafu rasmi na kumueleza kuwa, Serikali inatambua mchango wake na kwamba asisite kutoa mawazo  yake katika kujenga nchi na ustawi wa jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa amesema kuwa,  Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Kanisa Katoliki mkoani humo nia ikiwa ni kuchagiza maendeleo na amani mkoani Kagera.

Amempongeza Askofu Mpya, Mhashamu Jovitus Mwijage kwa kuwekwa Wakfu huo na kumtakia kila la heri katika majukumu yake mapya katika kukuza imani na masuala mengine yanayohusu jamii.

Aidha, ametoa pongezi kwa Askofu Mstaafu, Mhashamu Desderius Rwoma kwa utumishi wake uliotukuka na kueleza kuwa Mkoa wa Kagera unatambua mchango wake katika ustawi wa Mkoa wa Kagera.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Flavian Kasala amesema kuwa,  kuwekwa wakfu kwa Askofu huyo mpya wa Jimbo la Bukoba kumefanya majimbo yote yapatayo 35 nchini kuwa na Wachungaji Wakuu ambao ni Maaskofu na amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuendelea kusimamia ipasavyo Kanisa Katoliki duniani.

Amempongeza Askofu Mstaafu wa Jimbo hilo, Mhashamu Desiderius Rwoma (2013-2022)  kwa kuliongoza Jimbo hilo katika kipindi chote na kueneza injili katika Jimbo la Bukoba.

Pia, amemshukuru Dk. Doto Biteko kwa kuhudhuria sherehe hizo na hii ikionesha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali na madhehebu mbalimbali nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles