Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, imepanga kuitisha kikao cha dharura wakati wowote kuanzia sasa ili kujadili mustakabali wa kiongozi wao, Askofu Dk. Alex Malasusa.
Mwishoni mwa wiki Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo lilifikia uamuzi wa kumwadhibu Askofu Malasusa kwa kumtenga na kuwapa masharti maaskofu wengine wawili kuomba msamaha kwa tuhuma za usaliti.
Maaskofu ambao wametakiwa kuomba msamaha hadi Septemba mwaka huu, pamoja na Malasusa ni Askofu wa Dayosisi ya Kusini na Mashariki, Lukas Mbedule na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Solomoni Massangwa kutokana na Dayosisi wanazoziongoza kutousoma waraka wa Pasaka ulioandaliwa na Baraza la Maaskofu wapatao 27 wa kanisa hilo.
Wakati Mbedule akiitumia Jumapili ya juzi kuomba radhi waumini wake na hivyo kunusurika mtego wa kutengwa, Dayosisi inayoongozwa na Askofu Malasusa inajiandaa kukutana ili kulimaliza jambo hilo.
Gazeti hili limedokezwa kuwa kikao hicho ndicho ambacho kinaweza kutoa mwanga kuhusu hatma ya Uaskofu wa Dk. Malasusa.
“Unajua kwa utaratibu wa KKKT, Dayosisi zake zote 25 zinaongozwa na ama katiba au kanuni, sasa zipo Dayosisi ambazo zina katiba na nyingine hazina, zile ambazo hazina zinafuata katiba mama ya kanisa.
“Sasa Dayosisi ya Mashariki na Pwani yenyewe haina katiba inategemea ile ya kanisa, ina kanuni tu na ndio maana unaona hata uamuzi wa Baraza la Maaskofu dhidi yake umefanyika tofauti na maaskofu wale wengine wawili ambao hawajatengwa bali wamepewa adhabu,” alisema mchungaji mmoja aliyezungumza na gazeti hili.
Mchungaji huyo alisema pamoja na utaratibu huo kikao ambacho wametaarifiwa kinatarajiwa kuitishwa na Halmashari Kuu ya Dayosisi kitajadili uamuzi huo wa Baraza la Maaskofu na kimsingi ndicho ambacho kinaweza kuja na majibu zaidi kuhusu hatma ya Dk. Malasusa na nafasi yake.
Chini ya utaratibu wa kanisa hilo, inaelezwa pamoja na kwamba linaongozwa na Baraza la Maaskofu, lakini uamuzi wa kumvua uaskofu Dk. Malasusa uko chini ya dayosisi anayoiongoza.
Jana gazeti hili liliwasiliana na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Godfrey Nkini, kuhusiana na kuwako kwa maandalizi ya kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi hiyo, lakini alisema bado hawajaitisha.
Alipoambiwa kwamba gazeti hili limesikia kwamba tayari baadhi ya wachungaji wanafahamu kuhusiana na maandalizi ya kikao hicho, Nkini alihoji mtu anayetoa taarifa hizo na kisha akakata simu.
Jumapili gazeti hili liliandika juu ya uamuzi huo uliofikiwa na Baraza la Maaskofu wa KKKT kuwa pamoja na mambo mengine unamweka katika wakati mgumu zaidi ikiwa hata kuupoteza uaskofu wake iwapo hatatimiza sharti la kuomba msamaha.
Inaelezwa iwapo Dk. Malasusa atapuuza suala la kuomba radhi, huenda akakumbana na kukataliwa na wachungaji wa dayosisi yake, ambao kimsingi baadhi yao ndio waliopeleka taarifa za kumshtaki kwenye kikao cha Baraza la Maaskofu, wakidai kuzuiwa kuusoma waraka huo.
Jana kwa mara nyingine tena, chumba cha habari cha gazeti hili lilimtafuta Askofu Malasusa ili kufahamu iwapo ataliomba radhi kanisa kama alivyoelekezwa na kikao hicho cha Baraza la Maaskofu baada ya kupewa muda wa kujitafakari, lakini hakupatikana.
Ingawa inaelezwa kuwa katika kikao cha Baraza la Maaskofu Askofu Malasusa alijaribu kuomba msamaha lakini alikataliwa na kupewa muda wa kutafakari zaidi hadi Septemba mwaka huu.
Tangu uamuzi huo wa Baraza la Maaskofu uripotiwe kwa mara ya kwanza na gazeti hili, kumekuwa na mtazamo tofauti kuanzia kwa viongozi wa kanisa hilo, waumini na wafuatiliaji wengine wa mambo.
Jana mchungaji mmoja ambaye naye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini kwa kuwa si msemaji wa kanisa hilo alisema uamuzi wa Baraza la Maaskofu unatia shaka na kuzua maswali hasa kwa dhehebu ambalo linahubiri msamaha.
Alisema kimsingi yeye haoni uamuzi huo una afya kwa sababu kanisa siku zote limekuwa likiwahamasisha waumini wake kuhusu kutoa na kuomba msamaha na kuhoji iweje kwa viongozi kama maaskofu washindwe kusimamia misingi hiyo ya kiimani ambayo wamekuwa wakiihubiri.
Kiongozi mmoja wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani aliyezungumza na MTANZANIA Jumapili juzi alisema; “Nafasi hii aliyopewa Dk. Malasusa ni vizuri akaomba msamaha ili arudi kwenye mstari, akiamua kuacha kuomba msamaha na dayosisi ifanye uamuzi wake, atachafuka zaidi, dayosisi kama dayosisi hatuwezi kukubali kutokuwa na mwakilishi,” alisema.