23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE: MFUMO WA ELIMU UFUMULIWE

NA GABRIEL MUSHI, DODOMA


BAADHI ya wabunge wameitaka Serikali kuangalia upya mfumo wa elimu nchini, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuanzia ngazi ya chekechea hadi chuo kikuu.

Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ikitoa maoni yake baada ya kusomwa kwa hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2018/19, ilisema tangu mwaka 2016, imekuwa ikipendekeza mabadiliko kufanyika kwenye mfumo wa elimu nchini.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, akisoma maoni ya kamati hiyo kwa niaba ya mwenyekiti wake, Peter Serukamba, alisema licha ya kamati kupendekeza Serikali kutumia mbinu iliyotumiwa na Rais wa Marekani, Ronald Regans mwaka 1983 alipofanya maamuzi ya kuunda tume maalum kuchunguza changamoto ya mfumo wa elimu nchini humo, bado suala hilo halijafanyiwa kazi.

“Tume hiyo ilikuja na ripoti iliyojulikana kama “A nation at Risk, The Imperative for Education Reform” ambayo ilikuwa ndio historia ya mafanikio ya mfumo wa elimu nchini Marekani,” alisema.

Alisema hata Rais mstaafu, Benjamini Mkapa Novemba 2017, alibainisha wazi kuwa Tanzania haijaweka msukumo katika kutafakari upya mfumo wa elimu, kwa hali ilivyo tunahitaji kufanya mapinduzi kwenye elimu.

Aidha, Bashe alisema Machi mwaka huu Mkapa alibainisha tena kuwa anaamini kabisa kwamba kuna janga la elimu.

Akinukuu maneno ya Mkapa, Bashe alisema; “Hata ukisoma orodha ya shule zetu za sekondari kwenye ufaulu katika 10 bora za kwanza ukiangalia unaweza kuwa na uhakika kuwa nane si za serikali, ni za watu binafsi na wakati huo serikali ndio mhimili mkuu wa elimu, lazima tujiulize kuna kasoro gani?”.

Uhaba wa walimu
Akizungumzia kuhusu uhaba wa walimu nchini, Bashe alisema licha ya kuwa walimu ni nyenzo muhimu katika sekta ya elimu bado walimu waliopo hawatoshelezi mahitaji hali inayopelekea kuzorota kwa sekta hiyo.

“Kamati ina taarifa kuwa mahitaji ya walimu kwa shule za msingi ni 273,454, lakini walimu waliopo ni 175,946, hivyo kuwepo upungufu wa walimu 97,508 sawa na asilimia 35.6.

“Katika shule za sekondari hususani masomo ya sayansi, mahitaji halisi ya walimu ni 35,136, lakini waliopo ni 19, 285 hivyo kuwepo na upungufu wa walimu 15,851 sawa na asilimia 45.1,” alisema.

Kutokana na hali hiyo alisema Serikali haina budi kuchukua hatua za makusudi kuongeza ajira za walimu kunusuru Taifa kwani walimu wengi wapo mitaani hawana ajira

Aidha, Alisema kamati inapinga suala la walimu wa sekondari kufundisha shule za msingi kwa kuwa kila ngazi ya ualimu ina miongozo na mafunzo yake mahususi.

Alisema kitendo hicho kinapokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa jamii na walimu wenyewe ikiwemo kuhisi kuadhibiwa hivyo kushusha morali ya kufanya kazi.

“Kamati inaitaka Serikali kuliangalia hili kwa jicho la kipekee na kufanya maamuzi yaliyo sahihi kwa mustakabali mzuri wa elimu nchini,” alisema.

Hata hivyo, aliitaka Serikali kuunda Bodi ya taaluma ya ualimu ili  kuhakikisha wanapatikana walimu wazuri wenye uwezo wa kutoa elimu yenye ubora unaotakiwa.

Mikopo elimu ya juu

Akizungumzia kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Bashe alisema kamati inashauri kuanzia sasa kigezo cha ufaulu kipewe kipaumbele cha kwanza kwa kuangalia mtu aliyefaulu vizuri kuliko wengine.

“Lakini bodi hii ya mikopo ipewe fungu lake yenyewe na  sio ya miradi ya maendeleo ambayo asilimia 48,” alisema.

Aidha, alishauri serikali kuangalia upya kodi na tozo kwa shule binafsi ikiwa ni pamoja na kuweka uwiano wa kuchangia mfuko wa fidia kwa wafanyakazi kati ya shule za umma na shule binafsi kuwa ni asilimia 0.5 ya pato la mfanyakazi.

“Pia kuondoa urasimu katika upatikanaji wa misamaha ya kodi na tozo ili kuwezesha sekta binafsi kupata msukumo zaidi wa kuwekeza na hivyo kuendelea kuzalisha watalaam wengi na wazuri zaidi,” alisema.

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe (CCM) alisema sekta ya elimu inapitia mabadiliko makubwa katika kipindi cha miaka 10 ya Serikali za awamu mbalimbali.

Alisema sekta hiyo kwa sasa inaelekea pabaya hasa ikizingatiwa ufaulu wa wafunzi umeshuka.

“Sasa hivi mwanafunzi anayetoka chuo kikuu amehitimu shahada ya sheria hajui kuandika nakala ya hukumu kwa kiingereza.

“Ukiangalia matokeo ya mitihani kwa miaka yote wanaofaulu mtihani wa elimu ya msingi kwenye somo la hisabati hawazidi asilimia 17 kila mwaka na wanaofaulu kiingereza hawazidi asilimia 21.

“Hivyo kama watoto hawajui hesabu na kiingereza ambacho hatua inayofauata kinakuwa lugha ya kufundishia haiwezekani kupata elimu bora,” alisema.

Alisema ni lazima serikali kuwapatia vitendea kazi ikiwamo vitabu walimu wanaofundisha ili kuongeza kiwango cha ubora wa elimu nchini.

“Hata walimu nao ni tatizo kwa sababu nakumbuka kuna mtihani wa hesabu wa mwaka 1994 ulitolewa kwa walimu  na wanafunzi wa shule ya mkoa mmoja,  wanafunzi wakafaulu kwa asilimia 17 walimu asilimia 12, sasa unategemea nini hapo?” Alihoji Maghembe.

Aidha, alisema ni vema serikali kurudia kutumia vitabu vya Oxford ambavyo vilitumika katika miaka ya 1990 na 80 kufundishia kiingereza.

Kwa upande wake Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM), alisema kutokana na idadi ya asilimia 60 ya wanafunzi kupata daraja la nne na sifuri, ni vyema serikali ikawekeza kwenye elimu ya ufundi.

Alisema licha ya mwanafunzi kutumia miaka minne shuleni lakini matokeo yake anashindwa kufaulu mitihani ni vyema angeitumia kwenye elimu ya mafunzo ya ufundi.

Pia aliiomba serikali kupeleka vitabu vya darasa la nne, ili wanafunzi waweze kusoma kabla ya kuingia kwenye mitihani kwa sababu kuna shule zaidi ya 170,000.

Aidha, alilieleza Bunge kuwapo kwa baadhi ya walimu wa vyuo vikuu, wanaofelisha wanafunzi wa kike pindi wakinyimwa rushwa ya ngono.

“Nilipotoa hoja hii, waziri alisema hajanielewa sasa akishirikiana na mimi nitampatia majina ya vyuo vikuu vyenye walimu wanaotaka rushwa ya ngono kwa wanafunzi, nitakueleta majina ya walimu ambao ni madume ya mbegu kazi yao kufelisha wanafunzi kwa kutaka rushwa ya ngono.” alibainisha.

Naye, Mbunge wa Nkenge, Deudorus Kamala (CCM), aliipongeza kamati hiyo kwa kuwasilisha taarifa inayohuisha sekta ya elimu ila changamoto ni nyingi hasa ukizingatia kuna shule binafsi zaidi ya 4000.

Alisema kiwango cha ubora wa elimu nchini bado hakiridhishi hivyo mageuzi ya uhakika yanahitajika.

“Katika matokeo ya mwaka jana kati ya shule 100 nzuri, serikali ilikuwa na shule nne na 96 ni za binafsi. Hivyo kuna kazi ya kufanya ili na sisi tujivunie,” alisema.

Alisema Serikali ina kazi ya kufanya kwa sababu bado ufaulu kwenye shule za sekondari katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana, kati ya shule 100 bora, shule za Serikali zilikuwa nne pekee.

Naye Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), alisema ni vema kuwepo kwa bodi ya taaluma ya ualimu ili kuimarisha taaluma ya ualimu.

Alisema ufaulu wa wanafunzi kidato cha nne bado hauridhishi kwani katika mtihani wa mwaka jana katika shule kumi bora, shule za serikali hazikuwepo na katika shule 100 zilizofaulu zilikuwa shule sita pekee.

Bilago alisema hali hiyo inatokana na ukosefu wa motisha kwa walimu na uhaba wa walimu kwenye shule za serikali.

“Ualimu morali kwanza itoke moyoni. Hivyo tusijifiche kwenye kichaka cha elimu bure, wakati miundombinu haipo,’ alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles