24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Dar yaongoza ukusanyaji mapato

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), amesema Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kundi la halmashauri za majiji kwa kukusanya mapato kwa asilimia 38 ya makisio yake ya mwaka.

Katika makundi ya mikoa, Dar es Salaam imekuwa kinara ikikusanya Sh bilioni 39.53 huku Kigoma ikiwa ya mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya Sh bilioni 2.12.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana Dodoma, alipokuwa akitoa taarifa za mapato ya halmashauri zote katika robo ya kwanza ya mwaka wa mapato Julai mosi hadi Septemba 30, mwaka huu.

Jafo alisema wakurugenzi wa maeneo ambayo hawajafanya vizuri waendelee kujitathmini vinginevyo itakula kwao.

Akitoa takwimu za mapato kwa kulinganisha makundi ya halmashauri, miji, manispaa na majiji, alisema Wilaya ya Buhigwe imeburuza mkia katika makundi yote kwa kukusanya Sh milioni 35.

“Kwa wastani hadi sasa halmashauri zimekusanya Sh bilioni 166.24 ambayo ni asilimia 22 ya lengo la kukunya Sh bilioni 765.48 ambazo zilipitishwa na Bunge zikusanywe,” alisema Jafo.

Kwa asilimia katika majiji, Dar es Salaam imefikia 38 wakati ya mwisho ni Dodoma (18), kwa manispaa Sumbawanga imeongoza kundi hilo kwa asilimia 42, Kigoma Ujiji ikiwa na asilimia 9. Kwa miji Tunduru ni kinara (39) huku Nanyamba ikishindwa kufurukuta kwa kukusanya asilimia 4.

“Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya kwa asilimia 18 ya makisio yake ya mwaka,” alisema.

Hata hivyo kwa upande wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kuzingatia aina za halmashauri kwa kigezo cha asilimia ya makusanyo ukilinganisha katika  kipindi hicho Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongoza kundi la Halmashauri za Majiji kwa kukusanya mapato kwa asilimia 38 ya makisio yake ya mwaka.

Jafo alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imeongoza kundi la halmashauri za manispaa ambayo imekusanya asilimia 42 ya makisio yake.

Huku Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma imekuwa ya mwisho ikikusanya asilimia tisa ya makisio yake kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Jafo alisema bajeti iliyoidhinishwa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2019/20 ni Sh bilioni 76.48. 

Alisema kwa kipindi cha robo ya kwanza halmashauri zimekusanya jumla ya Sh bilioni 166.24 sawa na asilimia 22 ya makisio ya mwaka.

“Katika kipindi hiki, halmashauri zilipaswa kukusanya mapato kwa asilimia 25 ya makisio yake ya mwaka. Halmashauri 54 zimekusanya zaidi ya asilimia 25 ya bajeti zao zilizoidhishwa kwa mwaka wa fedha 2019/20,” alisema  Jafo.

Aidha, alisema halmashauri 121 hazikuweza kufikisha asilimia 25  ya makusanyo yake.

“Hata hivyo, natambua kuwa kila halmashauri inakusanya mapato mengi au kidogo katika vipindi tofauti kutokana na aina za vyanzo vya kila halmashauri.

“Mfano kuna halmashauri zinakusanya mapato kutoka kwenye mazao yanayopatikana kwa msimu mwishoni mwa mwaka wa fedha,” alisema Jafo.

Alisema uchambuzi unaonyesha kuwa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/20 halmashauri 54 kati ya 185 zimefanya vizuri kwani zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 25 au zaidi ya makisio ya mwaka wa fedha 2019/20.

Hata hivyo alisema Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imekuwa ya kwanza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 52 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka huu na Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa imekuwa ya mwisho kwa kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 3 ya makisio yake.

Jafo alisema kuwa Mkoa wa Rukwa umeongoza kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kipindi cha kuishia Septemba 30, 2019 ambao umekusanya wastani wa asilimia 31 ya makisio yake ya halmashauri za mkoa huo.

Aidha alisema mkoa wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mtwara ambao umekusanya wastani wa asilimia 13 ya makisio ya mwaka ya halmashauri za mkoa huo.

Jafo alisema Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa wingi wa mapato katika halmashauri za miji ikikusanya Sh bilioni 2.34 huku Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ikiwa  ya mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya Sh milioni 74.72.

“Hali kadhalika Halmashauri ya Chalinze imeongoza kwa kukusanya mapato mengi kwa halmashari ambapo imekusanya Sh bilioni 2.05 na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Sh milioni 35,” alisema Jafo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles