23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Daktari awashangaa wanaohoji afya ya JPM

MWANDISHI WETU –Dar es Salaam

DAKTARI wa binadamu katika Hospitali ya Lugalo, Dar es Salaam, Walter Nnko, amejitokeza na kueleza kushangazwa na hatua ya baadhi ya watu kuanza kutoa taarifa za kutetereka kwa afya ya Rais Dk. John Magufuli, akisema hatua hiyo inakiuka misingi ya utu, taaluma na hata sheria za nchi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Dk. Nnko alisema kutokana na namna ambavyo taarifa hizo zimekuwa zikisambaa, ni vyema wahusika ambao wanafahamika wachukuliwe hatua na vyombo vinavyohusika.

Alisema ni wazi kuwa kwa binadamu yeyote, kuugua ni suala la kawaida na yeyote ana haki ya kufanya ugonjwa wake kuwa siri, lakini ubaya unakuja pale watu wengine wanapoamua kwa sababu zao binafsi kuzusha ugonjwa na kusambaza taarifa mbaya kwa nia ya kuvuruga hali ya usalama wa nchi.

“Katika utaratibu wa kawaida, ni suala la uamuzi wa mtu binafsi kutangaza ugonjwa wake. Wakati mwingine mtu anaweza kuumwa hata asimwambie mwenza wake, akafanya matibabu akamaliza.

“Inapotokea kundi la watu wachache wakaanza kusambaza uvumi kuhusu kutetereka afya ya mtu au hata kifo, ni suala baya lisilokuwa na nia njema. Hasa uvumi huo unapomhusu kiongozi mkubwa wa kitaifa, ambaye kila siku tunamwombea awe mzima, mwenye afya tele ili atekeleze majukumu yake,” alisema.

Alisema yeye akiwa daktari, anatambua kuwa haki ya usiri wa mgonjwa ni suala la kimaadili, kwa hiyo anaona kuna hatari zaidi, hasa pale wanapojitokeza watu na kusambaza uzushi huku wakijua kabisa kuwa kwa kufanya hivyo wanalikosea taifa.

Dk. Nnko alisema anaamini Tanzania ni nchi yenye amani na isiyo na ubaguzi wa ukabila, kwamba mtu anaweza kufanya kazi popote na yeyote, hivyo uvumi wa ugonjwa, tatizo la kiafya au kifo kwa mtu mwingine ni suala linalochochea chuki.

Alisema kutokana na dhana hiyo, ni vyema Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na mamlaka zote zinazohusika ziwashughulikie wahusika na kuhakikisha kuwa suala kama hilo halijirudii kwa kuwa ni aibu kwa taifa, hasa ikizigatiwa watu wanaofanya hivyo ni watu wenye elimu na dhamana.

Dk. Nnko alisema anaamini watu wenye elimu ndio wenye uwezo wa kupima jambo na wakati mwingine wana utambuzi wa kujua mema na mabaya, hivyo kuwa na ufahamu unaowasukuma kufikiri kabla ya kutenda.

“Kwa akili ndogo tu, kwa mtu muungwana hutakiwi kumwombea jirani yako mabaya, na ukiona mtu anafanya hivyo basi ujue akili yake siyo nzuri, ukiona mtu anafurahia mtu mwingine apate matatizo, si jambo jema,” alisema.

Alieleza kuwa ni wazi asilimia 80 ya Watanznaia wametokea katika familia masikini, hivyo miongoni mwao hakuna anayeweza kufurahia kuona Rais ambaye amejipambanua kutetea rasilimali za taifa kusaidia wanyonge kwa nguvu zake zote anafanyiwa dhihaka.

“Inatakiwa tumwombee Rais kila siku, aendelee kuwa na afya njema, aendelee kwa nguvu ile ile kutetea haki za wanyonge. Hakuna binadamu mwenye haki ya kumtangazia mwenzake jambo baya, hata daktari haruhusiwi kutoa taarifa mbaya au kutangaza ugonjwa wa mtu,” alisema Dk. Nnko.

Alisema kwa sasa wakati wengine wakiendelea kujenga chuki kwa Rais Magufuli na Serikali yake, ndio wakati sahihi wa Rais kuendelea kujenga nchi kwa kuwa hata kama angekuwa malaika, watu hawawezi kuacha kumsema kwa mabaya.

“Tumejifunza mengi sana kupitia kwake, kwa jinsi ambavyo amekuwa na utendaji kazi wa kipekee na bado anapigwa vita. Rais endelea kuchapa kazi. Taifa linakutegemea katika kuchochea maendeleo,” alisema Dk. Nnko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles