23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Dar yakabiliwa na ongezeko la taka

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM 

JIJI la Dar es Salaam linakabiliwa na ongezeko la taka mbalimbali na inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2025 zitafikia tani 12,000.

Akizungumza wakati wa mkutano  wa wadau wa mazingira wenye lengo la kujadili changamoto za taka  uliofanyika jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (Nemc), Mhandisi, Dk. Samweli Gwamaka alisema ongezeko hilo linatokana na ukuaji wa viwanda na idadi ya watu. 

“Tumekutana hapa kujadili changamoto mbalimbali za udhibiti wa taka katika maeneo tofauti tofauti kama hospitali, majumbani, taasisi mbalimbali. Kimsingi ni changamoto ambayo imekuwa ikikua sana kutokana na ongezeko la watu. 

“Ongezeko la maendeleo ya viwanda linachangia pia na mpaka sasa inakisiwa kuwa ifikapo mwaka 2025  Dar es Salaam peke yake inaweza kukusanya tani 12,000 za taka za majumbani na maeneo mengine,” alisema Dk. Gwamaka.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanalazimika kuweka utaratibu  ambao ni endelevu ili kuhakikisha mazingira ya Tanzania yanaboreshwa.

“Sasa kuna changamoto nyingi ambazo zinajadiliwa hapa, kwa sababu ukizungumzia suala la taka kuna kukusanya, kusafirisha na  kutupa kwenye dampo, na utakuta wengine wanazichambua, wengine wanaenda kuzirejelesha. 

“Sheria ya mazingira ya mwaka 2014 inazitaka halmashauri zote, jiji na manispaa ziweke mfumo wa kutenga taka tangu pale zinapozalishwa na zinampa mamlaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wajibu wa kuweka mwongozo ambao utaelekeza taasisi, masoko, majumbani kwamba ni kwa jinsi gani wanatakiwa kutenga hizo taka,” alibainisha Dk. Gwamaka.

Alisema kuwa lazima jamii ielewe kuwa taka sio uchafu, bali ni fursa ya kujiingizia kipato, hivyo ni muhimu kutenga taka katika sehemu zote. 

“Kwanza taka sio uchafu ni fursa,  ukichambua na kuzirejeleza zinaleta ajira, lakini zinapunguza uletaji wa malighafi toka nje au malighafi mpya ikatumiwa, kwa hiyo utakuta zile taka ni fursa ya kuendeleza hata kwenye uchumi wa viwanda na kupunguza uletaji wa malighafi kutoka nje. 

“Ni kweli kuwa tunahitaji kuwa na mfumo wa kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kwamba wadau tunashirikiana kufanya mazingira yetu yanaboreshwa, changamoto kama hizo ndizo zinatukutanisha,” alisema Dk. Gwamaka.

Alisema kuwa kuna changamoto ambazo zinahitaji mabadiliko ya sera, lakini kuna zingine ni mpya.

“Sasa hivi tunaona kipindi cha Covid-19 kumekuwa na ongezeko la barakoa, chupa za plastiki, kuna mambo mengi, kwa jinsi watu wanavyoongezeka ndivyo na changamoto zinaongezeka,” alisema Dk. Gwamaka. 

Alibainisha kuwa kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi ili kuelewa jinsi ya kutenga taka na zingine kurudishwa katika urejeleshwaji.

“Umuhimu wa kuelimisha wananchi ni mkubwa sana kwa sababu pale unapotenganisha taka ni fursa,  kwa mfano taka za plastiki, vyuma, karatasi badala ya kutupa kuna watu wananunua, hivyo kujipatia kipato, Ndio maana tunataka kuelimsha jamii kuwa taka ni fursa hasa watakapojua kutenganisha na pia dampo zitakuwa hazijai na gharama za uzoaji zitapungua. 

“Lakini pia na uchumi wa viwanda uweze kufanikiwa ambao Mheshiwa Rais John  Magufuli anaupigania kila siku,” alisisitiza Dk. Gwamaka. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles