25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Damu ya binadamu yasafirishwa kiholela, Serikali yashtushwa

Na BENJAMIN MASESE

-MWANZA

SERIKALI imeshtushwa na kitendo cha Kampuni ya Tutume isiyojulikana kisheria kufanya kazi ya kusafirisha damu za binadamu, nyaraka nyeti za umma, majibu ya vinasaba, vifurushi na sampuli mbalimbali za dawa ambayo inapaswa kufanywa na Shirika la Posta Tanzania (TPC) jambo ambalo ni hatari kwa usalama.

Kutokana na hilo, imesema tayari iliwabaini vigogo wa Makao Makuu ya Posta kuwa ndio waliofanya udanganyifu kwa kuziondoa kinyemela taasisi zilizoingia mkataba halali na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufanya kazi hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alipokuwa akizungumza na  waandishi wa habari baada ya kuhitimisha kikao cha pamoja na watumishi wa TPC, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mkoani hapa.

Nditiye alisema taarifa hizo alizipata kutoka kwa watumishi wa shirika hilo katika kikao cha pamoja.

Alisema taarifa hizo zilidai kuwa Posta imenyang’anywa kazi ya kusafirisha damu na vifurushi katika Mkoa wa Kagera na Geita, hivyo shughuli hiyo inafanywa na kampuni binafsi inayojulikana kwa jina la Tutume.

Nditiye alisema baada ya kupokea taarifa na kufuatilia kwa haraka, ikiwamo kuwasiliana na viongozi wengine ngazi za juu, alibaini baadhi ya watumishi wa Posta Makao Makuu ndio waliofanya mchezo huo kwa kushirikiana na Tutume kwa manufaa yao binafsi.

“Haiwezekani mashirika ya umma yakachezewa na watumishi wasio na maadili kazini kwa manufaa yao, ni aibu mtu wa Serikali kuihujumu nchi iliyokuajiri na kushirikiana na kampuni binafsi, tena wanasafirisha vitu nyeti zikiwamo damu za binadamu, nyaraka za siri, vinasaba tena bila utaratibu,” alisema.

 Nditiye aliagiza kampuni hiyo kusimamisha huduma hizo na kuwasilisha nyaraka zao.

“Kuanzia sasa naagiza kampuni hiyo kusimama kufanya kazi hiyo, pia ndani ya siku saba nawaomba viongozi wa kampuni hiyo kuwasilisha nyaraka zao popote iwe TCRA au Posta zinazoonyesha uhalali wao, vilevile kibali cha kusafirisha damu na sampuli mbalimbali,” alisema Nditiye.

Baada ya kutoa kauli ya kusitisha kampuni hiyo, Nditiye aliagiza Posta kuendelea kufanya kazi hiyo.

“Naagiza Posta wakati tukisubiria vielelezo hivyo, endeleeni kusafirisha damu na vitu vingine katika mikoa hiyo ili shughuli za Serikali zisikwame na kwa kuwa tumekwishawajua wahusika ni watumishi wenzetu wa makao makuu, nakwenda kuwachukulia hatua, bila shaka mtasikia siku zijazo,” alisema.

Nditiye aliagiza mikataba yote iliyoingiwa na taasisi za umma zikiwamo TTCL, Posta na TCRA isitishwe na kuagiza uchunguzi wa haraka ili kubaini uhalali wao.

Akifafanua zaidi, Kaimu Meneja wa Posta Mkoa wa Mwanza, Philip Mchele, alisema awali Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliingia mkataba na Taasisi ya Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) ambayo ndiyo ilikuwa ikisafirisha damu.

“Baada ya mkataba wa AGPAHI kumalizika, wizara iliingia tena mkataba na Taasisi ya Usimamizi na Maendeleo ya Afya (MDH) na hizi taasisi ambazo zilikuwa zikipewa mikataba tulikuwa tunashirikiana vizuri, lakini ghafla tukaambiwa tusimame kufanya kazi hiyo, badala yake kuna Kampuni ya Tutume ndiyo itafanya shughuli hiyo,” alisema Mchele.

Alisema walibaini kuna mchezo baada ya kufuatilia na kuchunguza.

“Tulipofuatilia tulibaini kuna mchezo fulani na tukatoa taarifa ngazi za juu. Tulipofuatilia kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita na Kagera hatukupata majibu mazuri, tunashukuru Naibu Waziri Nditiye amelichukulia kwa uzito na kusitisha mikataba hiyo,” alisema Mchele.

MKONGO WA TAIFA

Katika mkutano huo, Nditiye aliongeza kuwa maelezo aliyoyapata kutoka kwa watumishi ni kwamba hata mkongo wa mawasiliano kuna kampuni kadhaa ikiwamo ya Simbanet zikiwa na mikataba yenye utata zimeingilia mkongo huo na kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi.

Kutokana na hilo, Nditiye aliwaagiza mameneja wa Kanda ya Ziwa na Mkoa wa Mwanza wa TCRA, TTCL na TPC kuhakikisha wanasimamia maagizo yake na kila mmoja kutimiza wajibu wake ili  taasisi hizo ziweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Naye Meneja wa TTCL Mkoa wa Mwanza, Jalili Bakari, alisema kuna baadhi ya kampuni zimeingilia mkongo wa taifa wa mawasiliano na kufanya kazi ya kuwahudumia watu huku akibainisha kwamba leseni au vibali hivyo hajui vinatolewa kwa namna gani huko ngazi za juu.

Bakari alisema kampuni hizo ikiwamo ya Simbanet zimekuwa zikifanya shughuli zao kwa kutumia mkongo wa mawasiliano, hivyo aliomba hatua zichukuliwe ili kubaini vibali vilikotolewa.

Hata hivyo alidokeza kuwa baadhi ya mali za TTCL zimekodishwa kwa kampuni hizo, lakini kiuhalisia TTCL inapata hasara ya Sh milioni 10 kwa mwezi.

TCRA

Akizungumza Meneja wa Kanda ya Ziwa wa TCRA,  Mhandisi Francis Mihayo aliagiza kampuni zenye mikataba ya kufanya kazi na TTCL na TPC kuiwasilisha ofisini ili kujiridhisha kwani mamlaka hiyo ndiyo inayotoa leseni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles