Na RAMADHAN HASSAN
-DODOMA
SERIKALI imeagiza Maofisa Utamaduni nchini kuanza kushirikishwa katika vikao vya maamuzi ili wapate kujua mikakati ya maendeleo kwa sekta zao.
Agizo hilo limetolewa jana jijini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo wakati akifunga kikao kazi cha maofisa utamaduni wa mikoa na halmashauri kilichokuwa na lengo la kujadili changamoto mbalimbali katika kada hiyo.
Jafo alisema kushirikishwa katika vikao vya maamuzi kwa watendaji wa Kada hizo kutasaidia kuongeza chachu ya kukua kwa sekta hizo katika mikoa pamoja na kutoa maoni ya kitaalum.
“Katika bajeti ya mwaka huu mtenge ya Kitengo cha maafisa utamaduni kwani kada hii ni muhimu kuwepo kwa lengo la kusaidia kutangaza maendeleo na fursa zilizopo katika Mkoa wenu,” alisema Jafo
Jafo alisema mara nyingi maofisa utamaduni hudharaulika kutokana na kufanya kazi kwa mazoea na kwamba wanatakiwa kuwa na ujuzi mpya utakosaidia kujenga na kuibua vibaji vingi katika jamii.
Alisema Serikali inataka wananchi wapate kujua shughuli zote za maendeleo ya utamaduni katika mikoa yao zinavyofanyika.