Daktari bingwa aeleza msongo wa mawazo unavyosababisha saratani ya matiti

0
635

AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Huduma za Kinga ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Crispin Kahesa, amesema msongo wa mawazo unachangia ongezeko la saratani ya matiti kwa wanawake kutokana na kuvuruga homoni za ukuaji zijulikanazo kwa kitaalamu kama Oestrogen. 

Akizungumza katika kuelekea kilele cha mwezi wa saratani jana, Dk. Kahesa alisema sababu nyingine ni mfumo mbaya wa maisha, ikiwamo aina ya ulaji wa vyakula na watu kutokufanya mazoezi. 

“’Stress’ pia inaweza kusababisha saratani ya matiti,  sababu saratani ya matiti kuna nadharia nyingi sana, moja ya kisababishi tunahusisha homoni ya oestrogen. Hii ni homoni ambayo pia inachochea ukuaji, hasa wa matiti.  

“Ndiyo maana wanasema kina mama ambao homoni hazipo au wamefikia ukomo wa uzazi, wako hatarini zaidi au wanene wanaotengeneza oesrtogen wapo hatarini, pia kutumia baadhi ya dawa za uzazi wa mpango.

“Msongo wa mawazo unasababisha usumbufu kwa homoni kwa sababu homoni hizo ndio zinaratibu ukuaji na kiwango cha matiti kulingana na kichocheo cha homoni. Mfano ukiwa kwenye hedhi, matiti yanaweza kuongezeka au kuuma, hizo zote ‘zina-controliwa’ na homoni, kwahiyo ukiisumbua inaweza ikasababisha saratani ya matiti,” alisema Dk. Kahesa.

 Pia alisema mtu akiwa na msongo wa mawazo, kiwango cha kinga za mwili kinashuka na hali hiyo inaweza kusababisha kinga kushindwa kudhibiti maradhi, ikiwamo saratani ya matiti, hivyo ni vyema kuweza kukabiliana na msongo wa mawazo.

Dk. Kahesa pia alieleza kuwa ni bora jamii ikazingatia mfumo bora wa maisha, hasa ulaji wa vyakula vyenye kujenga mwili, kufanya mazoezi na kupima saratani ya matiti mara kwa mara.

“Wito wetu ni kuiambia jamii saratani ya matiti inazuilika, moja ni kufuata mfumo bora wa maisha unaozingatia ulaji bora, kufanya mazoezi, lakini pia kula vyakula vyenye kujengea kinga za mwili kama matunda na mbogamboga, tunawasisitiza pia watu kwenda kituo cha afya kupima mara kwa mara,” alisisitiza.

HALI YA UGONJWA WA SARATANI YA MATITI

Kwa mujibu wa Dk. Kahesa, tatizo la ugonjwa wa saratani ya matiti limeongezeka kwa asilimia 14 kutoka 11 kwa miaka 10 iliyopita, huku kwa sasa ikishika nafasi ya pili baada ya saratani ya mlango wa kizazi.

Dk. Kahesa alisema tangu kuanza kwa vipimo mwezi Januari hadi Oktoba mwaka huu, jumla ya wanawake 1,493 walijitokeza kupata vipimo na kati ya hao wanawake  372 waligundulika na uvimbe, huku kina mama 68 walikuwa na dalili hatari za saratani.

“Mwezi huu wa Oktoba ambapo kesho (leo) ni kilele cha maadhimisho, sisi tunaadhimisha kwa kujenga uelewa wa jamii kuhusiana na dhana potofu kuhusu saratani ya matiti  kwa kuwaambia kuwa saratani ni ugonjwa ambao unazuilika na pia unatibika na kupona pale unapowahi.

“Mpaka sasa tumeweza kufanya uchunguzi kwa kina mama, hii imetusaidia kuwagundua katika hatua za awali, wengi tumewakuta wakiwa katika hali ya kwanza na ya pili tofauti na wasipogundulika wanaweza kukaa mpaka hatua ya nne,” alieleza Dk. Kahesa.

Alisema zamani watu waliokuwa wakipata saratani ya matiti walikuwa wanaanzia miaka 65, lakini kwa sasa ugonjwa huo unawapata zaidi watu miaka 25 hadi 52.

WANAUME WASHAURIWA KUPIMA 

Ugonjwa wa saratani ya matiti kwa kiasi kikubwa huwashambulia wanawake zaidi, lakini wapo wanaume wanaoupata ugonjwa huo pia.

Hata hivyo, Dk. Kahesa aliwashauri wanaume kujitokeza katika uchunguzi wa saratani ya matiti kwani hata asilimia ndogo wanaopata wanafika wakiwa tayari wana hali mbaya.

“Kati ya wagonjwa 100, mwanaume anaweza kuwa mmoja. Kwa bahati mbaya kina baba wengi hawajitokezi kufanya uchunguzi wa awali, wengi wanakuja wakati tayari wameshaathirika.

“Sababu za wanaume kutokupima wengi wanaona kuwa sio tatizo kubwa, mara nyingi kwa wanaume tatizo linaanza kama uvimbe usiouma, hivyo mpaka unafikia hatua za juu ambapo sasa maumivu yanaanza.  

“Nawashauri wanaume wajitokeze kupima saratani ya matiti kwa hatua za awali na pia watakapoona uvimbe waende hospitali kwani hata kwa mwaka huu hakuna mwanaume hata mmoja aliyekuja kupima, wanakuja wakati tayari ugonjwa umeshasambaa,” alishauri Dk. Kahesa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here