33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waliokutwa na tausi wa Ikulu kulipa fidia Sh mil 6

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru kwa masharti na kuamuru kulipa fidia ya Sh milioni 6 wakazi watatu wa Dar es Salaam, baada ya kukiri kosa la kukutwa na tausi watatu wanaodaiwa kuwa wa Ikulu.

Washtakiwa hao wametiwa hatiani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally na kuachiwa huru kwa masharti ya kutofanya makosa ya jinai ndani ya miezi sita na kulipa fidia waliyokubaliana.

Uamuzi huo ulifikiwa ikiwa ni siku tano tangu waende gerezani na kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini  (DPP) ya kumaliza kesi hiyo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliwataja washtakiwa kuwa ni David Graha, Mohamed Hatibu na Mohamed Ally ambao walifikia makubaliano Oktoba 28, mwaka huu na DPP.

Wankyo alidai kuwa washtakiwa walikubaliana kuondolewa mashtaka yote na kubakia na shtaka moja la kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Inadaiwa kwa kwa nyakati tofauti walikutwa na tausi watatu wenye thamani ya Sh Sh 3,444,150.

Kwamba tausi mmoja alikutwa Manzese Madizini na tausi wawili walikutwa nyumbani kwa mshtakiwa Mohammed, Oysterbay.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, walikiri na mahakama iliwatia hatiani.

Wankyo aliiomba mahakama iwape adhabu kutokana na makubaliano waliyoingia na DPP, aliomba tausi wataifishwe na kuwa mali ya Serikali.

Alidai walikubaliana kulipa fidia kwa hasara waliyosababisha kwa Serikali Sh 6,890,000 na tausi wabakie kuwa mali ya Serikali. 

Washtakiwa kwa nyakati tofauti wakiomba msamaha, waliomba wapunguziwe adhabu kwa sababu wana majukumu makubwa ya kifamilia.

Hakimu Ally akitoa adhabu, alisema mahakama inawaachia huru washtakiwa kwa masharti ya kutofanya kosa la jinai ndani ya miezi sita na endapo watafanya watapewa adhabu kwa mujibu wa sheria.

Mahakama pia imewataka washtakiwa kulipa fidia ya Sh 6,800,000. Wamelipa fedha hizo na tausi watatu wametaifishwa kuwa mali ya Serikali.

Washtakiwa hao inadaiwa walitenda makosa hayo kati ya Julai mosi mwaka 2015 na Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa katika kipindi hicho washtakiwa walikutwa na tausi watatu wenye thamani ya dola za Marekani 1,500 sawa na Sh 3,444,150 mali ya Serikali  bila ya kibali.

Katika mashtaka yaliyoondolewa, mshtakiwa Ally alikuwa anadaiwa Oktoba 14 mwaka huu alikutwa na tausi hao wanaodaiwa kupatikana kwa njia isiyo halali.

Ilidaiwa kati ya Juni mosi mwaka 2015 na Oktoba 2019 washtakiwa Graha na Hatibu walitakatisha Sh 300,000 huku wakijua zilitokana na kosa la wizi.

Mshtakiwa Ally anadaiwa kutakatisha Sh 300,000 kwa kuwapatia fedha hizo washtakiwa wenzake huku akijua zilitokana na kosa la wizi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles