28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

CUF Maalim wataka jaji mkuu aingilie hukumu

PATRICIA KIMELEMETA

CHAMA Cha Wananchi (CUF) upande unaomuunga mkono  Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, umemuomba Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuibana  Mahakama Kuu kutoa hukumu ya kesi namba 23/2016 inayohusu uhalali wa uenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba kwenye chama hicho.

Kauli hiyo imetolewa wiki moja baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaama, Benhaj Masoud, kuahirisha hukumu ya kesi hiyo hadi Machi 18.

Wakizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, baadhi ya wabunge wa chama hicho upande wa Maalim Seif,  walisema mpaka sasa wanashindwa kuendelea na majukumu ya  siasa kutokana na mgogoro wa  uongozi ndani ya chama hicho, hali iliyosababisha kufunguliwa kwa kesi mahakamani ikiwamo ya uhalali wa Lipumba.

“Tunaomba Jaji Mkuu, Profesa Juma au Jaji Kiongozi, Dk. Eliezer Felesh, kuingilia kati hukumu ya kesi yetu ambayo inachukua muda mrefu kutosomwa hali inayosababisha shughuli za  siasa kushindwa kufanyika kutokana na mgogoro wa  uongozi,”alisema Mbunge wa Malind, Ally Saleh ambaye ndiye aliyefungua kesi hiyo.

Alisema mgogoro huo umesabababisha kujitokeza  mgawanyiko wa wanachama ambako upande mmoja unamuunga mkono Lipumba na mwingine unamuunga mkono Maalim Seif.

Alisema  mpaka sasa hukumu hiyo imeahirishwa mara nnne na mara ya kwanza ilitakiwa kusomwa Oktoba 10, 2018, iliahirishwa hadi Novemba 30, 2018, ikaahirishwa tena hadi Januari 15, 2019,  ikiaahirishwa tena hadi  Februari 22, 2019 na sasa imeahirishwa hadi Machi 18, 2019.

Alisema kutokana na kujitokeza hali hiyo, wanachama wamepata wasiwasi wa kujua hatma ya uongozi ndani ya chama hicho hali iliyosababisha kumuomba Jaji Mkuu kuingilia kati.

Alisema mahakama ndiyo chombo pekee nchini kinachosimamia haki, hivyo basi wanaamini watatenda haki   hukumu hiyo itakapotolewa.

Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, chama kinahitaji kufanya mikutano ya ndani  kuteua viongozi mbalimbali watakaosimamia uchaguzi wa ndani na uchaguzi mkuu kuhakikisha wanashindwa, lakini kuwapo   mgogoro huo kumesababisha kushindwa kufanyika   mikutano.

Profesa Lipumba alijiuzulu nafasi ya uenyekiti Agosti 6, 2015 wakati chama kinaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais.

Alisema licha ya kupitia changamoto hizo, chama hicho kiliweza kufanya vizuri kwenye uchaguzi huo na kusaidia kupata wabunge wanne kutoka Zanzibar, walioingia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge wa uwakilishi viti 18 kutoka Pemba na viti tisa kutoka Zanzibar.

“Mpaka sasa CUF ina madiwani zaidi ya 300 nchini na inaongoza halmashauri tano ambazo ni Newala, Tandahimba, Mtwara, Kilwa na Liwale,”alisema.

  Mbunge wa Nchinga, Hamidu Bobali, alisema mgogoro uliopo ndani ya chama hicho umesababisha wanachama kugawanyika.

Alisema kundi linalomuunga mkono Lipumba linawazuia wabunge wanaomuunga mkono Maalim Sief kufanya shughuli za  siasa ndani ya majimbo yao.

“Mimi nipo upande wa Maalim Seif, Mwenyekiti na Katibu wa chama katika Halmashauri ya Nchinga, wapo upande wa Lipumba, kila nikitaka kufanya shughuli za chama  wanakwenda polisi kuweka zuio  jambo ambalo limeniathiri katika siasa,” alisema Bobali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles