28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Corona yaiingiza Marekani, China kwenye vita vipya

WASHINGTON, MAREKANI

MZOZO mkali umeibuka kati ya China na Marekani kuhusiana na virusi vipya vya corona, baada ya Rais Donald Trump kuighadhabisha Beijing kwa kuviita virusi hivyo kama “virusi vya China”.

Kwa siku kadhaa sasa mataifa hayo mawili yamekuwa yakishambuliana kuhusu chanzo cha virusi hivyo vya corona, huku ofisa mmoja wa China akituhumiwa kueneza nadharia za uwongo, akidai kwamba vililetwa nchini humo na jeshi la Marekani na maofisa wa Marekani wakitumia matamshi yanayoonekana yalilenga kuikandamiza China. 

Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter juzi usiku kwamba “Marekani itayasaidia kwa kiasi kikubwa yale mashirika kama ya ndege na mengineyo, ambayo yameathirika sana na Virusi vya China.”

Matamshi yake yamekosolewa vikali ndani ya Marekani, huku kukitolewa onyo kwamba yanaweza kuchochea kisasi dhidi ya jamii yenye asili ya Asia na Marekani.

Washirika wa Trump huko nyuma walilitaja janga hilo kama “virusi vya corona vya China”.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Geng Shuang alionya kuhusu matamshi ya Marekani kuhusu virusi vya corona.

Beijing imesema kwamba imekasirishwa sana na msemo huo ambao imeuita “aina fulani ya unyanyapaa”.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Geng Shuang aliwaambia waandishi wa habari kwamba, Marekani inatakiwa kuacha mara moja madai yake ambayo haijayathibithisha dhidi ya China.

Vita hivyo vya maneno vimeibua wasiwasi wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, ambayo yamekuwa katika mzozo wa kibiashara na mizozo mingine tangu rais Trumo alipoingia madarakani.

Wakati hayo yakiendelea, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, Tedros Adhanom Gebreyesus ametoa wito kwa mataifa kuongeza kiwango cha upimaji kama njia bora zaidi ya kupunguza kusambaa kwa virusi vya corona. Gebreyesus alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi jana.

“Lakini njia bora zaidi ya kuzuia maambukizi na kuokoa maisha na kukata minyororo ya maambukizi, na kufanya hivyo ni lazima kupima na kujitenga. Hauwezi kuzima moto wakati tumejifunika macho na hatuwezi kulizima janga hili ikiwa hatujui ambaye ameambukizwa. Tuna ujumbe rahisi kwa nchi zote: pima, pima, pima. Pima kila kisa kinachotiliwa shaka,” alisema Gebreyesus.

Nchini Ujerumani, kutaanza kuchukuliwa hatua za kuwarejesha raia waliokwama mpakani, wakati mipaka ikifungwa na mashirika ya ndege yakisitisha safari kutokana na janga la corona, hii ikiwa ni kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Heiko Maas, katika wakati ambapo Berlin ikitoa onyo rasmi dhidi ya watu wanaotaka kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya likizo.

Serikali ya Ujerumani imekubali kutumia Euro milioni 50, katika makubaliano iliyoingia na mashirika ya ndege ya kibiashara kuwarudisha raia hao nchini kwao.

Kansela Angela Merkel, juzi aliwaomba Wajerumani wote kusitisha likizo na kutangaza hatua pana za kuwazuia nyumbani ili kukabiliana na kusambaa zaidi kwa virusi hivyo.

Corona yaendelea kusambaa kwa kasi

Wakati mzozo huo ukiendelea, Somalia, Benin na Liberia nazo zimeripoti kesi za ugonjwa wa corona barani Afrika, huku virusi hivyo vikiendelea kusambaa kwa kasi katika nchi za bara hilo.

Waziri wa Afya wa Somalia, Dakta Fauziya Abikar alisema jana kuwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo ni miongoni mwa watu wanne waliokuwa wamewekwa karantini mjini Mogadishu, baada ya kurejea nchini humo hivi karibuni wakitokea China.

Wakati huo huo, Wizara ya Habari ya Liberia imesema, muathirika wa ugonjwa huo ni Mkuu wa Wakala wa Mazingira wa nchi hiyo, ambaye alirejea nchini hivi karibuni akitokea Uswisi.

Juzi Jumatatu pia, Waziri wa Afya wa Benin, Benjamin Hounkpatin alisema nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika ina kesi moja ya Corona, na muathiriwa ni raia wa Burkina Faso ambaye hivi karibuni aliitembelea Ubelgiji.

Kadhalika Serikali ya Tanzania juzi Jumatatu ilitangaza kuwepo mgonjwa wa corona ambaye aliingia nchini Jumapili akitokea Ubelgiji pia.

Kufikia sasa, nchi 30 kati ya 54 za Afrika zimekumbwa na virusi vya Corona, huku jitihada zikiendelea za kuzuia mripuko wa ugonjwa huo katika nchi ambazo hazijaathiriwa na vile vile kuzuia maambukizi zaidi katika nchi zilizoathiriwa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles