27.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Wanawake wameharibu lengo Viti Maalum bungeni – Makinda

Tunu Nassor -Dar es Salaam

MWAKA huu imetimu miaka 25 tangu kuitishwa kwa mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.

Mkutano huo ulikuwa ukiangazia na kutilia mkazo usawa wa kijinsia, maendeleo na amani ambapo wanawake waliohudhulia kwa pamoja walitoa tamko lililoitwa Tamko la Beijing.

Katika mkutano huo, waliweka mpango kazi ulioangazia masuala ya wanawake na umasikini, afya, elimu, ukatili, vita, uchumi, siasa na uongozi, mtoto wa kike na wanawake wa vijijini.

Tanzania iliwakilishwa vyema huku mwanasiasa mkongwe nchini Getrude Mongella, akiwa ndiye Katibu Mkuu wa mkutano huo.

Katika kusherekea jubilee hiyo, wadau mbalimbali wamezungumzia mafanikio na changamoto zilizopo nchini baada ya mkutano huo.

Mmoja wa wadau hao ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na haki za binadamu(LHRC), Anna Henga, anasema mkutano huo umesaidia kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya haki za wanawake.

“Kesi za masuala ya ukatili wa kujinsia zimeongezeka kutokana na jamii kutambua haki ya mwanamke na mtoto wa kike katika nyanja mbalimbali,” anasema Anna.

Anasema hili limechangiwa na kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika vituo vya polisi jambo lililorahisisha wengi kupata sehemu sahihi ya kupeleka malalamiko yao.

Anasema katika hili, bado kuna changamoto ambazo hazijapata ufumbuzi ikiwamo upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati.

“Mila na desturi pamoja na sheria kandamizi zimeendelea kuwa changamoto mfano, sheria ya ukeketaji inataka mtoto chini ya miaka 18 asikeketwe hivyo kutoa fursa kwa wanawake wenye umri zaidi ya huo kukeketwa,” anasema Anna.

Anasema sheria ya mirathi ya kimila inamtambua mwanamke kuwa daraja la tatu baada ya watoto wa mke mkubwa na mke mdogo kupata mirathi.

“Katika kusimamia mirathi, mwanamke atatafutiwa mtu wa kusimamia mirathi na familia…Hii imewafanya wanawake wengi kurithi vyombo kama bakuli huku watoto wakiacha shule kwa kukosa ada,” anasema Anna.

Anasema sheria bado zinaruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 15 kuolewa kwa idhini ya wazazi wake jambo linaloruhusu ndoa za utotoni kuendelea kuwapo.

“Sheria hii tunaipinga mahakamani na tayari tumekwisha kufungua jalada,” anasema Anna.

Anasema tamko la kimila bado linaruhusu wanawake kupigwa jambo ambalo ni kinyume na haki za binadamu.

Naye Ofisa Miradi wa Jinsia, Wanawake na Watoto kutoka LHRC, Getrude Dyabene, anasema moja ya mpango kazi wa mkutano huo ulikuwa ni kupambana na umasikini kwa wanawake.

Anasema kwa hapa nchini, wanawake wengi wamekuwa wakipambana na umasikini kwa kuwa wajasiriamali.

Anasema wamekuwa wakijiunga katika vikundi vya vikoba ili kupata mitaji na uwezo wa kifedha.

“Wanawake sasa wamepata uhuru wa kiuchumi na kuwa na uwezo wa kufanya uamuzi wa fedha wanazopata kupitia ujasiriamali na mishahara ya kazi zao,” anasema Getrude.

Anasema sambamba na hilo, pia wanapata mikopo kupitia halmashauri na taasisi nyingine za kifedha zilizosaidia kuanzisha biashara na ujasiriamali.

Anasema changamoto katika hili ni wanaume kuingilia umiliki mali zao wanazozalisha kuwa chini ya wanaume.

Anasema pia upatikanaji wa mikopo inayotolewa na taasisi zisizo za kiserikali nyingine kuwa riba kubwa na kusababisha mzigo mkubwa wa madeni.

Akizungumzia elimu, anasema mafanikio yamepatikana kwa watoto wa kike kufanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya kitaifa.

Anasema idadi ya watoto wa kike wanaochagua kusoma masomo ya sayansi imeongezeka na wengi wao wanafanya vizuri katika mitihani ya mwisho.

 Anasema mafanikio kwa upande wa afya ni kuboreshwa kwa huduma ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa vituo vya afya na zahanati nyingi nchini.

“Mafanikio mengine ni ushirikishwaji wa wanaume katika masuala ya uzazi ambapo kwa sasa wanaongozana na wenza wao kwenda kliniki ya baba, mama na mtoto,” anasema Getrude.

Anasema changamoto zilizopo katika sekta hii ni umbali wa kuzifikia hospitali na kuongezeka kwa vifo vitokanavyo na uzazi kwa mama na mtoto.

Anabainisha kuwa Katiba ya nchi haitamki kuwa haki za wanawake ni zipi jambo ambalo limebaki kwenye sheria tu.

Anasema kwa upande wa ajira, nafasi nyingi kwa sasa zinazotoa fursa kwa wanawake kuomba lakini changamoto inakuja kwenye malipo ambayo hayana usawa na wanaume.

Anasema wanawake wamepiga hatua kubwa kutoka kwenye uamuzi wa fedha wanazopata tofauti na awali ambapo alilazimika kukabidhi kwa mumewe.

“Bado kuna wanaume wanaowanyang’anya mishahara wanawake na kuwaacha wakiwa hawana fedha za kujikimu,” anasema Getrude.

Anasema ubaguzi wa ajira katika baadhi ya taasisi na unyanyapaa na changamoto ya kulea familia bado ni mzigo mkubwa kwa wanawake.

Anasisitiza kuwa pamoja na wanawake wengi kujiingiza katika ujasiriamali, changamoto inakuja katika ukosefu wa masoko ya bidhaa wanazozalisha.

Anasema katika suala la uongozi, wanawake wamefanikiwa kushika nafasi mbalimbali nchini ikiwamo umakamu wa rais, spika wa bunge wakuu wa taasisi na idadi kubwa wanagombea.

“Changamoto iliyopo katika hili ni ubaguzi katika utoaji wa nafasi za uongozi na uteuzi wa wagombea mfano, vyama vya siasa kushindwa kuwateua wanawake wenye uwezo wa kuongoza kwa sababu tu jimbo lile wakimweka mwanamke watashindwa na vyama vingine,” anasema Getrude.

Anasema bado kuna changamoto katika uteuzi wa viti maalumu ambavyo vimekuwa vikitolewa bila usawa kwa wanawake.

Anasema hata hivyo, baadhi ya maeneo, jamii imeshindwa kuwakubali wanawake kuwa wanaweza kuongoza hivyo kuwanyima kura.

Akizungumzia changamoto za ndoa, anasema kumekuwapo ugumu kwa mwanamke aliyeolewa na mwanamume kutoka nje ya nchi mumewe kupata uraia.

“Mwanaume anapooa mwanamke asiye raia mkewe hupata uraia kwa urahisi tofauti na mwanamke anapoolewa na mume asiye raia,” anasema Getrude.

Akizungumzia mkutano wa Beijing, Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda, anasema mwaka 1995 akiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, alishiriki kuandaa mkutano huo.

“Sikufanikiwa kwenda Beijing kwa sababu ulikuwa mwaka wa uchaguzi na nilikuwa nagombea katika Jimbo la Njombe,” anasema Anna.

Chanzo kuanzishwa Viti Maalum

Anasema tangu alipokuwa mdogo alipenda kupigania haki za wanawake kuona kuwa wanashika nafasi mbalimbali za uongozi.

Anasema kipindi hicho Tanzania Bara kulikuwa na mbunge wa kike mmoja na Zanzibar walikuwa sita.

“Tulianza kupambana kuhakikisha tunaongeza uwakilishi wa wanawake bungeni ambapo tulifanikiwa kupata viti maalumu kwa asilimia 15,” anasema Anna.

Anasema waliendelea kupambana kwa kuwabana watunga sera na kufanikiwa kuongeza hadi asilimia 20 na sasa imefikia asilimia 35.

Anasema lengo la viti maalumu lilikuwa ni kuwajengea uwezo wanawake ili waweze kugombea majimboni na kuongeza idadi ya wabunge.

Anasema pia walitegemea kupitia viti maalumu wanawake wengi watajengewa uwezo na kupambana na wanaume majimboni jambo ambalo limekuwa kinyume na matarajio yao.

Anashangaa kuona wanawake ambao wamepitishwa kupitia viti maalumu kuendelea kung’ang’ania viti hivyo tofauti na lengo la kuanzishwa kwake.

“Si sifa njema kwa wabunge wa viti maalumu kuendelea kushikiria viti hivyo kwa zaidi ya miaka 40.

“Wanawake tunaitumia vibaya nafasi hiyo kwa kuzikalia kwa muda mrefu bila kuwapisha wengine.

“Tulianzisha utaratibu wa viti maalumu ili iwe sehemu ya kupata uzoefu ukagombee na kama huwezi unatakiwa ukafanye kazi zingine,” anasema Makinda.

Anasema hadi sasa majimbo yanayoongozwa na wabunge wanawake ni asilimia sita pekee huku kila uchaguzi yanachukuliwa na wanaume.

“Njia ya kuweza kuwa na uwakilishi wa wabunge wengi wa kike ilikuwa ni viti maalumu lakini haikutumika ipasavyo jambo ambalo linachelewesha kufikia 50 kwa 50,” anasema.

Bisimba anena

Naye Mkurugenzi Mstaafu wa LHRC, Dk. Hellen Kijo Bisimba, anasema yeye ni mmoja wa waliokwenda Beijing katika mkutano huo.

“Kwa Afrika, tulikutana nchini Senegal kujadili jambo tutakalozungumza huko Beijing. “Waliniteua kuwa mmoja wa walioingia katika mkutano wa viongozi wa serikali Dunia nzima,” anasema Bisimba.

Ansema katika tamko la Beijing lilikoluwa na mpango kazi uliongazia mambo 12, Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika baadhi ya mambo.

Anasema serikali imefanikiwa kutengeneza sheria ya ardhi ya mwaka 1999 ambapo ibara ya pili inatoa haki ya kumiliki kwa usawa japo utekelezaji bado.

Anaongeza kuwa kwa upande wa ukatili wa kijinsia sheria nzuri ipo japo kuna changamoto katika suala la ukeketaji linalotoa mwanya kwa wanawake wanaozidi miaka 18 kufanyiwa vitendo hivyo.

“Sheria inakataza kumkekeketa mtoto aliyechini ya umri wa miaka 18 hivyo kutoa fursa kwa wazazi watoto wao wanapofikisha miaka 19 kuwakeketa,” anasema.

Anasema kwa upande wa elimu hatua kubwa imepigwa kwa watoto wengi wa kike kupata fursa ya kwenda shule.

“Bado tunapambana kuhakikisha tunafanikiwa kuwarudisha shuleni watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni.

“Tulifikia pazuri katika maongezi na wizara lakini zimejitokeza changamoto ambazo ndizo tunapambana nazo,” anabainisha.

Naye Mwanaharakati Mary Ndalo, anasema kundi la wanaume limeachwa nyuma kupata elimu juu ya haki za wanawake.

“Ni vyema kuwaelimisha wanaume kuwa si kila mwanamke ni mali yao na mwanamke atachagua ni wakati gani atamuhitaji na si kila wakati,” anasema Mary.

Anasema baadhi ya wanawake wanashirikishwa katika uzalishaji lakini hawahusishwi katika mali wanazozalisha katika familia na kubaki kuomba kwa wenza wao.

“Mfano asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima wakiwamo wanawake ambao hulima aidha sawa na wanaume katika familia au zaidi, lakini wakati wa kuuza mazao hawashirikishi na wenza wao hivyo tunaweza kusema asilimia kubwa ya wanawake hawashirikishwi katika mapato,” anasema Mary.

Anasema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi wa kike shuleni, idadi hiyo hupungua kutokana na mimba za utotoni.

“Kuna idadi kubwa ya wasichana wanaobeba mimba na kufukuzwa shule hivyo kuongeza idadi ya wanawake wasiokuwa na elimu na kuzalisha wanawake tegemezi,” anasema Mary.

Anaongeza kuwa pamoja na kupata ujauzito, bado kujifungua ni bahati nasibu kwa kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi bado iko juu.

Naye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mkutano huo Getrude Mongella anasema ni jambo la kujivunia kufikisha miaka 25 baada ya mkutano huo.

Anasema kama nchi mengi yamefanyika na hatua kubwa zimefikiwa katika kupambania haki za wanawake.

“Namshukuru Mungu kuwa nimefanya mambo mengi na kubadilisha fikra watu wengi huku nikishuhudia mafanikio kupitia mkutano huu,” anasema Mongella.

Anasema mkutano huo ulifungua njia kwa wanawake kujitambua na sasa ni jukumu la kila mmoja kupambana kutafuta haki.

“Mambo mengine tunahitaji kupambana wenyewe kuyatafuta kwa sasa kwa kuwa sheria nyingi zimeturahisishia hivyo ni jukumu letu kumalizia kazi hii,” anasema Mongella.

Anasema alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Mkutano huo alikabidhiwa ofisi ikiwa haina fedha za kuendeshea mkutano huo na watumishi 12 tu ikabidi afanye juhudi za kutafuta fedha.

“Ukipewa kitu kizito ndio kinakupa ujasiri wa kufanya kazi nami nashukuru kwa kuwa nilitafuta fedha kupitia wafadhili wakaweza kunisaidia na mkutano ukafanikiwa,” anasema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,554FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles