25.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

Chuchu bandia hatari unyonyeshaji watoto

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

OFISA lishe mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Fatuma Mwasora amesema chupa na chuchu bandia ni hatari kwa afya ya mtoto kutokana na chuchu hizo kujaza gesi tumboni na kupunguza kiwango cha unyonyaji wa mtoto.

Katika mahojiano maalumu na MTANZANIA, Dar es Salaam mwishoni mwa maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Agoti mosi hadi 7, Fatuma alisema madhara zaidi ya chuchu hizo na chupa humfanya mtoto akatae kunyonya  maziwa ya mama na hivyo kukosa virutubishi vinavyotakiwa.

 “Hili ni hakika mtoto anapopewa chupa au chuchu bandia atakataa kunyonya maziwa ya mama yake, akiwekewa chuchu ya mama mdomoni ataanza kufananisha, ataona kama kuna utofauti, ataona hili sio ziwa lenyewe. 

“Kitu kingine ambacho watu wanaona ni fasheni, wanachukua zile chuchu wanamwekea mtoto mdomoni kutwa nzima mtoto anashinda nacho, hapa anavuta hewa hapati virutubishi wala hapati chakula kutoka kwa mama yake.

“Akivuta hewa inamjazia gesi  tumboni, watoto wa aina hii mara nyingi wanakuwa wanalialia sana kwa sababu hawapati chakula cha kutosha, na watoto wa namna hii wanakuwa wamedhoofu kwani gesi ikijaa tumboni wanashindwa kunyonya inavyotakiwa,” alisema Fatuma.

Alisema madhara mengine ya kutumia chupa kumlishia mtoto ni kutokuzingatiwa kwa usafi wa chupa hizo, hilo humfanya kupata magonjwa.

 “Unakuta chupa nyingi hazifanyiwi usafi, ni hatari kwa afya ya mtoto, kuna sheria inayomlinda mtoto, miongozo inamtaka kila mama anayejifungua amnyonyeshe mtoto ndani ya saa moja apate maziwa na virutubishi vya kutosha, pia maziwa ya mama yanakinga kwa mtoto na kumnyonyesha kwa kipindi cha miezi sita pasipo kumchanganyia kitu chochote.

 “Akipewa chuchu au chupa bandia inamkosesha nafasi ya kupata maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita, matokeo yake mtoto anapata utapiamlo  kwa sababu anatakiwa kunyonyeshwa kwa miaka miwili na nusu, inamaana akikataa kunyonya atakosa virutubishi vilivyoko kwenye maziwa ya mama,” alisema Fatuma.

Alieleza kadiri mama anavyomnyonyesha mtoto ndivyo maziwa yanavyozidi kutengenezwa.

“Ni muhimu mtoto kunyonya maziwa ya mama mara kwa mara,” alisema Fatuma.

 Alisema njia salama ya ulishaji wa mtoto kwa maziwa ya mama yanayokamuliwa ni kumpa kwa kikombe pekee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,637FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles