24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 30, 2023

Contact us: [email protected]

Waliofariki dunia ajali lori la mafuta Moro wakumbukwa

Na Ashura Kazinja -Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Loata ole Sanare amewaongoza viongozi wa dini, Serikali na wananchi wakati wa ibada maalumu ya kuwaombea watu waliopoteza maisha wakati wa  ajali ya moto, baada ya lori la mafuta kuanguka na kulipuka.

Ajali hiyo iliyotokea Agosti 10, mwaka jana  ilisababisha vifo vya watu 115 ambao walizikwa makaburi ya pamoja eneo la Kola, Manispaa ya Morogoro na wengine 21 walijeruhiwa.

Akizungumza wakati wa ibada iliyofanyika jana, Sanare alisema mkoa unafanyia kazi maombi ya wadau mbalimbali ya kutaka kujengwa njia ya mchepuko kwa magari yanayobea mafuta, kemikali na sumu.

 “Kuwepo njia ya mchepuko kwa ajili ya magari makubwa yanayobeba mafuta, kemikali na sumu itakayopita nje ya mji, itasaidia kupunguza ajali zisizo za lazima, kuna changamoto ya tabia ya watu kufuata barabara ilipo bila kujali athari zitakazojitokeza,” alisema.

Alisema pamoja na mambo mengine, mamlaka husika zinapaswa kuwajengea uwezo madereva wanaosafirisha mafuta umbali mrefu ili wawe na tahadhari ya ajali sambamba na kuimarishwa utaratibu wa kutumia madereva wawili ili kusaidiana pindi mmoja anapochoka.

Sanare alisema licha ya kuwapo sheria inayowataka wamiliki wa magari makubwa yanayosafiri umbali mrefu kuwepo na madereva wawili, bado baadhi ya wamiliki wamekuwa wakikiuka sheria hiyo na kuwafanya madereva hao kuchoka wakiwa safarini na kusababisha ajali.

Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Mohamed Salum alimshukuru Mungu kupona katika tukio hilo.

Pia aliwashukuru wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Namshukuru Mungu kupona kwenye  ile ajali, namshukuru Rais wetu, John Magufuli kwa kuboresha huduma za afya na kusaidia madaktari, hasa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na Hospitali ya Taifa Muhimbili, walitusaidia mno,” alisema Salum.

Ashura Ramadhani aliyefiwa na mume wake katika ajali hiyo, aliiomba Serikali  kuwasaidia, ikiwemo kuwapa mtaji kwani baadhi yao wamejikuta katika majukumu mazito  wanayoshindwa kuyamudu kutokana na kuondokewa na watu muhimu ambao walikuwa wakiwategemea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,285FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles