31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mfumko wa bei waongezeka

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MFUMUKO wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia Julai, mwaka huu, umeongezeka hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.2, kwa mwaka ulioishia  Juni, mwaka jana, huku baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula zikitajwa kuchangia.

Hayo yalielezwa jijini Dodoma jana na Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema hali hiyo inamaanisha kasi na mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Julai, mwaka huu, imeongezeka kidogo ukilinganisha na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Juni, mwaka huu.

Ruth alisema baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka bei kwa Julai, mwaka huu  zikilinganishwa na bei za Julai mwaka jana, ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 7.9, mtama kwa asilimia 4.8, unga wa muhogo kwa asilimia 3.0, dagaa kwa asilimia 3.8, matunda kwa asilimia 4.0 na mbogamboga kwa asilimia 9.6.

Alisema kwa upande wa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei kwa Julai, mwaka huu, zikilinganishwa na bei za Julai, mwaka jana, ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.8, gesi ya kupikia kwa asilimia 5.9, samani kwa asilimia 2.7, gharama za utengenezaji na ukarabati wa nyumba kwa asilimia 6.2 na mkaa kwa asilimia 11.6.

Ruth alisema mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji baridi kwa Julai mwaka huu, umebaki kuwa asilimia 3.8 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2020.

Alisema hali ya mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia Julai, mwaka huu nchini Kenya umepungua hadi kufikia asilimia 4.36 kutoka asilimia 4.59.

Ruth alisema kwa nchi ya Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Julai umeongezeka hadi asailimia 4.7 kutoka asilimia 4.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles