CHENGE, NGELEJA, KAFUMU WAVUNJA UKIMYA

0
655

 

 

Na Fredy Azzah-Dodoma

VIGOGO waliotajwa katika ripoti ya pili ya kuchunguza makontena yenye mchanga wa madini (makinikia)  kuisababishia Serikali hasara ya matrilioni ya fedha kupitia sekta ya madini, walipokuwa wakihudumu katika nyadhifa zao serikalini wamevunja ukimya.

Vigogo hao wamezungumzia ripoti hiyo ya pili iliyowasilishwa kwa Rais Dk. John Magufuli Ikulu Dar es Salaam jana, ambapo kamati husika ilichunguza hasara ambayo nchi imepata tangu 1998 usafirishaji wa mchanga wa dhahabu nje ya nchi ulipoanza.

Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (CCM), alipoulizwa maoni yake juu ya kutajwa na kamati hiyo, alisema hataki kuzungumza chochote juu ya ripoti hiyo, huku Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), akisema sheria ya madini ya 2010 ingefuatwa, nchi isingekuwa hapa ilipo.

Kwa upande wake Kamishna wa Madini wa zamani, Dk. Dalaly Kafumu, alisema kwa sasa  hawezi kuzungumza jambo lolote kwa kuwa ni yeye ni mmoja wa watuhumiwa waliotajwa kwenye ripoti hiyo.

Chenge

Baada ya kutoka kwenye kipindi cha asubuhi cha Bunge ambacho alikuwa akikiendesha, Chenge alipotakiwa kuzungumzia ripoti hiyo, alijibu kwa ufupi.

“Sizungumzi na mtu,” na alipoulizwa kama hata salamu hataki, alisema. “Sizungumzi na mtu mimi,” alisema Change ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Chenge alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kati ya 1972 na 1990, ambapo mwaka 1993 aliteuliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali nafasi ambayo alidumu nayo hadi mwaka 2005.

Dk. Kafumu

MTANZANIA ilimpomtafua Mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu (CCM), ambaye ametajwa kutaka kuingilia ripoti ya kamati ya kwanza iliyochunguza mchanga huo, alisema hataki kuzungumza chochote kwa sasa ingawa anaamini kila kitu kiko sawa.

“Kwa kuwa nimetajwa kama mtuhumiwa, sitaki kusema kitu kwa sasa kwa sababu hili ni sawa na jambo lililo mahakamani tu kwa kuwa wamesema tutahojiwa, lakini kila kitu kiko sawa,” alisema Dk. Kafumu.

Alipoulizwa kama ni kweli alikutana na Profesa Abdulkarim Mruma, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ya kwanza na ni nini walichozungumza, Dk. Kafumu alisema. “Nimeshasema no comment (sina la kusema ),” alisema Dk. Kafumu.

Dk. Kafumu ni moja ya watumishi waliohudumu ndani ya Wizara ya Nishati na Madini ambapo alifanyakazi kazi ndani ya wizara hiyo kuanzia mwaka 1983 hadi 2011, alipoacha na kwenda kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa marudio wa Igunga, baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Rostam Aziz.

Taarifa zilizopo kwenye tovuti ya Bunge zinaonesha, mwaka 1983 mpaka 1987, Dk. Kafumu alikuwa mtaalamu wa miamba na madini wa wizara hiyo, mwaka 1987 mpaka 1992, mkufunzi na mtafiti wa madini, mwaka 1992 mpaka 2002 akawa mtaalamu mwandamizi wa madini, mwaka 2002-2004, mtaalamu wa miamba mkuu na mbobezi  wa madini, mwaka 2004-2006, alikuwa ofisa mawasiliano na mwaka 2006 mpaka 2011, alikuwa kamishna wa madini.

Ngeleja

Kwa upande wake Ngeleja aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, kuanzia mwaka 2008 hadi 2012, alisema hataki kuzungumzia juu ya kilichoelezwa na kamati hiyo ikiwamo kutajwa kwake, bali anachoweza kusema ni kuwa, Rais Magufuli ameonesha uzalendo. 

“Sitaki kuzungumza yaliyo kwenye ripoti ya uchunguzi, ila tu nisema kwa wale tuliosikiliza wakati ripoti inawasilishwa na wakati Rais mwenyewe anazungumza, unaona hisia za uzalendo ambazo Rais anazo, na ameeleza kwa uchungu mkubwa namna ambavyo tunastahili kupata zaidi kuliko tunachopata sasa.

“Lakini jambo kubwa alilolifanya, amesema atamkabidhi taarifa (Spika wa Bunge), kwa sababu msingi wa mambo yote haya ni sera na sheria za nchi.

“Kwamba sisi kama Bunge tutimize wajibu wetu tuhakikishe mapungufun yote yaliyo pale tunayafanyia kazi, lakini kikubwa  amesema chenji (fedha zilizokwepwa na migoni) yetu irudi na amewakaribisha wawekezaji wakae mezani, lakini baada ya kuzingatia masilahi ya upande wetu, ni jambo jema.

 “…wakati nachangia bajeti ya Wizara ya Nishati nilisema, sheria hata tuliyo nayo sasa tungekuwa tumeitekeleza vizuri tusingekuwa hapa tulipo na moja ni kuhusu mikataba iliyofungwa kabla ya mwaka 2010,” alisema

Alisema kifungu cha 116 cha Sheria ya Madini, kinasema mikataba yote iliyofungwa kabla ya kutungwa kwa sheria ya madini ya mwaka 2010, inatakiwa iheshimu na  itambulike kwa utaratibu wa sheria hiyo.

“Kwenye kifungu cha 11 cha hii sheria ya madini, inasema kila baada ya miaka mitano baada ya kuanza kutumika hii sheria, mikataba yote ya madini ipitiwe upya.

“Mimi nilijiuzulu uwaziri Mei 4, 2012, sasa ni miaka mitano imepita, na wakati najiuzulu mimi tulikuwa tumemaliza kutunga kanuni, ninachotaka kusema ni kwamba kupitia hicho kifungu cha 11 hilo ndilo dirisha la kujadiliana yale ambayo kipindi kile kilishindikana,” alisema

Waziri huyo wa Nishati na Madini wa zamani, alisema kuwa kifungu cha 10 cha sheria hiyo kimeweka wazi namna Serikali inavyoweza kumiliki hisa kimkakati kwa kutumia dirisha hilo.

“Utaratibu huo ndiyo tumeutumia kwa Mchuchuma na Liganga, ambapo serikali ina asilimia 20 za bure, Ngaka ina asilimia 30 za bure, hayo ndiyo niliyosema,” alisema Ngeleja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here