MAGUFULI AIKUBALI RIPOTI YA KAMATI

0
603
Rais Dk. John Magufuli, akipokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa mchanga wa madini kwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Nehemiah Osoro, Ikulu Dar es Salaam jana. Kushoto ni Spika wa Bunge, Job Ndugai. Picha na Loveness Bernard

 

 

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amekubali mapendekezo ya kamati ya pili kuhusu Ripoti ya Kamati ya kuchunguza mchanga wa madini kwa asilimia 100.

Kutokana na hali hiyo amevitaka vyombo vya dola kuwahoji wahusika wote waliotajwa katika ripoti hiyo.

“Mapendekezo nimeyapokea na kuyakubali kwa asilimia 100, iwe bado uko serikalini, nje ya serikali, unafanya biashara zako kama Karamagi, vyombo vya dola vifuatilie wahojiwe watoe ushirikiano ili kusudi ukweli upatikane katika suala hili.

“Wizara zote zidai fedha zetu na Acacia wakitubu kwamba walituibia na wakasema wako tayari kufanya biashara, tutakuwa tayari kwa majadiliano na ninasema hakuna mchanga kutoka nje,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Sheria ya madini kupitiwa upya

Alimuagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, kuunda timu ya wanasheria kwa ajili ya kupitia upya sheria zote za madini ili zifanyiwe marekebisho.

“Wanasheria wasimame katika hili kwa ajili ya masilahi mapana ya Taifa, sheria za madini, gesi zote zipitiwe. Na wewe profesa (Waziri wa Katiba na Sheria), ukishindwa hizi sheria ndogo ndogo nitakushangaa.

“Mkawe na timu ya wanasheria si wale wanaohongwa hongwa, ni nafuu tuchelewe lakini tuwe na sheria nzuri…Nyerere alisubiri kwanza, tutangulize Tanzania badala ya masilahi binafsi.

“Wako wengine wanatisha, mtu anapayuka na mdomo wa ajabu, tumechezewa vya kutosha haiwezekani tukawa sisi ndio wa kuibiwa tu,” alisema.

Alisema kama ikibidi atamwomba Spika wa Bunge, Job Ndugai, waongeze muda wa Bunge ili kuzifanyia marekebisho sheria hizo.

Alitolea mfano wa mkataba wa uchimbaji madini ya almasi ambao uliingiwa tangu mwaka 1949 lakini hadi sasa serikali haijawahi kupata gawio huku hisa zake zikiwa zimeshushwa kutoka asilimia 50 hadi kufikia asilimia 35.

Alisema baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali zilizopo wamekuwa hawajali maisha ya Watanzania bali masilahi yao binafsi.

 “Kwa Mtanzania yoyote mwenye akili timamu ukisikia ripoti kama hii inatia uchungu sana. Ninashindwa nianzie wapi, nizungumze nini katika ripoti hii.

“Mungu alitupenda Watanzania, alituwekea maliasili nyingi ziwanufaishe Watanzania. Kila kitu kipo, madini, gesi lakini pamoja na haya tumeendelea kuwa masikini. Hata shetani anatucheka kwamba umaskini wetu ni wa kujitakia,” alisema.

Alisema wako watoto wanaokufa kwa sababu ya kukosa dawa na wengine wanakufa kwa sababu ya miundombinu mibovu ya usafiri wa majini, maji na wakulima wanakosa pembejeo wakati mali zipo.

“Wakati mwingine tunakopa kwa masharti ya ajabu ajabu wakati mali tunazo, waliopewa madaraka ya kusimamia rasilimali zetu wamekuwa chanzo cha kuwaibia masikini,” alisema.

Rais Dk. Magufuli alisema licha ya kuwapo kwa makampuni yaliyokuwa tayari kujenga mashine ya kuchenjulia makinikia lakini hayakuruhusiwa na badala yake yalipigwa danadana tu.

 “Kuanzia waziri hadi wataalamu wake wanaambiwa makinikia yanapelekwa kwenye smelter wala hawajiulizi hata siku moja kwenda kuangalia, wanaomba kibali cha kusafiri Ulaya lakini hawataki kwenda kuangalia kwenye smelter.

“Makampuni mengi yalikuja na kutaka kujenga smelter lakini hayaruhusiwi, makampuni ya kujenga chuma, saruji, vigae yanaruhusiwa ambayo yanayeyusha vitu vugumu kuliko dhahabu yanaruhusiwa. Hili ni soko la ajabu, madini yetu yanasombwa tunabaki hatuna kitu watu wenyewe (wawekezaji) hawana huruma hata kulipa kodi wanakwepa.

WACHIMBAJI WADOGO

Alisema katika maeneo mbalimbali ya nchi wachimbaji na wafanyabiashara wadogo wadogo wamekuwa wakinyanyaswa kwa hoja kwamba wamevamia maeneo ya wawekezaji na kufanya biashara bila kuwa na leseni. 

“Wachimbaji wadogo wakijaribu kuchimba wanafukuzwa na kuambiwa eti eneo ni la mwekezaji, mwekezaji gani ambaye hana rekodi kwa mahala alipofanyia uwekezaji?

“Acacia haina usajili unaotambuliwa kisheria lakini inafanya biashara ya matrilioni, tujiulize sisi viongozi ni mara ngapi Watanzania wenzetu wasiposajiliwa tunawashughulikia kwa mitutu ya bunduki.

“Wamachinga wanafukuzwa kwenye maeneo yao ya kufanyia kazi, ni mara ngapi wafanyabiashara wa maduka madogo madogo ambao hawana leseni tunavyowashughulikia sisi viongozi.

 “Tunafukuzana na watoto maskini kuwaomba kodi wakati kodi ambayo ipo tumepewa na Mungu hatuishughulikii, ni unyama mkubwa. Tunaambiwa sisi masikini na hawa watu wanatudharau sana…tumechezewa mno, tunahitaji wawekezaji kutoka kokote kule lakini ‘we are support to share the profit,” alisema.

BENKI KUU

Rais Dk. Magufuli alisema Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ndiyo wasimamizi wa mwenendo wa uchumi na ina watalaamu 17 wenye shahada za uzamivu (Phd) lakini akashangaa imeshindwaje kuwa na kumbukumbu za madini yanayosafirishwa.

“Unaweza kujiuliza maswali mengi, Pamba, Korosho wanarekodi lakini dhahabu hawakurekodi, kwani hawajui kama tunachimba, waliuliza wakanyimwa hizi takwimu…ndiyo Tanzania ilipofikia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here