RIPOTI YA PILI YA MAKINIKIA: VIONGOZI WAMPONGEZA JPM

0
726
Rais Dk. John Magufuli

 

 

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

VIONGOZI wa dini, wanasiasa na wadau mbalimbali wamempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi aliouchukua wa kuunda kamati ya kuchunguza mchanga wa madini katika makontena 277 yanayoshikiliwa.

Viongozi hao walitoa maoni hayo muda mfupi baada ya Rais Magufuli kupokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa mchanga wa madini (makinikia), Ikulu Dar es Salaam jana.

 BUTIKU

Akizungumza kwa niaba ya wazee, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Butiku alimpongeza Rais Magufuli huku akiwataka walio chini yake wamsaidie.

Aliwaomba wazee wenzake waendelee kumwunga mkono Rais na wasiwe wazee mradi bali wawe wazee wanaomshauri mkuu huyo wa nchi.

“Mzee Cheyo, mzee Mrema, msiwe wazee mradi wazee bali mumshauri hata kusema unajua Rais kuna… Kusoma tumesoma lakini ujasiri hatuna, nishukuru kwamba tunaye msomi mmoja jasiri ambaye ni Rais. Usisite kutuita, kutuuliza na tutakusaidia,” alisema Butiku.

SPIKA NDUGAI

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema ataunda timu yake itakayofuatilia suala la madini ya almasi.

Pia alimwahidi Rais Magufuli kuwa sheria zitakazopelekwa bungeni watazirekebisha kwa masilahi ya Watanzania.

Alisema kwa kushirikiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye ni kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, watasaidiana kuunda timu hiyo ili kumsaidia Rais katika masuala ya madini.

“Kabla Bunge hili la bajeti halijaisha, nitaunda timu kufuatilia suala la madini ya almasi. Tayari nilishaunda timu ya kuchunguza suala la madini ya Tanzanite. Kwa pamoja, Rais ukienda huko na sisi tukienda huku, tutafika,”alisema Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa.

KINANA

Naye Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alimpongeza Rais Magufuli akisema amekubali kuwajibika kama kiongozi wa wananchi.

“Rais anastahili kupongezwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi na sasa amekubali kulinda na kusimamia rasilimali zetu,”alisema Kinana.

ASKOFU CHIMELEDYA

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya ambaye pia ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria tukio hilo, alisema ripoti hiyo aliyokabidhiwa mkuu wa nchi ni nzuri lakini inayoumiza na kwamba Mungu hakuumba Tanzania iliyo masikini bali usimamizi mzuri na uadilifu ulikosekana.

“Mungu naye ana maono na watu wake…lazima tushikamane kila mtu na nafasi yake, pasipo kuangalia dini zetu na vyama vyetu. Ni wajibu wetu kuyatunza madini yetu,”alisema askofu Chimeledya.

Mufti Zuberi

Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zuberi bin Ally, alisema juhudi aliyonayo Rais Magufuli ni kubwa na kwamba ripoti hiyo imeonesha ukweli na uzalendo.

“Nimefurahishwa sana na ripoti hii kwani imeonesha ukweli na uzalendo. Juhudi aliyonayo Rais ni kubwa mno. Maagizo aliyoyazungumza Rais Magufuli yako sahihi, kuna umuhimu sasa wa kujenga nidhamu hapa nchini,” alisema Mufti Zuberi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here