25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Chemba watakiwa kuweka mikakati madhubuti ya ukusanyaji mapato

Na Ramadhan Hassan,Chemba

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma limeitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo kuweka mikakati madhubuti ya ukusanyaji mapato ikiwemo kuitumia chanjo ya mifugo kama chanzo cha kujiingizia mapato.

Wakizungumza jana katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Wilayani Chemba,Madiwani hao wamesema bado kuna changamoto ya ukusanyaji mapato katika Halamshauri hiyo hivyo kunahitajika jitihada za dhati ili kukusanya mapato vizuri.

Diwani wa Kata ya Tumbakose, Elisha Kaka amesema chanjo ya mifugo ni njia nzuri ya Halmashauri kujiingizia kipato hivyo wanaohusika wanatakiwa kuisimamia vizuri kwa kuhakikisha inafika kila mahali katika Wilaya hiyo.

“Ukusanyaji wa  fedha katika chanjo sio mzuri, mfano mnada wa Makongoro pale kuna upotevu mkubwa wa mapato halafu hii chanjo kuna sehemu wamefanya sehemu zingine hawajafanya sasa hatuoni kwamba tunapoteza mapato,”amesema.

Naye, Diwani wa Kata ya Jangalo, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Abdi Msuri, amesema walikubaliana chanjo hiyo ifanyike kila sehemu katika Wilaya hiyo lakini wanashangaa kufanyika katika  baadhi ya maeneo hivyo Halmashauri kukosa mapato.

Hata hivyo, Msuri ameiomba Halmashauri hiyo kuwarejesha kazini  watendaji 50 wa Halmashauri hiyo ambao walisimamishwa kazi kwani wamesababisha makusanyo kushuka.

Akilitolea ufafanuzi hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Jofrey Pima amesema zoezi la utoaji wa chanjo lilianza mwaka jana lakini lilikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa dawa hivyo zoezi hilo linatarajiwa kuendelea hivi karibuni.

“Awali zoezi letu lilianza vizuri lakini baadae tulipata changamoto kwani mahitaji yalikuwa makubwa hivyo dawa zilihitajika kwa wingi sasa tumejipanga na zoezi litaendelea na tutahakikisha chanjo inafanyika katika kila eneo katika Halmashauri yetu,”amesema.

Pia, Kaimu Mkurugenzi huyo amesema mikakati ya kuongeza mapato katika Halmashauri hiyo ni pamoja na kuongeza wigo wa vyanzo vya ukusanyaji mapato,ujenzi wa Stand mpya ya mabasi,usimamizi madhubuti, kuongeza mashine za ukusanyaji mapato za Poss na kuimarisha uadilifu katika ukusanyaji mapato.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halamshauri hiyo, ambaye pia ni Diwani wa Mondo, Sambala Said amesema Halmashauri hiyo imeanza kujitathmini upya katika masuala ya uchumi,mipango na fedha kwa kuviboresha vyanzo vipya na kuweka mazingira wezeshi pamoja na kuwa na mashine za kutosha za ukusanyaji mapato.

Katika kikao hicho yaliulizwa maswali ya papo kwa papo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo na pia ziliwasilishwa taarifa za maji, barababa, ukimwi,uchumi na fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles