LONDON, ENGLAND
CHAMA cha soka nchini England (FA) kimezitoza faini Klabu ya Chelsea na West Ham kutokana na utovu wa nidhamu uliooneshwa katika mchezo wa Ligi Kuu huku Chelsea ikiambulia kichapo cha mabao 2-1.
Chelsea wao wametozwa faini ya pauni 50,000 wakati West Ham ikitozwa pauni 40,000 kutokana na kukiri mashtaka ya utovu wa nidhamu ulioonyeshwa Oktoba 24 kwenye Uwanja wa Upton Park. Wachezaji watano wa Chelsea walioneshwa kadi za njano huku kiungo wao wa kati Nemanja Matic akioneshwa kadi nyekundu pamoja
na kocha wa klabu hiyo, Jose Mourinho baada ya kumshambulia mwamuzi wa mezani.
Kutokana na tukio hilo, Mourinho alisimamishwa kuhudhuria mchezo mmoja wa Ligi Kuu huku timu yake ikicheza na Stoke City na ametakiwa kulipa faini ya pauni 40,000.
Wachezaji wa West Ham walionekana kumzingira mwamuzi Jonathan Moss, baada ya Matic kumkaba shingoni Diafra Sakho katika dakika ya 44.
Wachezaji wa Chelsea pia walimzingira refa baada ya Matic aliyeonyeshwa kadi ya njano awali kupewa kadi nyingine ya njano na kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
“Shtaka lilihusu klabu hizo kushindwa kuwamiliki wachezaji wake juu ya nidhamu uwanjani hapo, hata hivyo baada ya adhabu hiyo klabu zote mbili zimeonywa vikali kurudia makosa hayo,” imesema FA.