22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 3, 2023

Contact us: [email protected]

CHADEMA YATAFUTA USHIRIKIANO KIMATAIFA


Na JANETH MUSHI-ARUSHA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na wanachama wa chama hicho wanaoishi nje ya nchi, wameanza mikakati kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Katika ushirikiano huo, juzi chama hicho kilisaini hati ya ushirikiano baina yake na tawi la Chadema lililopo Mjini Seattle-Washington, Marekani katika ofisi zake za kanda zilizopo jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kabla ya kusaini hati hiyo, Katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema miongoni mwa masuala waliyokubaliana katika hati hiyo ya ushirikiano ni pamoja na kulenga wenzao hao kuwasaidia katika uchaguzi huo pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Alisema kwamba, katika hati hiyo pande hizo mbili zimekubaliana kushirikiana ili kuhakikisha wanaeneza chama hicho, ikiwa ni pamoja na kutengeneza vitu mbalimbali kwa ajili ya kusambaza katika maeneo mbalimbali ili visaidie chama hicho wakati huo wa uchaguzi.

“Tunalenga haya kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Tutatengeneza vitu kama kofia, fulana, kalamu na vitu vingine, wao watatusaidia kuvipata vitu hivi kwa wingi na tutavisambaza maeneo mengi nchini,” alisema.

Golugwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, alisema masuala mengine waliyokubaliana ni kushirikiana kwa kupeana taarifa zinazohusiana na fursa za elimu ikiwamo kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi na kupeana fursa za biashara, masoko, siasa na masuala ya kijamii.

“Tumekubaliana pia kuhamasisha Watanzania wengine wanaoishi nje ya nchi ambao ni wanachama wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuiona Tanzania kama nchi yenye fursa za uwekezaji.

“Chini ya utaratibu huo, watahamasishwa ili waje kuwekeza nchini ikiwa ni pamoja na kushirikiana na halmashauri zilizopo chini ya Chadema ili wafanye uwekezaji ulio na tija utakaozalisha ajira nyingi,” alisema.

Naye kiongozi wa chama hicho kutoka nchini Marekani, Paschal Kikuji, alisema Watanzania waishio nje ya nchi bado wanaikumbuka Tanzania na wanataka kushiriki masuala mbalimbali ya kujenga nchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,270FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles