26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Chadema yaonya wagombea wasaliti

Na YOHANA PAUL, MWANZA

KATIBU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Victoria inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera, Zacharia Obad ametoa onyo kwa wanachama wa chama hicho waliopitishwa kugombea nafasi mbalimbali kutotoa visingizio ili wajitoe kushiriki uchaguzi mkuu, kwani kufanya hivyo ni usaliti.

Alitoa onyo hilo wakati akizungumuza na wanachama waliopitishwa kuwania nafasi za udiwani na ubunge mkoani Mwanza jana.

Alisema hawategemei kuona hujuma ya aina yeyote kutoka kwa watu walioaminiwa na chama hicho,  chama kimefanya uwekezaji mkubwa kuanzia mchakato wa kura za maoni mpaka kuelekea kampeni zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Alisema iwapo mgombea amepitishwa  na wajumbe pamoja na kamati kuu ya chama, yeye mwenyewe kwa hiari yake akakubali kuchukua fomu, basi suala la kurejesha fomu na kushiriki uchaguzi mkuu ni lazima na siyo hiari tena vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa wale watakaofanya hujuma, ikiwamo kutorejesha fomu.

Alisema haiwezekani mgombea apitie michakato yote kuanzia kutia nia, kupokea barua ya uteuzi, kuchukua fomu ya kugombea, kutafuta wadhamini na baadae fomu yake kusainiwa na katibu wa chama kanda harafu,kwa sababu zake tu binafsi asirejeshe fomu na ajitoe kushiriki uchaguzi kwa kuwa huo ni usaliti mkubwa.

Alisema inawezekana  kipindi hiki, baadhi ya wagombea wa Chadema wakafuatwa na vyama vingine na kushawishiwa kujitoa, mchezo ambao haukubaliki na chama na wote wenye mlengo huo,lazima watambue habari za kukichezea chama zimeshafikia kikomo na hawatavumiliwa tena.

Aliliomba jeshi la polisi kuhakikisha linatoa ushirikiano na ulinzi kwa wagombea wote katika kipindi cha kampeni bila kujali itikadi ya vyama vyao.

Alitoa shukrani za chama kwa mahakama zote nchini kuwapa ushirikiano wagombea wote waliohitaji kusainiwa fomu zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles