29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

CHADEMA YAIANDIKIA BARUA MAREKANI, UJERUMANI

Na MWANDISHI WETU


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeziandikia barua Marekani na Ujerumani kuzitaka kuziangalia tuhuma zilizoelekezwa dhidi yao za kukihusisha na chama hicho katika kile kinachodaiwa kuwa ni mipango ya kuhatarisha usalama wa Tanzania.

Barua mbili za Chadema ambazo zimeandikwa Machi mosi mwaka huu na kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari cha chama hicho, Tumaini Makene, zimetaka balozi za nchi hizo nchini kujibu tuhuma hizo ambazo zilielekezwa na Cyprian Musiba aliyejitambulisha kama Mkurugenzi wa Kampuni ya CZI.

Gazeti hili ambalo limefanikiwa kuona barua hizo jana, Chadema kimesema kimeona umuhimu wa kuchukua hatua hiyo ili kupata mwitikio wa nchi hizo juu ya tuhuma hizo nzito ambazo zinatakiwa kuangaliwa zaidi.

Katika barua yenye kumbukumbu No. C/HQ/ADM/KS/24/02  ambayo imeelekezwa kwa John Espinos ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Uchumi, Ubalozi wa Marekani, Chadema imeeleza kwamba Februari 25, mwaka huu mtu aliyejulikana kwa jina la Cyprian Musiba, aliituhumu Marekani kwa kufanya mipango na mikakati mbalimbali ya kuhatarisha usalama wa Taifa la Tanzania.

Barua hiyo ilielezea kwa urefu kwamba Musiba kwa kupitia majukwaa mbalimbali ya kubadilishana taarifa na mawasiliano vikiwamo vipande vya video vilivyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii alisema Marekani inadaiwa kupanga watu au kuendesha mikakati inayohatarisha usalama wa Tanzania.

“Musiba alikwenda mbali zaidi kwa  kutuhumu kuwa nchi yako imekuwa ikishirikiana na Chadema kupanga uhatarishaji wa usalama wa nchi. “Alituhumu FBI (Federal Bureau of Investgation) kuwa inajihusisha na baadhi ya Watanzania katika mipango hiyo.”

Pia barua hiyo ilisema kuwa Musiba alitaka dunia na Afrika yote kutambua uwapo wa hiyo mipango hatari dhidi ya Tanzania ambayo Marekani inahusishwa kwa namna moja au nyingine kufanya mipango hiyo.

“Kutokana na mapenzi na uwajibikaji wetu kwa nchi yetu ya Tanzania na kama taasisi  ikiwa ni sehemu ya wadau kwa maisha yajayo ya nchi yetu pendwa, kwa kuweka mbele masilahi ya nchi na wakazi wake ndani na nje ya nchi, katikati ya kila kitu na kwa kuguswa na tuhuma kama mdau, tunahisi msukumo na kuona umuhimu wa kukuandikia, hivyo tunaweza kupata mwitikio wako kwa tuhuma hizi nzito na tunafikiri kuziangalia zaidi.

“Katika barua hii tumeambatanisha CD zenye vipande vya video vinavyomwonyesha Cyprian Musiba akiviambia vyombo vya habari siku tajwa hapo juu.”

Kwa kupitia hoja kama hizo barua ya pili yenye kumbukumbu No C/HQ/ADM/KS/24/01 ambayo ilielekezwa kwenda kwa Joerg Hererra ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Uchumi cha Ubalozi wa Ujerumani, Chadema ilisema Musiba alikaririwa akikituhumu chama tawala cha nchi hiyo cha Christian Democratic Union (CDU) kushiriki mipango ya kuhatarisha usalama wa Tanzania.

Jumapili iliyopita Musiba alizungumza na baadhi ya waandishi wa habari na kutoa tuhuma nzito kwa nchi hizo mbili huku akitoa orodha ya watu ambao aliwaita ni hatari kwa usalama wa Taifa.

Watu hao ni Mange Kimambi ambaye alimtuhumu kuwa anatumiwa na FBI kuchochea machafuko nchini.

Wengine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Maria Sarungi, Zitto Kabwe, Tundu Lissu, John Heche, John Marwa, Evarist Chahari, Julius Mtatiro pamoja na kikundi cha Janja weed alichodai kinaratibiwa na wafuasi wa CUF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,220FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles