23 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

KIVULI CHA KUNYIMWA KURA MWAKA 2020 CHAMTESA MABULA

Na BENJAMIN MASESE -MWANZA

MBUNGE wa Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula, amewapigia magoti wananchi wa jimbo hilo na kuwaomba  kuachana na mfumo wa kuongozwa na wabunge kwa kipindi cha miaka mitano tu kama ilivyotokea kwa watangulizi wake waliodumu kwa awamu moja.

Akitoa ombi hilo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kishili kwa kuwahoji wananchi waliohudhuria kama wapo tayari kumrudisha bungeni, baadhi yao walikaa kimya huku wengine wakiguna na kucheka, Mabula, alisema ana imani kubwa na CCM kumpitisha tena kutetea nafasi hiyo katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020 kwa sababu kipindi cha miaka mitano hakitoshi kuonyesha mafanikio au kupima uwakilishi wa mbunge katika jimbo.

Mabula alisema hata kama hatarudi bungeni, lakini atakuwa mbunge wa kwanza kutekeleza ahadi zake tofauti na wabunge wengine waliomtangulia.

“Nawaombeni tuachane na historia ya miaka mitano, mnachagua mbunge mwingine, miaka hiyo haitoshi kumtathmini mtu, nirudisheni tena kwa kipindi cha pili mtaona matokeo yake, naamini katika utawala huu wa Rais Dk. John Magufuli, mtapata mafanikio kwa sababu changamoto za umeme, barabara, maji zitapatiwa ufumbuzi,” alisema.

Awali, wenyeviti wa Serikali za Mitaa 11 walisema kilio kikubwa cha wananchi wa Kishili ni migogoro ya ardhi, maji na umeme na kumhoji Mabula sababu ya wataalamu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutokwenda kueleza ukweli.

“Huu umati wa wananchi kujaa hapa uwanjani si kwamba wamekuja wakiwa na furaha, sote tunajua Kishili ndiyo inayoongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi, pia robo tatu ya wakazi wake hawana umeme wala maji, tunashangaa unakuja peke yako sijui unawaeleza nini wananchi,” alisema Mwenyekiti wa Kanindo (Chadema), Ndalawa Masibuka.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kishili B (CCM), Kitambo Bulugu, alisema: “Kitendo tulichofanyiwa na maofisa ardhi wa jiji mwaka 2012 kupima ardhi yetu bila ushirikishwaji hakikuwa sawa, leo hii tunaishi kwa hofu na hatujui hatima yetu, je, kama mwakilishi wetu una msimamo gani.”

Kabla ya Mabula kujibu maswali ya wenyeviti hao, alitoa nafasi kwa wananchi kuuliza maswali na walihoji sakata la ardhi huku wakimtaka kueleza sababu iliyomfanya kukaa kimya wakati wakazi wa Kishili walipojitokeza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kulalamikia suala hilo huku maofisa ardhi wakitoa majibu kwamba hakuna mgogoro wa ardhi.

Mabula alisema alishindwa kusimama mbele ya Majaliwa wakati maofisa ardhi wakitoa taarifa kwamba Kishili hakuna mgogoro kwa sababu yule ni kiongozi wa ngazi za juu hivyo aliona si busara kusutana.

“Sote tunajua yule ni kiongozi wangu wa ngazi ya juu, niliamua kufyata mkia ila ninachowahakikishia ni kwamba kwa kuwa Majaliwa aliagiza wale watu wa jiji waje kuwaelimisha, basi nitawapigania hadi tone la mwisho lakini yapo mambo ya muhimu kama huduma za kijamii lazima tuziache.

“Kwa juhudi zangu nimewasiliana na waziri husika juu ya mpango wa kurasimisha makazi, nimemweleza kuwa Nyamagana haujafika mitaa mingi na ameniongezea miezi sita, hivyo litakoma Juni 30, mwaka huu kwa sababu hiyo maofisa ardhi watakuja kukaa na nyinyi kikubwa ni kutoa ushirikiano,” alisema.

Pia alijitetea kwamba sababu ya kutoonekana mara kwa mara jimboni inatokana na kuwa katika timu ya utafiti iliyoundwa na Magufuli kufuatilia masuala ya changamoto zilizopo kwa lengo la kuzitatua na kukuza uchumi wa Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,305FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles