24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yakumbuka maamuzi magumu ya Lowassa, Rostam aangua kilio

Nora Damian na Esther Mnyika, Monduli

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi ametaja mambo matano watakayomkumbuka waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Lowassa akisema msiba huo ulikuwa ni habari mbaya kwake.

Dk. Nchimbi amesema Lowassa alikuwa mchapakazi, mwenye maamuzi magumu, mzalendo, mnyenyekevu na aliyependa watu wote bila kuwabagua.

Moja ya uamuzi mgumu unaoendelea kukumbukwa ni hatua ya kiongozi huyo aliyoichukua ya kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 na ile ya kujiunga Chadema mwaka 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 16,2024 nyumbani kwa Lowassa Kijiji cha Ngarash wilayani Monduli Mkoa wa Arusha, Dk. Nchimbi aliyetumia dakika mbili na sekunde 56 amesema kifo cha Lowassa ni pigo kubwa kwa nchi.

“Nilihisi kupoteza rafiki, kaka na mlezi lakini pia niliona jinsi ambavyo chama changu kimepoteza mtu. Niliona jinsi ambavyo nchi yetu imepoteza mtu, lakini niliona jinsi ambavyo vyama vingine vilivyokuwa karibu naye vimepoteza mtu muhimu sana kwao…pigo hili nililihisi binafsi na niliona ambavyo linaathiri nchi yetu, ni pigo kubwa sana kwa nchi yetu.

“Lowassa alikuwa Mwanaafrika wa kweli, alikuwa mtu wa maamuzi magumu na alikuwa mchapakazi, watu wanaweza wakapishana katika kila maelezo wanayotoa kuhusu Lowassa lakini hakuna hata mtu mmoja anayeweza kuwa na ujasiri wa kusema alikuwa mvivu au alikuwa hapendi kufanya kazi au hakuwa na mapenzi na nchi yake…alikuwa mchapakazi wa hali ya juu, hakupoteza muda hata mara moja kuacha kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania,” amesema Dk. Nchimbi.

Mfanyabiashara Rostam Aziz (kushoto) akijifuta machozi baada ya kutoka kutoa heshima katika Jeneza la rafiki yake mkubwa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Lowassa, kijijini kwake Ngarash Monduli mkoani Arusha leo Februari 16,2024. Katikati ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Taifa Group, Absalom Kibanda.

Amesema Lowassa alikuwa hachagui marafiki na kwamba wanapaswa kujifunza kupitia kiongozi huyo kwa kuishi maisha ya uadilifu na kuwa kuwa na marafiki wa aina zote na kuwatumikia watu wote bila ubaguzi.

“Alikuwa mnyenyekevu sana, nafasi alizozishika, aina ya marafiki aliokuwa nao, alikuwa na marafiki ambao haangalii nafasi zao, vyeo vyao na hata katika eneo hili tulilopo (nyumbani kwa Lowassa) wako watu wametoka mikoa mbalimbali nchini, watu wa kawaida kabisa ambao walikuwa marafiki wa Lowassa.

“Tunapopewa nafasi za uongozi lazima tuwapende tunaowatumikia hili ndilo jambo muhimu sana la kujifunza kutoka kwa Edward Lowassa.

“Nina ugonjwa wa kupenda watu wachapakazi, watu wa kweli, watu wanaoipenda nchi yao kwa dhati hayo yote ambayo mimi nayapenda Edward alikuwa nayo, haya ni mambo ya pekee ambayo nitamkumbuka.

“Ni mambo ambayo ningependa kuendelea kuyaenzi na kuwashawishi Watanzania wengine wayaenzi lakini mapenzi yake hayakuchagua aina ya itikadi ya mtu yeyote ndio maana alikuwa na marafiki CCM, Chadema, ACT vyama vyote vilikuwa ni marafiki zake,” amesema.

Rostam aangua kilio
Mfanyabiashara Rostam Aziz ameshindwa kujizuia na kuangua kilio baada ya kufika nyumbani kwa Lowassa kutoa pole.

Rostam aliyewasili kijijini Ngarash saa mchana alikwenda kutoa pole kwa familia lakini wakati anatoka alionekana akijifuta machozi.

Rostam ambaye anatajwa kuwa rafiki wa karibu wa kiongozi huyo, mwaka 1995 alikuwa miongoni mwa waliomshawishi Lowassa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kuwania urais. Kikwete na Lowassa walitia nia ya urais lakini walishindwa katika mchakato wa ndani ya chama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles