25.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

CAG: Deni Muhimbili halilipiki

AGATHA CHARLES

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2017/18, imeeleza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ina ongezeko la makisio ya madeni yasiyotarajiwa kulipwa (bad debts) ambayo yalifikia hadi Sh bilioni 1.44 kufikia Juni 30, 2018.

Katika sura ya saba ya ripoti hiyo ya ukaguzi wa mahesabu ya Serikali ambayo CAG, Profesa Mussa Assad aliitoa hivi karibuni, imeeleza kiwango hicho kiliongozeka kutoka Sh milioni 941.32 zilizokuwapo mwaka uliopita.

“Pamoja na juhudi na hatua madhubuti zilizochukuliwa na hospitali kukusanya madai kutoka kwa wateja mbalimbali, nilibaini kuongezeka kwa madeni yasiyotarajiwa kulipwa (bad debts) mpaka kufikia Sh bilioni 1.44 katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2018 kutoka Sh milioni 941.32 zilizokuwapo mwaka uliopita,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Kutokana na hilo, CAG katika ripoti hiyo alipendekeza kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ichukue hatua ambazo zitahamasisha taasisi za Serikali kujiunga na bima mbalimbali za afya zilizopo.

Pamoja na hilo, CAG alieleza katika ripoti hiyo kuwa, Hospitali ya Muhimbili kupitia Idara ya Rediolojia imeshindwa kuitumia vizuri programu ya Jeeva, iliyonunuliwa mwaka 2005 ili kuongeza ufanisi katika mchakato wa shughuli za kutunza taarifa za kitabibu.

Alieleza katika ripoti hiyo kuwa pamoja na Jeeva kuwa na machaguo ya kuweka maelezo ya kitabibu, alibaini kuwa madaktari hawajazi maelezo kwenye programu.

“Hali inayosababisha Idara ya Rediolojia kuendelea kutumia karatasi kuandika maelezo ya kitabibu pamoja na kufundishwa jinsi ya kutumia mfumo huo.

Napendekeza kuwa MNH ihakikishe programu husika inatumika kwa ukamilifu na watumiaji wote waliokusudiwa katika idara za watumiaji,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.

Katika ripoti hiyo, CAG alibaini pia udhibiti dhaifu katika chakula wanachopatiwa wanafunzi na wagonjwa waliolazwa.

Alisema alibaini hakukuwapo mgawanyo wa kazi katika kusimamia mkataba wa kutoa chakula kwa wanafunzi na wagonjwa waliolazwa, pamoja na bili kazi ambayo aliifanya mtu mmoja.

“Udhibiti wa gharama za ugavi wa chakula unaweza kuwa mgumu kwa kukosa mgawanyo wa majukumu katika kuhakikisha vyakula na kuidhinisha bili. Hivyo napendekeza MNH iboreshe udhibiti kwa kufanya uangalizi wa ndani kwa ufanisi zaidi,” alieleza CAG.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles