27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Gawio la Mlimani City -UDSM la Sh milioni 44 lamshtua CAG

AGATHA CHARLES

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameeleza katika ripoti yake kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hakitimizi majukumu yake ya kimkataba ya kupitia viwango vya tozo vinavyotokana na upangaji vinavyowasilishwa kwao na Kampuni ya Mlimani Holding Ltd (MHL).

Katika sura ya tano ya ripoti hiyo sehemu inayohusu usimamizi wa mapato katika taasisi za umma, CAG alibainisha UDSM hakijatimiza wajibu huo wa kusimamia mapato ya matangazo, kumbi na maegesho kutoka kwa kampuni ya MHL katika kipindi cha mwaka huo wa fedha.

“Kwa kipindi cha mwaka ulioishia Juni 30, 2018 imebainika UDSM hakitimizi majukumu yake ya kimkataba kwa kushindwa kupitia viwango vya tozo; hivyo kutegemea taarifa zitolewazo na Kampuni ya MHL.”

Taarifa hiyo ilieleza kuwa jumla ya kiasi cha Dola za Kimarekani 10,869.90 (sawa na Sh 25,163,265.68 ) na dola 8,204.73 (sawa na Sh 18,992,865.24) ambazo jumla ni sawa na Sh 44,156,130.921ziliwasilishwa UDSM kama kiwango cha gawio la mwaka kutokana na mgawanyo wa hisa katika mapato ya eneo la matangazo na maegesho ya magari, mtawaliwa.

“Hata hivyo, nimethibitisha kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakijafanya uhakiki wowote kujiridhisha na usahihi wa hesabu za mapato hayo,” alieleza CAG katika ripoti hiyo.

Pamoja na hilo, CAG alibainisha kuwa UDSM hakina idadi kamili ya vikao na makongamano yaliyofanyika ndani ya ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, hivyo kutokujua kiwango halisi cha mapato yaliyopatikana kutokana na kukodishwa ukumbi huo.

“Kutokana na kushindwa kumsimamia mpangaji, ni dhahiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakiwezi kuthibitisha thamani halisi ya hisa zilizopo na kiwango cha gawio kinachostahili kulipwa,” alieleza CAG.

Alipendekeza kuwa, Menejimenti ya chuo hicho ifanye ufuatiliaji wa karibu na wa mara kwa mara, ikiwamo ukaguzi wa vitabu, ili Chuo kiweze kupata stahiki zake kwa usahihi kutoka kwenye mradi wa Mlimani City.

Mgongano wa kimaslahi

CAG alieleza katika ukaguzi wake alibaini kuwa Kampuni ya BICO ambayo ni ya Uhandisi Ushauri iliyosajiliwa na Bodi ya Usajili ya Wahandisi, ikiwa na namba ya usajili 035 kwa kazi za uhandisi mshauri kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Meneja wake alikuwa na mgongano wa kimaslahi na Wamiliki wa Kampuni ya Uhandishi Ushauri iliyopewa Kazi (sub contracted).

Alieleza kuwa Desemba 9, 2013, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) liliingia mkataba na BICO kutekeleza mkataba wa gharama ya Sh bilioni 2.60.

CAG alieleza kuwa Oktoba 20, 2016, BICO na NHC walisaini mkataba wa nyongeza kwa kazi zilizoongezeka zenye gharama ya Sh bilioni 1.79 (50%) ukiondoa kodi za ndani na huduma zitolewazo na watu wengine kwa gharama ya Sh milioni 100 na kufanya jumla ya gharama za mkataba kuwa Sh bilioni 5.49.

“Hata hivyo, nilibaini kuwa wakati mchakato wa manunuzi ukiendelea, BICO na kampuni binafsi ya uhandisi ushauri zilisaini mkataba mdogo Agosti 27, 2013 ikiwa ni sehemu ya mkataba mkuu uliotajwa hapo juu wa kuchangia mapato yatokanayo na ushauri kwa kuzingatia uwiano wa utaalamu wa watumishi,” ilieleza sehemu ya ripoti.

CAG alieleza kuwa BICO iliwakilishwa na watu wawili, mmoja akiwa na nguvu ya kisheria (power of artorney), na wakati huo huo akiwa ni kiongozi wa majadiliano; na mwingine akiwa ni mtaalamu.

Alieleza kuwa katika kufuatilia umiliki wa kampuni iliyoingia mkataba mdogo wa mhandisi mshauri, ilibainika kuwa wawakilishi wa kampuni ya BICO walikuwa wamiliki wa kampuni hiyo binafsi.

“Ambapo, mwakilishi mtaalamu alimiliki hisa asilimia 40, wakati mwakilishi kiongozi wa majadiliano alimiliki hisa kwa asilimia 20. Hili lilifanyika makusudi ili kiasi kikubwa cha mapato kiende kwa kampuni binafsi ambayo inamilikiwa na wawakilishi hao wa BICO; hivyo BICO kama taasisi ya Umma ifaidike na mapato ya 156 kiasi cha asilimia 24.4 tu,” ilieleza sehemu hiyo ya taarifa.

Ripoti ilieleza kuwa, wawakilishi hao wa BICO waliitumia BICO kama kampuni iliyo mstari wa mbele ili kukwepa kodi za serikali kama kodi ya zuio kwa kuwa malipo yalitoka NHC kwenda BICO.

“Kutokana na makubaliano yaliyosainiwa, BICO ilikuwa na haki ya asilimia 24.4 tu ya jumla yote ya mkataba. Kiasi kilichobaki (cha asilimia 75.6) kilikuwa haki ya kampuni binafsi ambayo ni ya wawakilishi wa BICO.

Kuhusiana na mgongano wa kimaslahi, mtaalamu kutoka BICO alipokea kiasi cha Dola za Kimarekani 340,000 kama ada za kitaaluma katika mkataba mdogo wa mhandisi mshauri na si kama mtaalamu kutoka BICO,” alieleza CAG.

Kutokana na hilo, CAG alipendekeza Chuo cha Dar es Salaam kihusishe vyombo vya kusimamia sheria kufanya uchunguzi zaidi na hatua stahiki zichukuliwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles