21.9 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

CAG aibua udhaifu kila kona

MAREGESI PAUL -DODOMA

SINTOFAHAMU juu ya kuwasilishwa ama kutowasilishwa bungeni kwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imemalizika baada ya kuwasilishwa bungeni jana, huku ikionyesha udhaifu katika maeneo luluki.

 Hata hivyo, tofauti na miaka ya nyuma, ripoti hiyo iliwasilishwa bungeni bila CAG kuwepo ndani ya ukumbi wa Bunge kama ambavyo imezoeleka.

Kwa kawaida, wakati ripoti hiyo ikiwasilishwa bungeni na waziri mwenye dhamana, CAG huwa ndani ya ukumbi wa Bunge eneo la wageni wa Spika na baada ya kuwasilishwa, yeye pamoja na viongozi na wabunge wa kamati za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), huzungumza na waandishi wa habari juu ya kilichobainika katika ripoti hiyo.

Lakini jana, CAG Profesa Mussa Assad na timu yake walizungumza na waandishi wa habari katika ofisi zao jijini hapa huku hukiwa hakuna wawakilishi wa PAC wala LAAC.

Akizungumzia hali hiyo ambayo imetokana na Bunge kupitisha azimio la kutofanya naye kazi, alisema aliamua kufanyia mkutano huo ofisini kwake baada ya kuhisi kwamba wasingekaribishwa katika majengo ya Bunge.

Pia alisema walitoa mwaliko kwa PAC na LAAC, lakini alishangaa kwamba hawakufika na kwamba watahakikisha wanawapatia ripoti hiyo.

 Akizungumzia ripoti yake ya ukaguzi katika mwaka wa fedha 2017/18, Profesa Assad alieleza jinsi baadhi ya mapendekezo ya ripoti zake za kikaguzi yasivyofanyiwa kazi na mamlaka husika ili kunusuru upotevu wa fedha za umma.

Akizungumzia matokeo ya ukaguzi maalumu, Profesa Assad alisema ofisi yake ilifanya ukaguzi huo katika Shirika la Bima la Taifa (NHIF) na kugundua jinsi fedha za umma zilivyotumika vibaya.

“Shirika hilo liliingia mkataba wa kununua mfumo wa kidijitali uitwao ‘Genisys’ Juni 18, mwaka 2012 kwa ajili ya kuunganisha kazi kuu tatu za mfuko huo ambazo ni bima ya maisha, bima zisizo za maisha pamoja na uhasibu.

“Katika eneo hilo, mfuko ulikubali na kupokea mfumo huo na kulipa Dola za Marekani milioni 3.59. Hata hivyo, ukaguzi wangu umebaini kuwa mfumo huo haufanyi kazi kikamilifu na kulifanya shirika kutumia mfumo mwingine uitwao ‘Unisys’.

“Kutokana na changamoto hizo, thamani ya fedha zilizotumika kununua mfumo huo haijaweza kupatikana kwani malengo yaliyotakiwa hayakufikiwa.

“Pia katika kufanya uchunguzi wa vitabu vya fedha, taarifa za benki na hati za malipo za mfuko huo, nilibaini kuwapo kwa malipo ya Sh bilioni 3 na kati ya malipo hayo, Sh bilioni 2.61 yalikuwa malipo hewa, Sh milioni 350.87 yalikuwa ni malipo ambayo walipwaji walishindwa kubainika na Sh milioni 42.6 hazikuweza kuthibitika kupokewa na walipwaji.

“Malipo hayo yalitakiwa kulipwa watoa huduma za afya kwa kutumia hundi zilizofungwa, lakini yalifanywa kwa fedha tasilimu kinyume na kanuni za fedha za mfuko huo,” alisema Profesa Assad.

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

Akizungumzia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Profesa Assad alisema ofisi yake katika ukaguzi huo ilibaini kuwa ilinunua mashine za BVR 8,000 kwa ajili ya usajili wa wapigakura na kati ya hizo, 5,000 hazikukidhi vigezo vilivyoainishwa katika mkataba.

Kwa mujibu wa CAG, mashine hizo hazikufanana kimatumizi na mashine zilizonunuliwa awali na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na Wakala wa Taifa wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

“Kutorandana huku kumeisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 862.08 zilizotumiwa na NIDA kununulia leseni mpya za ‘windows’ na ‘biometric algorithms’ ili kubadilisha mashine hizo 5,000 zilizopokelewa kutoka NEC ili ziweze kufanya kazi na mfumo wa BVR na NIDA.

“Aidha, nilibaini kwamba mzabauni alilipwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 72.30 badala ya Dola za Marekani 72.15 ambazo zilikuwa kwenye mkataba.

“Pia mafunzo kwa maofisa 15 wa Tehama wa tume hiyo ya taifa ya uchaguzi hayakufanyika licha ya mzabuni kulipwa Dola za Marekani 358,650 kwa ajili ya mafunzo hayo,” alisema CAG.

POLISI

Kuhusu Jeshi la Polisi, Profesa Assad alisema ukaguzi uliofanywa na ofisi yake katika mwaka huo wa fedha uligusia ununuzi wa mfumo wa utambuzi wa alama za vidole uitwao AFIS.

“Ukaguzi maalumu wa mfumo wa utambuzi wa alama za vidole ulibaini kwamba mahitaji ya kitaalamu kutoka idara inayotumia mfumo huo, hayakuzingatiwa wakati wa kutathmini na kutoa zabuni.

“Na pia tulibaini kwamba Jeshi la Polisi lilishindwa kuthibitisha malipo ya Sh bilioni 3.30 yaliyolipwa kwa mzabuni aliyetoa huduma za matengenezo na msaada wa kitaalamu wa AFIS katika mikoa ya kipolisi ya Temeke, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Kigoma, Geita na Kinondoni.

“Pia tulibaini kwamba vifaa vya utambuzi wa alama za vidole vyenye thamani ya Sh bilioni 1.73, havikufungwa kwenye magereza 35 yaliyoainishwa na badala yake vilihifadhiwa katika ofisi ya upelelezi, makao ya Jeshi la Polisi.

“Pamoja na hayo, ukaguzi wetu ulibaini kwamba malipo ya Sh milioni 604.39 kwa ajili ya mafunzo kwa wataalamu 30 hayakufanyika.

“Kwa ujumla ni kwamba Jeshi la Polisi lilishindwa kuonyesha timu yangu ya ukaguzi mahali zilipokuwa monita 58 za kompyuta aina ya Dell zenye thamani ya Sh milioni 159.16 zilizopelekwa kwenye kitengo cha uchunguzi wa kisayansi cha makao makuu ya Jeshi la Polisi kiitwacho Forensic Unit.

“Pamoja na hayo, monita 213 za kompyuta aina ya Dell zililipwa Sh milioni 195.22 kwa mzabuni Lugumi Enterprises Limited, lakini mzabuni hakuzileta,” alisema Profesa Assad.

UNUNUZI WA SARE ZA POLISI

Katika ukaguzi huo maalumu, Profesa Assad alisema ofisi yake ilibaini Jeshi la Polisi lililipa Sh bilioni 16.66 bila kuwapo ushahidi wa uagizaji na upokeaji wa sare za askari polisi kwa boharia mkuu wa jeshi hilo.

“Pia nilibaini kwamba maoni ya kisheria ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanayohusu uwasilishaji wa kiapo cha nguvu ya kisheria na leseni halali ya biashara, hayakuzingatiwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wa kusaini mkataba namba ME.014/PF/2015/2016/G/30 Lot 2 uliohusu ununuzi wa sare za askari polisi,” alisema Profesa Assad.     

UWANJA WA NDEGE SONGWE

Akizungumzia ukaguzi maalumu wa uwanja wa ndege wa Songwe, Profesa Assad alisema ukaguzi wake ulionesha jinsi malipo ya Sh bilioni 1.43 yalivyofanyika mara mbili kwa udanganyifu kupitia maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).

Kwa mujibu wa Profesa Assad, jumla ya Sh bilioni 1.95 zililipwa bila kuwapo kwa jedwali la vipimo na hati za madai zilizoidhinishwa na mhandisi mshauri.

“Yaani, kati ya malipo ya awali ya Sh bilioni 1.70 alizolipwa mkandarasi kwa ajili ya kuanza shughuli za ujenzi, ni Sh milioni 176.56 tu ndizo zilizorejeshwa hadi ukaguzi huu unafanyika.

“Pia jumla ya Sh milioni 570.50 zililipwa zikiwa ni zaidi ya gharama zilizoidhinishwa na mhandisi mshauri na jumla ya Sh bilioni 5.48 zililipwa kwa mkandarasi bila kuidhinishwa na mhandisi mshauri,” alisema.

Pamoja na hayo, Profesa Assad alishauri Serikali ichukue hatua dhidi ya waliosababisha ubadhirifu huo wa fedha ili liwe fundisho kwa wengine.   

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,717FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles